2015-05-27 11:13:00

Mwenyeheri Sr. Irene Stefania, Utuombee!


Umati mkubwa wa Familia ya Mungu kutoka ndani na nje ya Afrika Mashariki ulishangilia pale Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania,  kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko alipomtangaza Mtumishi wa Mungu Sr. Irene Stefania, mtawa wa Shirika la Consolata kuwa Mwenyeheri hapo tarehe 23 mei 2015, Jimboni Nyeri, Kenya. Ibada ya Misa Takatifu imeongozwa na Kardinali John Njue, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya.

Katika mahubiri yake, Kardinali Njue amemwelezea Mwenyeheri Sr. Irene Stefania kuwa ni mtawa aliyakita maisha yake katika huduma ya upendo kwa maskini na wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii, kiasi hata cha kuhatarisha maisha yake. Mwenyeheri Irene Stefania ni kielelezo cha wito, sadaka na majitoleo katika maisha na utume wa kimissionari, changamoto kwa Wakristo kutangaza na kushuhudia Injili kwa Watu wa mataifa.

Kardinali Njue anawataka vijana kushiriki kikamilifu katika mchakato wa ujenzi na ustawi wa Kanisa na Jamii kwa ujumla, kwa kufuata mfano wa maisha na utume wa Mwenyeheri Sr. Irene Stefania aliyejitosa kimasomaso kushuhudia upendo wa Kristo uliokuwa unamwilishwa katika huduma. Ni mfano bora wa kuigwa na Familia yote ya Mungu, kwa kujikita katika tunu msingi za Injili zinazowaunganisha watu kutoka katika kila kabila, lugha, jamaa na taifa.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Peter Kairo wa Jimbo kuu la Nyeri, Kenya amewataka waamini kuiga mfano bora wa maisha ya Mwenyeheri Sr. Irene Stefania, „Nyaatha“ aliyejisadaka kwa Kristo na Kristo akawa ni yote katika maisha yake. Awe ni mfano bora wa kuigwa katika kukuza na kudumisha imani, umoja, upendo na mshikamano sanjari na kuwajali pamoja na kuguswa na mahangaiko ya wengine.

Tukio hili la kihistoria limehudhuriwa pia na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya ambaye pamoja na mambo mengine amekazia umuhimu wa kudumisha maridhiano kati ya waamini wa dini mbali mbali nchini Kenya, ili kuendeleza uhuru wa kuabudu. Serikali ya Kenya itaendelea kulinda na kudumisha uhuru wa kuabudu bila wasi wasi wala woga.

Sr. Irene Stefania aliyekuwa na maisha bora nchini Italia, aliamua kuacha yote na kufuata wito wa kimissionari, ili kuitumikia Familia ya Mungu Barani Afrika, akaonesha upendo katika huduma, daima akitafuta mafao ya wengi. Ni mtawa aliyekuwa na imani thabiti, tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu; mambo msingi yaliyosaidia kuleta mabadiliko katika maisha ya watu amesema Mwai Kibaki, Rais mstaafu wa Kenya katika Ibada hii.

Mwenyeheri Sr. Irene Stefania aliwasili nchini Kenya kunako mwaka 1915 na kufariki dunia kunako mwaka 1930 baada ya kuambukizwa ugonjwa wa tauni. Itakumbukwa kwamba, Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linaendesha pia mchakato wa kutaka kumtangaza Kardinali Maurice Otunga kuwa Mwenyeheri na hatimaye Mtakatifu kadiri ya mapenzi ya Mungu. Lakini kwa sasa Familia ya Mungu nchini Kenya inaye mwombezi mbinguni, yaani Sr. Irene Stefania.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican kwa msaada wa CISA na CANAA.








All the contents on this site are copyrighted ©.