2015-05-26 16:06:00

Watanzania jiandikisheni kwenye Daftari la Wapiga Kura!


Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda amewataka Watanzania wote watumie fursa ya uboreshaji wa Daftari la Wapiga Kura kwa kujiandikisha ili waweze kushiriki uchaguzi mkuu ujao unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu. Akizungumza mara baada ya kujiandikisha kwenye Ofisi ya Mtendaji Kata iliyopo kijiji cha Kibaoni, wilayani Mpanda, mkoani Katavi hivi karibuni Waziri Mkuu alisema hii ndiyo fursa pekee ya kuwawezesha kushiriki uchaguzi mkuu ujao.

“Ninawasihi Watanzania wote tusiache kutumia fursa hii… kila mtu ahakikishe kuwa anajiandikisha. Ni fursa pekee itakayohakikisha kila mwananchi anashiriki uchaguzi wa kumpata Rais, Mbunge na Diwani,” alisema. Waziri Mkuu alisema amefarijika kwa kazi aliyoiona ikifanyika kwani hadi sasa Halmashauri za Nsimbo na Mlele zimefanikiwa kuandikisha watu kwa zaidi ya asilimia 100.

Mapema, akiwasilisha taarifa ya uandikishaji katika Halmashauri ya Mlele, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Bw. Godwin Benne alisema walilenga kuandikisha watu 19,482 lakini hadi kufikia jana walifanikiwa kuandikisha watu 20,292 sawa na asilimia 105. Uandikishaji katika wilaya ya Mlele ulianza tarehe 18 Mei, mwaka huu.

“Mlele tuna vituo 84 katika tarafa tatu za Inyonga, Mpimbwe na Mamba. Inyonga tuna vituo 28, Mpimbwe viko 23 na Mamba viko 33." Akifafanua zaidi, Bw. Benne alisema katika kata ya Kibaoni ambayo ina vituo sita, jana peke yake walifanikiwa kuandikisha watu 1,007 kikiwemo kituo cha Kibaoni ambacho Waziri Mkuu Pinda alijiandikisha. Alivitaja vituo vingine kuwa ni Milumba, Sungusungu, Ilalangulu, Manga na Shule ya Msingi Kakuni ambako Mama Tunu Pinda alijiandikisha jana hiyo hiyo.

Naye, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo, Bw. Neneka Rashid, uandikidhaji ulianza Mei 18, 2015 kwenye kata 12 na kwamba hadi kufikia jana, kata nne zilikwishaandikisha watu 12,001 sawa na asilimia 108.9 licha ya kuwa matarajio yao yalikuwa ni kuandikisha watu 11,014. Alizitaja kata hizo kuwa ni Nsimbo, Kapalala, Magamba na Uruwira.

Na Ofisi ya Waziri mkuu.








All the contents on this site are copyrighted ©.