2015-05-29 08:59:00

Mwenyeheri mtarajiwa Louis-Edouard Cestac alijisadaka kwa ajili ya maskini


Kardinali Angelo Amato kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 31 Mei 2015 anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumtangaza Mtumishi wa Mungu Louis-Edouard Cestac kuwa Mwenyeheri. Ibada hii itafanyika Jimboni Bayonne, nchini Ufaransa. Mwenyeheri mtarajiwa Cestac  alikuwa ni Padre wa Jimbo na mwanzilishi wa Shirika la Watawa Watumishi wa Maria kunako mwaka 1868.

Kardinali Amato anasema kwamba, Mwenyeheri Mtarajiwa  Cestac alizaliwa kunako mwaka 1801 huko Ufaransa. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi akapewa Daraja takatifu la Upadre 1825 akiwa na umri wa miaka 24. Akatekeleza maisha na utume wake wa Kipadre kwa ari na moyo mkuu. Akaguswa na mahangaiko ya wasichana yatima na maskini, akaamua kuanzisha kituo cha watoto wadogo, ili kuwapokea na kuwapatia nafasi ya kusoma.

Ni Padre alijisadaka kwa ajili ya kuwaokomboa wasichana na wanawake waliokuwa wanatumbukizwa katika utumwa mamboleo, kwa kuwapatia fursa za kujiendeleza, ili hatimaye, waweze kujitegemea wenyewe. Aliwataka wasichana na wanawake hawa kukita maisha yao katika toba na wongofu wa ndani ili kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao.

Ili kufanikisha azma hii, akaanzisha nyumba ya kuwapokea na kuwatunza wasichana na wanawake hawa. Kunako mwaka 1842 akaanzisha Shirika la Watawa Watumishi wa Maria, ambao aliwakabidhi dhamana ya kusimamia na kuratibu shughuli za kichungaji alizokuwa amezianzisha. Akafariki dunia katika hali ya utakatifu kunako tarehe 27 Machi 1868. Shirika alilolianzisha, likaendelea kupanuka na kuchanua kama Mwerezi wa Lebanon, leo hii limeenea sehemu mbali mbali za dunia.

Kardinali Amato anabainisha kwamba, Mwenyeheri Mtarajiwa ni Padre aliyetoa kipaumbele cha pekee katika maisha yake kwa kumpenda Yesu Kristo, Kanisa na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Alikuwa na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu; Ibada kwa Bikira Maria na Watakatifu. Ni Padre ambaye aliyakita matumaini yake katika huruma ya Mungu, iliyomwajibisha kupenda, kufariji, kusamehe na kukimbilia neema na huruma ya Mungu.

Mwenyeheri Mtarajiwa Padre Cestac ni kielelezo cha imani kwa Mungu na neema zake katika maisha ya binadamu. Huyu ni Mungu ambaye anaendelea kujifunua katika historia ya binadamu, Kanisa na katika maisha ya familia na watu wa kawaida. Binadamu ni watoto wa Mungu anayewapenda na kuwaongoza; anayewafundisha kuhusu upendo kwa jirani. Padre Cestac alionesha upendo na huruma kwa maskini na wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Akawaonesha ukarimu na huruma.

Mwenyeheri Mtarajiwa Padre Cestac ni kielelezo cha utakatifu wa maisha ya Kikristo unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha, kwa kujikita katika uaminifu na uchapakazi. Wakristo wawe tayari kukimbilia huruma na upendo wa Mungu unaojikita katika Sakramenti ya Upatanisho. Lengo ni kudumisha neema ya utakaso, ili kumpokea Yesu katika Fumbo la Ekaristi kwa moyo mnyofu. Hii ndiyo changamoto inayotolewa na Mwenyeheri Padre Cestac kwa Familia ya Mungu nyakati hizi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.