2015-05-27 12:09:00

Hati ya kutendea kazi ya Sinodi ya familia kutolewa wakati wowote!


Baba Mtakatifu Francisko ameshiriki kwa ukamilifu katika mkutano wa tisa wa Baraza la kawaida la Sinodi ya Maaskofu, lililokuwa pamoja na mambo mengine linapembua kwa kina na mapana hati ya kutendea kazi ya Mababa wa Sinodi ijulikanayo kama “Instrumentum Laboris” kwa ajili ya Sinodi ya familia itakayoadhimishwa  hapa mjini Vatican kuanzia tarehe 4 hadi tarehe 25 Oktoba 2015. Sinodi hii inaongozwa na kauli mbiu “Wito na utume wa Familia ndani ya Kanisa na Ulimwengu mamboleo”.

Taarifa kutoka katika Sekretarieti kuu ya Sinodi ya Maaskofu iliyokutana kuanzia tarehe 25 hadi tarehe 26 Mei 2015 inaonesha kwamba, kazi ya kuandaa hati ya kutendea kazi imekamilika na hati hii itatolewa katika kipindi cha muda mfupi kuanzia sasa, tayari kutoa nafasi ya kuendelea kufanya tafakari, tayari kushirikisha mang’amuzi, mawazo na tafakari wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu.

Baba Mtakatifu Francisko kwa namna ya pekee, amekazia umuhimu wa mchakato wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu. Muswada wa Hati ya kutendea kazi umeboreshwa zaidi kutokana na hati elekezi iliyotolewa na Mababa wa Sinodi maalum kwa ajili ya familia, iliyoadhimishwa, mwaka 2014.

Muswada huu pia unajumuisha maboresho ya majibu yaliyotolewa kwenye hati elekezi ya maadhimisho ya Sinodi ijulikanayo kama “Lineamenta” iliyokuwa imetumwa kwa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia, taasisi na wadau wenye dhamana ya kutangaza Injili ya Familia kwa Watu wa Mataifa. Majibu yote haya yamewawezesha wajumbe wa Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu kufanya maboresho makubwa ili hatimaye, hati ya kutendea kazi iweze kuchapishwa.

Kimsingi, wajumbe wamekubaliana na maudhui yaliyopendekezwa. Sekretarieti imepewa dhamana ya kuchapisha hati hii kwa lugha mbali mbali, tayari kuzinduliwa rasmi. Baada ya kazi hii kukamilika, wajumbe wamepewa mapendekezo ya taratibu na kanuni za maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya familia, itakayoadhimishwa hapa mjini Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.