2015-05-26 15:22:00

Jimbo kuu la Maputo Msumbiji mwenyeji wa Injili ya Familia Barani Afrika


Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya, CCEE na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM kuanzia tarehe 28 hadi tarehe 31 Mei 2015 wanafanya semina inaoongozwa na kauli mbiu “Furaha ya Familia”, Semina hii inafanyika Maputo, nchini Msumbiji. Huu ni mwendelezo wa ushirikiano kati ya Makanisa haya mawili kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Familia ya Mungu, ili kujadiliana changamoto zinazolikabili Kanisa.

Maaskofu wanajadiliana changamoto hizi mintarafu Waraka wa kichungaji wa Baba Mtakatifu Francisko Injili ya Furaha na masuala mazito yatakayojadiliwa wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Familia itakayofanyika mwezi Oktoba, hapa mjini Vatican. Lengo kuu ni kuziwezesha Familia kutangaza na kushuhudia Injili ya Familia katika ulimwengu mamboleo, ambao unaendelea kutoa changamoto mbali mbali.

Taarifa kwa vyombo vya habari inaonesha kwamba, wajumbe wa Semina hii pamoja na mambo mengine watajadili kuhusu: changamoto za kiutu, kijamii na kikanisa kwa ajili ya familia: Furaha na mahangaiko ya familia: changamoto za kichungaji. Mambo mengine ni dhamana ya Kanisa na Askofu katika kutangaza Injili ya Familia; Dhamana ya Kanisa na Askofu katika mchakato wa majadiliano na jamii pamoja na Serikali kuhusiana na masuala ya Injili ya Familia.

Baada ya maadhimisho ya Semina hii, Maaskofu watatoa tamko la pamoja. Askofu Lucio Muandula, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Msumbiji ndiye mwenyeji wa semina itakaongozwa na Askofu mkuu Gabriele Mbilingi, Rais wa SECAM. Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya litawakilishwa na mjumbe maalum kutoka kwa Kardinali Peter Erdò, Rais wa CCEE.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.