2015-05-27 16:18:00

Tafakari ya Neno la Mungu, Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu!


Mpendwa msilikilzaji wa Neno la Mungu, leo tunaadhimisha Fumbo la Utatu Mtakatifu. Ni sherehe kati ya sherehe za Bwana ambayo huadhimishwa Dominika inayofuata mara baada ya Pentekoste. Mama Kanisa ameweka sherehe hii baada ya Pentekoste kwa sababu anajua tayari fumbo zima la Utatu Mtakatifu limekwishafunuliwa na kufundishwa kwa kina na Mama Kanisa. Na kwa namna hiyo Mama Kanisa anatushirikisha furaha ijayo kwetu kila siku kwa njia ya Utatu Mtakatifu. Anatushirikisha fumbo la Mungu kukaa nasi daima mpaka ukamilifu. Kwa njia ya fumbo hili upendo wa Mungu kwa wanadamu unafunuliwa hatua kwa hatua mpaka ukamilifu wake. Basi ninakualika kutafakari Neno la Mungu kwa furaha kuu ukitambua kuwa kwa njia ya Utatu Mtakatifu umekuwa mwana wa Mungu.

Tunasikia katika somo la kwanza, katika kitabu cha Kumbukumbu la Torati, Musa anawaalika Waisraeli kutafakari matukio kadhaa katika historia ya maisha yao na ni jinsi gani Mungu alivyowapendelea kiasi kwamba mara zote amewaokoa katika taabu mbalimbali. Kwa namna hiyo anataka wajenge tumaini kuu katika yeye daima wakitambua kuwa Mungu ni mkuu katika mbingu na nchi. Wanapaswa kutambua na kusimulia kwa mataifa kuwa Mungu wao ni upendo usio na mwisho. Namna ya kuthibitisha na kutangaza kwa mataifa tendo la upendo wa Mungu ni kwa njia ya kushika amri za Mungu kama kielelezo na cha imani na mapendo kwa Mungu.

Hivi leo ndugu yangu mpendwa yako mambo mengi ambayo Mungu amekutendea ambayo tukiyaorodhesha karatasi hazitatosha! Tuseme tu kidogo, amekujalia ubatizo ukawa mtoto mteule wake, amekupa afya njema, amekuepusha na ajali, amekuweka katika familia na zaidi anakusindikiza mara zote ili ukadumu katika imani. Je kwa haya hupaswi kumrudishia angalau kidogo kwa kushika amri zake? Tafakari. Basi ndugu yangu mpendwa tukumbuke Mungu wetu ni upendo usio na mwisho, usio na ubaguzi bali mkamilifu kwa ajili ya wote.

Mtume Paulo anapowaandikia Warumi anawakumbusha zawadi ya Roho Mtakatifu waliyoipokea kwa njia ubatizo. Anasema kwa njia ya Roho Mtakatifu waliyepewa wamekuwa wana wa Mungu na wanaweza kumwita Mungu, Baba. Wakishakuwa wana wa Mungu wanakuwa warithi wa kiti cha enzi pamoja na Kristo. Ewe rafiki yangu mpendwa oneni jinsi Roho Mtakatifu alivyo chimbuko la kila aina ya zawadi za kimungu. Kumbe tunaposhangilia na kusherehekea fumbo la Utatu Mtakatifu tunashangilia na kumshukuru Mungu kwa zawadi mbalimbali alizotujalia. Tunashangilia hasa lile fumbo la sisi kufanywa wana wana wa Mungu.

Mwinjili Matayo katika sehemu ya Injili yake anatuambia kuwa wanafunzi kumi na mmoja wako Galilaya kama ambavyo Bwana aliwaagiza. Bwana anawatokea na wanamsujudia, ingawa baadhi yao wana mashaka! Akiwatia moyo anawatuma akisema enendeni sasa duniani kote mkafundishe na kuwafanya mataifa yote kuwa wanafunzi wangu. Anawaambia, kisha kufundisha mkawabatize katika Utatu Mtakatifu. Kwa njia ya ubatizo katika Utatu Bwana anaanzisha maisha mapya, maisha ya kimungu. Anaweka mbegu ambayo inapawswa ikue na kuzaa matunda. Anapowatuma katika ulimwengu hawaachi peke yao bali anawahaidi kuwa familia ya Utatu Mtakatifu itakuwa pamoja nao.

Kama ambavyo Mwinjili Matayo anaanza Injili yake kwa kumweka Yesu katikati ya ukoo wa Daudi na jinsi ambavyo anapewa jina Emmanueli yaani Mungu yuko pamoja nasi (Mt. 1:23) ndivyo Matayo anavyomalizia Injili kwa ahadi ya Kristu kuwa pamoja nasi mpaka ukamilifu wa dahari. (Mt 28:20) Kwa habari hii njema ya furaha yakuwa Bwana yu pamoja nasi yatuonesha kuwa Utatu Mtakatifu ni upendo mkamilifu kwa wote na kwa vizazi vyote.

Mpendwa, Fumbo la Utatu Mtakatifu kwa kawaida ni fumbo kuu kati ya mafumbo makuu matatu, yaani fumbo la Ekaristi Takatifu na umwilisho, fumbo la neema za Mungu na Utatu Mtakatifu ambao ndio tunasherehekea leo. Ni fumbo ambalo si rahisi kulielewa kwa undani na ukamilifu wake kwa maana ndiyo Mungu mwenyewe. Tunachotambua ni kuwa Mungu Baba ni muumbaji, na alipokwisha kuumba mbingu na nchi alimtuma Mwanae ili aokoe mwanadamu aliyepoteza uzuri aliokabidhiwa na Mungu Baba na hivi Mungu Mwana ni Mkombozi.

 

Mwana alipokwisha kufundisha na kumaliza kazi yake kabla ya kupaa mbinguni alihaidi kumpeleka Roho Mtakatifu  mfariji na mwalimu atakayetukumbusha yote na tena hatafanya kinyume na yale yaliyofundishwa na Bwana. Kumbe, Utatu Mtakatifu ni Mungu mmoja lakini nafsi tatu zisizogawanyika, yaani Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Kutambua na kujaribu kuelewa tunahitaji kuwa na imani thabiti. Ninakutakieni sherehe njema, ukajazwe imani, furaha na mapendo katika maisha yako katika Utatu Mtakatifu.

Tumsifu Yesu Kristo. Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya, C.PP.S.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.