2015-05-27 15:59:00

Fumbo la Utatu Mtakatifu: Kazi ya Kuumba, Kukomboa na Kutakatifuza


Katika maadhimisho ya Fumbo la Utatu Mtakatufu, tunaongozwa na Liturujia ya neno la Mungu kutoka katika vifungu vifuatavyo: MASOMO – 1. Mithali 8: 22-31. 2. Rom 5: 1-5. 3.Yoh 16: 12-15. Inafaa, kuchukua Biblia yako au Misale ya Waamini ili kuvisoma vifungu hivi ili uweze kupata utajiri wa Neno la Mungu na tafakari inayofuatia. Mungu ameongea nasi katika historia. Ndugu wapendwa, sherehe yetu ya leo ni matokeo ya uwepo huo wa Mungu katika matukio ya maisha yetu.

Somo la kwanza: Halizungumzii hasa Utatu Mtakatifu - ila zipo dalili za ukweli huo. Aidha iko wazi habari ya Mungu mmoja wa Israeli - Mungu ni mmoja. Na huyu Mungu anaonekana kwao katika matukio mbalimbali ya maisha yao ambayo kabla yake hayakuwa hivyo.

Katika somo la Pili: Mt. Paulo – anazungumzia Utatu Mtakatifu ukiwa kazini - hatuna maelezo ya utatu mtakatifu yanayotolewa - bali twaona kile ambacho Mungu Baba, Mwana na Roho Mtakatifu wanafanya katika maisha yetu. Aongea juu ya kuitwa wana wake n.k ila hilo limewezekana tu kwa sababu ya ufunuo wa Mwana na kwa njia yake sisi tunakuwa wana.

Je, Mtume Paulo alifahamuje ukweli huu? Ni katika maisha ya wafuasi na katika maisha yake mwenyewe. Wote walimwita Mungu Baba kama alivyofanya Yesu. Ni nguvu gani inamsukuma Paulo? Ni Roho wa Mungu. Katika barua zake nyingine, mtume Paulo aongea kumtambua Roho katika nafasi mbalimbali kama kufundisha, kuponya n.k. Katika Rom. 5.1-5 huunganisha Fumbo la Utatu Mtakatifu na maisha ya kila siku ya mkristo.

Mtakatifu Paulo anaunganisha mtandao mzima wa haki na wokovu kama kuwa na amani na Mungu. Kuwa na uhusiano na Mungu ni wajibu wetu mkuu na ni njia ya Kristo - 5:1-2 - basi tukiisha kuhesabiwa haki itokayo katika imani na tuwe na amani kwa Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo. Ambaye kwa yeye tumepata kwa njia ya imani kuifikia neema hii ambayo tunasimama ndani yake katika tumaini la utukufu wa Mungu.

Katika Injili –habari juu la Fumbo la Utatu Mtakatifu iko wazi. Mitume na wafuasi wanatumwa kubatiza na katika ubatizo, fumbo la Utatu Mtakatifu huanza kuwepo katika maisha yetu. Ungamo la imani yetu katika sala ya nasadiki huthibitisha rasmi tamko letu la upendo kwa fumbo hilo.

Mt. Agostino wa Hippo akitaka kueleza utatu mtakatifu kadiri ya akili ya mwandamu - siku moja akitafakari jambo hili maeneo ya ufukweni ghafla akamwona mtoto mdogo peke yake. Huyo mtoto alikuwa ametengeneza kishimo na alikuwa akichota maji baharini na kuyamwaga katika kale kashimo. Mt. Agostino akamwuliza unafanya nini? Mtoto akamjibu nataka kuweka bahari hii katika kashimo haka. Mt. Agostino akamwambia itawezekanaje? Kujaza kashimo haka kwa maji ya bahari yaliyo mengi kiasi hiki?

Naye yule mtoto akamwambia nawe je wadhani kuwa kichwa chako kidogo na moyo wako mdogo utaweza kuelewa kwa kina na kupenda kikamilifu fumbo la utatu mtakatifu? Mara mtoto yule akatoweka.

Mapenzi ya Mungu Baba ni kutupata sisi na matumaini yetu ni kuwa pamoja na Baba. Hii inawezekana kwa njia ya Kristo. Matumaini yetu ni kushiriki utukufu wa Mungu. Hii huwezekana kwa njia ya imani inayotupa matumaini. Mungu ametupa matumaini hayo – Rom. 5:5 na tumaini halihatarishi kwa maana pendo la Mungu limekwisha kumininwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi. Huu upendo wa Mungu umemwagwa mioyoni mwetu kwa njia ya Roho Mtakatifu.

Msingi wa maisha ya Kristo hujengwa katika Utatu Mtakatifu na hii ndiyo tofauti moja kubwa kati ya dini ya kikristo na dini nyingine. Dini nyingine hutazama mhusika (mwamini) na Mungu wake tu. Ukristo pia una mtazamo huo, ila huongeza uwepo wa Yesu Kristo (MKOMBOZI) anayetuunganisha na Baba (MUUMBA) na Roho Mtakatifu (ANAYETAKATIFUZA).

Wajibu wetu wa Kikristo hauanzii na kuishia tu katika imani kwa Kristo na kupewa haki na Mungu. Huo tu ni mwanzo. Toka hapa huanza kazi ya kusaka wokovu, kuwa watakatifu kama Baba alivyo mtakatifu. Sherehe ya PENTEKOSTE tuliyosherekea jumapili iliyopita inashika kasi hapa. Kwa njia ya roho, upendo wa Mungu humwagwa mioyoni mwetu na kwa njia yake tunajifunza kumpenda Mungu na jirani kama alivyotufundisha Bwana.

Swali muhimu - hili fumbo linatuambia nini juu ya Mungu tumwaminiye na ni aina gani ya watu tunapaswa kuwa? Mambo mawili. a) Katika Mt. 5:48 tunasoma hivi; basi ninyi mtakuwa wakamilifu kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu. Mungu ni wa ushirika - tasaufi ya kikristo inatuwajibisha ulimwenguni.

b) Pendo la kweli lahitaji watu watatu – angalia msemo wa zamani - wawili ni ushirika, watatu ni umati. Baba/mama/mtoto hutengeneza upendo. Huyu Mungu tumwaminiye sisi hufahamika kwetu katika Utatu. Kidunia tunahusiana kati yetu na kimbingu tunahusishwa na Mungu. Mimi ni mkristo kweli nikiishi katika ushirika wa upendo na Mungu na watu wake.

Kwa hakika fumbo la Utatu Mtakatifu haliwezi kueleweka wazi. Ukuu wake hubaki kuwa fumbo. Na leo hatutegemei kupata jibu kwa fumbo hilo. Wakristo wa kwanza kwa akili yao walielewa ufunuo wa Baba kwa njia ya Mwanae. Yesu ameongea nasi habari ya Baba aliyemtuma na juu ya Roho mtakatifu atakayempeleka. Hii iko wazi kwenye maandiko matakatifu. Yesu hutuambia wazi kuwa Mungu amemkabidhi yote, naye amemkabidhi yote Roho mtakatifu. Hapa twaona muungano wa Fumbo la  UTATU Mtakatifu.

Kama ilivyokuwa kwa Mt. Agostino - hatutaelewa ni kwa namna gani ila ni kwanini Mungu amejifunua kwetu. Ukuu wa fumbo hili ni huu: sisi tumeumbwa kwa mfano na sura yake Mungu. Kwa kadiri tunavyomuelewa Mungu ni jinsi hiyo hiyo tunavyojielewa zaidi. Wataalamu wa mambo ya dini wanatuambia kuwa waabuduo hujitahidi kufanana na kile wanachokiabudu. Wanaoabudu Mungu wa vita huwa watu wa vita. Wanaoabudu Mungu wa upendo huwa watu wa mapendo n.k. Kama alivyo Mungu anayeabudiwa ndivyo walivyo wale wanaomwabudu.

Tumsifu Yesu Kristo.

Na Pd. Reginald Mrosso, C.PP.S.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.