2015-05-30 16:53:00

Msikumbatie utamaduni wa kifo, kwa kudharau utu na heshima ya binadamu!


Kardinali Angelo Bagnasco, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, Ijumaa tarehe 29 Mei 2015 ametoa hotuba ya ufunguzi kwa Chama cha Sayansi na Maisha, kinachoadhimisha kumbu kumbu ya miaka 10 tangu kilipoanzishwa nchini Italia. Mkutano huu umeongozwa na kauli mbiu: “Sayansi ipi na kwa ajili ya maisha gani?” Katika hotuba yake, Kardinali Bagnasco anasema maisha ni msingi wa mafao ya wengi; changamoto za maisha zinapaswa kushughulikiwa kwa kuzingatia kanuni ya ukweli na haki; umuhimu wa kujenga na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia na kwamba, sayansi haina budi kuongozwa na mwanga wa imani.

Kardinali Bagnasco anabainisha kwamba, maisha ya binadamu ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu yanapaswa kulindwa, kutetewa na kuendelezwa tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake, hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mapenzi ya Mungu. Jamii isimame kidete kushuhudia na kutangaza uzuri wa ndoa na maisha ya familia yanayojikita katika upendo wa dhati kati ya bwana na bibi na wala si vinginevyo. Sayansi haina budi kufanya majadiliano ya kina na imani.

Kardinali Bagnasco anasikitika kusema kwamba, leo hii binadamu anapigwa danadana kama mpira kwa kukumbatia nadharia ambazo ni kinyume kabisa cha ukweli kuhusu: heshima, utu na maisha ya binadamu, kwa madai ya uhuru wa binadamu anayejitafuta mwenyewe na kusahau utakatifu wa maisha, unaopata chimbuko lake kutoka kwa Mwenyezi Mungu na hivyo inapaswa kuheshimiwa. Hii ni changamoto kwa wanachama wa Chama cha Sayansi na Maisha kuendelea kukabiliana na changamoto zote hizi katika misingi ya ukweli na haki, kwani leo hii maisha ya mwanadamu yako hatarini sana.

Majadiliano kuhusu usawa wa kijinsia, yasiwe ni kigezo cha kubeza ndoa na maiafa ya familia yanayojengwa kati ya bwana na bibi kadiri ya mpango wa Mungu na wala si kwa tamaa na vionjo vya binadamu. Tunu msingi za maisha ya ndoa na familia zinapaswa kulindwa na kudumishwa kwani ni kwa ajili ya mafao ya wengi. Familia ni taasisi ambayo haina mbadala na kwamba, familia inapaswa kuwa ni kiini cha majadiliano ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Wakristo pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, watoke kifua mbele kutangnaza na kushuhudia Injili ya Familia inayojengwa katika mahusiano ya bwana na bibi na matunda ya muungano huu wa upendo ni watoto ambao ni zawadi kutoka kwa Mungu.

Kardinali Angelo Bagnasco anabainisha kwamba, Chama cha Sayansi na Maisha nchini Italia kilianzishwa kunako mwaka 2005 wakati ambapo Bunge la Serikali ya Italia lilipoamua kuitisha kura ya maoni kuhusu Sheria namba 40 inayoruhusu utoaji mimba kwa msaada wa wahudumu katika sekta ya afya. Chama hiki kikaanzishwa ili kusimama kidete kutetea Injili ya Uhai tangu pale mtoto anapotungwa mimba hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mapenzi ya Mungu. Injili ya Uhai ni kiini cha haki msingi za binadamu na demokrasia ya kweli. Sayansi inaposhindwa kutetea uhai wa binadamu madhara yake yanamwelemea mtu mwenyewe na jamii inayomzunguka.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.