2015-05-29 14:48:00

Kardinali Dominique Mamberti atunukiwa tuzo ya heshima na Rais wa Croatia


Bibi Kolinda Grabar-Kitarovic, Rais wa Jamhuri ya Croatia, Alhamisi tarehe 28 Mei 2015 amemtunukia Kardinali Dominique Mamberti, Mwenyekiti wa Mahakama kuu ya Kitume ya Kanisa Katoliki, tuzo ya heshima ya hali ya juu ya Mfalme Trpimir wa Jamhuri ya Croatia kutokana na mchango wake mkuu uliowezesha mchakato wa maboresho kati ya Vatican na Croatia.

Kardinali katika hotuba yake fupi ya kushukuru anasema kwamba, kunako mwaka 879, Papa Yohane VIII katika barua aliyomwandikia Mfalme wa Croatia Bwana Branimir aliitambua Croatia kama nchi huru, hatua kubwa katika masuala ya kisiasa Barani Ulaya kwa wakati ule. Wananchi wa Croatia wameendelea kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa Bara la Ulaya kwa njia ya maboresho ya tunu msingi za maisha ya Kikristo, kiutu, kiroho, kitamaduni na katika uzuri.

Ni matumaini ya Kardinali Mamberti kwamba, ushirikiano huu kati ya Vatican na Croatia utaendelea kudumishwa kwa ajili ya mafao ya pande hizi mbili pamoja na kuzingatia kwamba, kwa sasa Croatia ni nchi mwanachama wa Umoja wa Ulaya. Kardinali Mamberti amemshukuru Rais Kolinda kwa kumtunukia heshima hii kubwa na kwamba, anaiombea nchi ya Croatia awajalie maendeleo na ustawi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.