2015-05-29 08:36:00

Papa Francisko: Onesheni upendo na huruma kwa wahamiaji; dumisheni ndoa!


Wakimbizi na wahamiaji wahudumiwe kwa huruma na upendo; Jamii isimame kidete kupambana na biashara pamoja na matumizi haramu ya dawa za kulevya; Kanisa liendelee kujikita katika kutangaza Injili ya Familia ili kukabiliana na changamoto za kitamaduni; Wakleri wafundwe barabara na kulindwa dhidi ya Mbwamwitu, bila kusahau utunzaji bora wa mazingira.

Haya ni mambo msingi ambayo yametiliwa mkazo na Baba Mtakatifu Francisko alipokutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Jamhuri ya Watu wa Dominican, Alhamisi, 28 Mei 2015 wakati huu wanapoendelea na hija ya kitume inayofanyika walau kila baada ya miaka mitano hapa mjini Vatican. Salam za Maaskofu hao kwa Baba Mtakatifu Francisko zimetolewa na Askofu Gregorio Nicanor Pena Rodriguez, Rais wa Baraza la Maaskofu wa Jamhuri ya Watu wa Dominican.

Baba Mtakatifu Francisko kwa namna ya pekee, anawaalika viongozi wa Kanisa nchini Jamhuri ya Watu wa Dominican kuwasaidia na kuwahudumia wahamiaji na wakimbizi kwa moro wa huruma, upendo na mshikamano wa kidugu. Hawa ni wakimbizi na wahamiaji wanaotoka katika Visiwa vya Haiti, wanaotafuta maisha bora. Viongozi wa Kanisa waendelee kufanya kazi bega kwa bega na Serikali ili kupata suluhu inayojikita katika mshikamano kwa wale ambao hawana nyaraka wala vibali vya kuishi nchini humo au wamenyimwa haki zao msingi.

Maaskofu wajitahidi kukuza mchakato wa udugu na amani kati yao na Maaskofu wa Haiti. Wakimbizi na wahamiaji washirikishwe kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza Maaskofu wote ambao hadi sasa wamekuwa mstari mbele kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji nchini Jamhuri ya Watu wa Dominican, kwani hawa ndio wale ambao Yesu mwenyewe alijitambulisha pamoja nao.

Baba Mtakatifu anawataka Maaskofu kusimama kidete kupambana na biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya kwani hizi ni kati ya changamoto kubwa zinazowaandama wananchi wao, bila kusahau biashara haramu ya binadamu; rushwa na ufisadi; kipigo kwa wanawake majumbani; unyanyasaji na utumikishaji wa watoto wadogo pamoja na ukosefu wa usalama wa kijamii. Hapa Maaskofu wakumbuke kwamba, Kanisa linajikita katika mchakato wa Uinjilishaji mpya unaokwenda sanjari na ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Baba Mtakatifu anakiri kwamba, ndoa na familia ni kati ya changamotokubwa katika ulimwengu mamboleo. Hii inatokana na ukweli kwamba, kuna kasi kubwa ya kumong’onyoka kwa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, changamoto kwa Wakristo kutangaza na kushuhudia uzuri wa ndoa ya Kikristo kwani ni kielelezo cha neema ya Mungu. Familia ni mahali ambapo watu wanajifunza kuishi hata katika utofauti wao pamoja na kuonjeshana upendo na msamaha. Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, uwe ni muda uliokubalika wa kuhamasisha na kuimarisha maisha ya ndoa na familia; upatanisho wa kifamilia, amani na utulivu na maridhiano.

Baba Mtakatifu Francisko kwa namna ya pekee anawaalika Maaskofu kuwalinda Mapadre wao dhidi ya mashambulizi ya “Mbwamwitu” wanaoendelea kuwashambulia hata Wakleri. Seminari iwe ni mahali pa kujikita katika malezi ya kiutu, kiakili na kiroho ili kuwawezesha Majandokasisi kukutana na Yesu Kristo katika hija ya maisha yao, tayari kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake kwa kukumbatia na kumwilisha useja n aumoja katika utekelezaji wa shughuli za kichungaji.

Baba Mtakatifu anawapongeza Wakleri kutoka Jamhuri ya Watu wa Dominican kwa uaminifu na ushuhuda wa maisha ya Kikristo, sanjari na kuwahudumia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, dhamana inayotekelezwa kwa kuzingatia sera na mikakati iliyobainishwa na Maaskofu wa Amerika ya Kusini, katika hati yao maarufu ya Aparecida. Makanisa mahalia yajenge umoja na mshikamano na kwamba, wawe pia ni mashuhuda wa mikakati hii katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku.

Baba Mtakatifu anawataka Maaskofu kuhakikisha kwamba, wanajielekeza zaidi katika kuwajengea uwezo waamini walei katika maisha ya kiroho yanayojikita kwenye mafundisho tanzu ya Kanisa, tayari kujitosa kimaso maso kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wenye mashiko na mvuto. Waendelee kutoa elimu shuleni ili kuwasaidia vijana wa kizazi kipya kufahamu tunu msingi za maisha ya Kikristo, kiroho na kiutu. Kanisa liendelee kuwasaidia watu kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira, kwa ajili ya maendeleo ya sas ana yale ya kizazi kijacho.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.