2015-05-26 08:52:00

Mt. Giovanna Antida Thouret alijisadaka kwa ajili ya huduma ya mapendo!


Mama Kanisa ana utajiri mkubwa wa watoto wake ambao walijitosa kimasomaso, wakiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu ili aweze kuwatumia kama vyombo vyake vya kazi kwa mwanga wa Roho Mtakatifu. Hivi ndivyo ilivyokuwa kwa Mtakatifu Giovanna Antida Thouret, mwanzilishi wa Shirika la Watawa wa Upendo na wenzake Wenyeheri Enrichetta Alfieri, Nemesia Valle pamoja na Mtakatifu Agostina Pietrantoni. Watawa hawa walijisadaka kwa ajili ya huduma ya upendo kwa maskini na wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii bila kuwasahau wagonjwa waliokuwa wanahudumiwa mjini Roma.

Hayo yamesemwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Jumamosi jioni tarehe 23 Mei 2014 wakati wa mahubiri yake kwenye Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumbu kumbu ya miaka 250 tangu alipozaliwa Mtakatifu Giovanna Antida Thouret. Mahubiri ya Kardinali Parolin yaligusia kwa namna ya pekee kuhusu dhamana na nafasi ya Roho Mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa kama ilivyokuwa kwa Mitume wa Yesu wakati wa kuzaliwa kwa Kanisa la Mwanzo.

Mitume walishikwa na woga kiasi cha kujifungia katika undani wao, lakini waposhukiwa na Roho Mtakatifu, wakapata nguvu na ujasiri wa kutoka kifua mbele kumtangaza na kumshuhudia Kristo, kama walivyofanya watakatifu wa nyakati mbali mbali katika historia na maisha ya Kanisa. Mitume hao ni mfano wa watawa wanne wa Shirika la Upendo, waliobahatika kukutana na Yesu kwa njia ya huduma kwa maskini, wagonjwa na wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii.

Mtakatifu Giovanna Antida Thouret alilazimika kuishi uhamishoni, akaonja mateso, dhuluma na Msalaba katika maisha na utume wake, kiasi cha Shirika kugawanyika mikononi mwa wale ambao walikuwa wamepewa dhamana ya kulilinda na kuliendeleza. Lakini akaonesha moyo mkuu na upendo kwa ajili ya maskini, wafungwa na wote waliokuwa wanateseka. Akawaonjesha wale waliokata tamaa na matumaini ya maisha, mapendo na huruma ya Mungu.

Kwa mwaliko wa Sr. Nunzia De Gori, Mama mkuu wa Shirika la Watawa wa upendo wa Mtakatifu Giovanna Antida Thouret, Kardinali Pietro Parolin alizindua vitabu viwili vilivyoandikwa na Padre Ennio Apeciti, Gombera wa Seminari kuu ya Lombardo pamoja na Sr. Paule Germaine Corbani anayesimulia uzoefu na mang’amuzi ya Mwenyeheri Alfieri wakati wa maisha na utume wake nchini Sudan, mahali ambapo watawa wa Shirika hili wameendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa Familia ya Mungu, nchini humo, kwa kuwaonjesa faraja na upendo unaobubujika kutoka kwa Yesu Kristo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.