2015-05-30 15:34:00

Jitahidini kumwilisha huruma na upendo wa Mungu katika maisha yenu!


Mpendwa msikilizaji wa kipindi hekimishi cha Hazina yetu, Tumsifu Yesu Kristo. Karibu mpendwa tuendelee kumtegea sikio Mama Kanisa, mwalimu anayetufundisha kweli za maisha, kweli za kiimani zinazoweza kutusaidia tutembee salama katika hija hii ya hapa duniani. Maisha (hata kama yakawa ni ya siku chache), ni safari ndefu ambayo twaipita katika njia ndefu yenye kona nyingi, kona kali, mabonde, milima mikali na wakati mwingine utelezi mwingi na hatarishi.

 

Hayo yote hujitokeza katika namna mbalimbali za maisha yetu ya kila siku. Kwetu sisi tunaomsadiki Kristo na watu wote wenye kumpenda Mama Kanisa, tutasafiri na kufika salama endapo tu, tupo tayari kuongozwa na Mama Kanisa, aliye kweli Mama na Mwalimu kwa watu wote na wa nyakati zote.

Kwa wakati huu mpendwa msikilizaji, Mama yetu na Mwalimu wetu, yaani Mama Kanisa, kwa mwangwi wa waraka wa Kichungaji wa Baba Mtakatifu Francisko, maarufu kwa jina la Misericordiae vultus, yaani uso wa huruma; anaendelea kutuhekimisha juu ya uzuri na thamani ya huruma ya Mungu katika maisha yetu ya kila siku. Ni mwito kwetu sote ambao tunaonjeshwa huruma ya Mungu katika mapito yetu ya kila siku, tutoke kifua mbele kwa ujasiri makini, tuwaendee watu wote kuwaonjesha huruma, wema na upendo wa Mungu. Tuimwilishe huruma ya Mungu katika maisha yetu ya kila siku.

Tukijigongagonga vichwa na kujifukuafukua dhamiri zetu, kila mmoja wetu, na kila mtu kwa namna yake, tutakumbuka kwamba ipo siku Mungu alituonjesha huruma ya ajabu tena huruma yake kubwa sana; alitufanyia fadhili. Hakika huruma ya Mungu kwetu, imekuwa mwavuli wakati wa mvua kali ya maisha, imekuwa kivuli wakati wa jua kali la maisha, imekuwa nuru wakati wa giza nene la maisha, imekua upepo mwanana wakati wa joto kali la maisha, imekuwa faraja na amani wakati wa mitikisiko mikali ya maisha, imekuwa tumaini jema wakati wa mashaka mazito ya maisha. Huruma ya Mungu, ndiyo wimbo wangu, nitaiimba milele. Hayo ni maneno ya mshairi fulani.

Mshairi anaendelea kusema, Sote tunafunikwa kwa huruma ya Mungu, tunahifadhiliwa, na kulindwa kwa huruma ya Mungu. Ni kweli! Kumbuka, kuna siku uliwahi kumwasi Mungu kwa kuishi maisha ya kishetani kabisa, lakini Bwana hakukuangamiza. Kwa maana huruma yake ni ya milele. Kuna siku ulifanya dhambi chafu na za aibu sana, lakini Bwana hakukuaibisha, alikuhifadhi, kwa maana huruma yake ni ya milele.

Kuna siku uliharibu amani ya watu kwa kusema uwongo mzit-hatarishi, tena uwongo angamizi ukuwachonganisha na wengine ukawaharibia maisha yao, lakini Bwana hakukuumbua, kwa maana huruma yake ni ya milele. Kuna siku uliharibu kazi na watu wengi wakaumizwa sana, lakini hukufukuzwa kazi, Bwana alikutetea, kwa maana huruma yake ni ya milele. . Kuna siku pia ulisingiziwa jambo baya sana ambalo ulipaswa uangamizwe; kakini Bwana alikuwa upande wako akakukingia kifua, kwa maana huruma yake ni ya milele.. Kuna siku uliabudu miungu wawili; mchana ulimtamka Mungu na usiku ulimwabudu shetani; lakini Bwana aliendelea kukuita ‘mwanangu’! kwa maana huruma yake ni ya milele. Kuna siku ndugu yangu ulipatwa na ajali mbaya sana, lakini Bwana alikuinua hai, sio kwa sababu wewe ni mwema kuliko wengine bali kwa maana huruma yake ni ya milele.

Mshairi anasisitiza; hakika huruma ya Mungu iheshimiwe milele. Mimi na wewe ebu tufikirie milima ya dhambi na vifusi vya ukorofi, na uvundo wa fujo tunaokuwa nao rohoni, lakini Mungu anatuvumilia, anatuhurumia, tunaendelea kutembea kwa maringo mtaani. Kwa nini? Ni kwa sababu tu, huruma yake kwetu sisi ni kuu, na huruma yake ni ya milele. Sasa, kama Mungu anakuhurumia katika hayo yote ambayo umeyabeba moyoni, kwa nini wewe unawaaibisha wenzako?

Mshairi anahoji! Kwa nini wewe mdomo wako umekuwa mjasiri sana katika kutangaza mapungufu ya wenzako? Na kwa nini akili yako imekuwa pekuzi sana kutafutatafuta makosa na dhambi za wenzako, ili uzianike hadharani? Wewe sio mkamilifu, ni huruma ya Mungu tu imekuhifadhi, ndiyo maana hadi leo hujakamatwa. Huruma ya Mungu inakulinda.

Aheri kutumia muda mwingi kuishukuru huruma ya Mungu kwa kuishi katika unyenyekevu na kuendelea kuomba huruma ya Mungu kwa ajili yako mwenyewe na kwa ajili ya wengine pia. Badala ya kuwasemasema wengine ambao wewe unafikiri ni wadhambi sana, aheri uwaombee tu. Na huo ndio msaada mkubwa, na ni namna bora ya kuwaonjesha wengine huruma ya Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko ndani ya Misericordiae Vultus, anatuasa, kuishinda hasira, chuki, kinyongo na kisasi kwa njia ya kuhurumia na kusamehe. Hiyo ndiyo roho aliyokua nayo Yule Baba mwenye huruma, katika hadidhi ya ‘mwana mpotevu’. Mara nyingi tunajisahau na kuwaka hasira yenye sumu ya uuaji dhidi ya wale wanaofanya makosa, badala ya kuwahurumia na kuwainua. Kumbatio na busu la Baba mwenye huruma, lilimponya na kumwinua sana Yule mwana mpotevu kuliko litania ya maneno ya kuomba msamaha aliyoiandaa. Kusamehe inawezekana! Ukiamua, ukitaka, ukipenda kusamehe sio kugumu. Wengi hatupendi na hatujaamua tu.

Watu wamekasirikiana miaka nenda, miaka rudi, hawasalimiani wala kutazamana usoni. Mshairi anahoji: Ni nini kisichosameheka hicho? Hasira inaharibu afya ya akili, afya ya mwili na ya roho pia. Hasira pia inapunguza nguvu ya kufikiri. Hasira inafukuza marafiki, na badala yake inakaribisha wanafiki. Ukiwa na hasira daima, utazungukwa na wanafiki na waoga wengi, na utakosa marafiki wa kweli.

Tunapoitafakari huruma ya Mungu, Baba Mtakatifu Francisko ndani ya Misericordiae vultus yaani uso wa huruma, anatualika kuyatafakari sana mausia ya Mtume Paulo asemapo “Usiache jua likazama, ukiwa umebaki na hasira” (Ef. 4:27). Na mstari unaofuata Mtume Paulo anaongeza “msimpe shetani nafasi”. (Ef. 4:27). Kwa mwangwi wa mafundisho ya Mtume Paulo, ni wazi kwamba wengi wetu tunajaribiwa sana wakati tukiwa na hasira. Kwa nafsi inayojaa mchemko mkali wa hasira, ni ngumu kabisa kupata utulivu wa nafsi, na ni ngumu kutawala kichwa. Na badala yake, shetani anaingia kupitia hasira hiyo, kichwa kinayeyuka, na hatimaye mtu anatenda mambo ya ajabuajabu hata ya kujidhuru mwenyewe. Mtu mwenye hasira asiyejua kusamehe, huwa haoni gharama kujiangamiza yeye mwenyewe kwa matendo yake ya harakaharaka.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kumtafakari Yesu aliyeweka huruma kuwa kama kioo cha maisha adilifu na pia kama kigezo cha unadhifu wa imani yetu. Bwana anasema “ Heri wenye huruma, kwa maana hao watahurumiwa” (Mt. 5:7). Baba Mtakatifu anakaza kusema, hii ndiyo heri ambayo kwa namna ya pekee tunapaswa kuitafakari kwa kina katika Mwaka huu Mtakatifu wa huruma ya Mungu.

Kama tuonavyo katika Maandiko Matakatifu, huruma ni neno-msingi linaloonesha kazi ya Mungu kwetu sisi wanadamu. Mungu haishii tu kuonesha upendo wake, bali kwa njia ya huruma anaufanya upendo huo uonekane na ugusike. Zaidi ya hayo, anasema Baba Mtakatifu, upendo hauwezi kuwa tu wa kinadharia. Kwa asili yake, upendo unaonesha kitu fulani kinachogusika: katika nia, mielekeo na tabia ambazo zinaoneshwa katika maisha ya kila siku.

Huruma ya Mungu ni upendo wake wenye kujali kwa kila mmoja wetu. Mungu wetu,  anajisikia kuwajibika, yaani anatutakia mema na anataka kutuona sisi tunafurahi, tumejaa furaha tele na amani.

Ndani ya Misericordiae vultus, anaendelea kusema Baba Mtakatifu, hayo ndiyo mapito ambapo upendo wenye huruma wa Wakristo unapaswa kuwa. Kama vile Baba alivyo na upendo, ndivyo na watoto pia wanapaswa kuwa na upendo. Jinsi Baba alivyo na huruma; ndivyo nasi pia tunavyoitwa kuwa, kwa kila mmoja wetu. Asante kwa kuisikiliza Radio Vatican. Mpendwa Msikilizaji, usisahau dawa kiboko ya magonjwa ya hasira na chuki. Dawa gani hiyo? Baba Mtakatifu ametupatia: yaani,  Kusali Rozali ya Huruma ya Mungu, ili Mungu atuhurumie sisi na dunia nzima; kwa kuwa huruma yake yadumu milele.

Kutoka katika Studio za Radio Vatican, ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.