2015-05-27 11:35:00

Mwenyeheri Oscar Romero ni mfano wa kuigwa katika kutetea haki na amani


Hivi karibuni Mama Kanisa amemtangaza Askofu mkuu Oscar Arnulfo Romero kuwa Mwenyeheri. Ni kiongozi aliyesimama kidete kuwalinda, kuwatetea na kuwatunza maskini na wote waliokuwa wanaonewa na kunyanyasika. Alijitosa kimasomaso kwa ajili ya kutetea utu na heshima ya binadamu, kiasi cha kuuwawa kikatili kunako mwaka 1980 kutokana na chuki za imani. Kiongozi huyu wa Kanisa aliuwawa wakati wa maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, sadaka kwa ajili ya wananchi wa El Salvador na Amerika ya Kusini katika ujumla wake.

Familia ya Mungu Barani Amerika inamwona na kumtambua Mwenyeheri Oscar Romero kwamba, alikuwa ni kiongozi aliyekuwa na upeo mpana, mwono ambao umekuwa ni dira na mwongozo wa sera na siasa kwa wapenda haki na amani Barani Amerika. Ni maneno yaliyomo kwenye tamko la Rais Barack Obama wa Marekani lililotolewa hivi karibuni wakati wa maadhimisho ya kumtangaza Askofu mkuu Oscar Romero kuwa ni Mwenyeheri, tukio ambalo limehudhuriwa na bahari ya watu kutoka ndani na nje ya El Salvador.

Kwa namna ya pekee, Rais Obama anamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa uamuzi wake wa kumtangaza Askofu mkuu Oscar Romero kuwa ni Mwenyeheri. Anasema, alipotembelea El Salvador kunako mwaka 2011, alipata heshima ya kwenda kusali kwenye kaburi la Askofu mkuu Oscar Romero, kiongozi mwenye hekima na busara; mwenye ujasiri aliyethubutu kupambana na changamoto za maisha bila kuogopa.

Rais Obama anasema kwamba, Askofu mkuu Oscar Romero alisimama kidete kupinga uonevu na baa la umaskini miongoni mwa watu wake. Siku moja kabla ya kuuwawa kwake, aliwataka Askari kutokubali kutumiwa kama vyombo vya mauaji na Serikali dhalimu na matokeo yake, akauwawa wakati akiwa anaadhimisha Ibada ya Misa takatifu. Akawa ni shuhuda wa imani  kwa El Salvador na Amerika, na baadaye watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia wakatambua na kuguswa na ushuhuda wa imani yake, kiasi cha kutambua utakatifu wa maisha yake.

Rais Obama anasema kwamba, ushuhuda wa maisha na imani yake, uwe ni changamoto kwa Familia ya Mungu kusimama kidete: kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu. El Salvador katika kipindi cha miaka thelathini na mitano imepiga hatua kubwa kwa kujenga na kudumisha demokrasia, lakini bado kuna mengi ambayo yanapaswa kufanyia maboresho kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wa El Salvador.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.