2015-05-25 14:47:00

Uchaguzi mkuu nchini Tanzania kufanyika tarehe 25 Oktoba 2015!


Jaji Damiani Lubuva Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi nchini Tanzania anasema kwamba, kampeni za uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utaanza kutimua vumbi tarehe 22 Agosti hadi tarehe 24 Oktoba 2015. Watanzania watapiga kura hapo tarehe 25 Oktoba 2015 ili kuwachagua viongozi watakaowaongoza baada ya Rais Jakaya Kikwete kung’atuka kutoka madarakani kwa mujibu wa sheria.

Tume ya uchaguzi inaendelea na mchakato wa maboresho ya Daftari la kudumu la wapiga kura, zoezi ambalo linatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Julai na mwanzoni mwa juma la pili Mwezi Agosti, 2015. Wachunguzi wa mambo wanabainisha kwamba, mchakato wa uchaguzi mkuu nchini Tanzania kwa mwaka huu unaweza kutawaliwa na hasira ya wananchi kuhusiana na ongezeko la umaskini na hali ngumu ya maisha; rushwa na ufisadi wa mali ya umma.

Vyama vya upinzani vinapania kuweka mgombea mmoja atayewakilisha kambi yote ya upinzani na hapa wachunguzi wa mambo wanasema “hapa ni patashika nguo kuchanika” kwa upinzani kuking’oa Chama cha Mapinduzi kutoka madarakani. Wanachama wa CCM wapatao 15 hadi 17 wanatarajiwa kuchukua fomu za kuwania Urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi na kati yao, pengine wanachama watano tu ndio watakaopewa nafasi ya kufanya kampeni ili hatimaye aweze kupatikana mwanachama mmoja atakayepeperusha bendera ya CCM wakati wa uchaguzi mkuu.

Tanzania ina sifa ya kufanya chaguzi zake tangu mwaka 1995 kwa amani na utulivu, ingawa maneno maneno hayakosekani. Hali ya hewa kisiasa kwa baadhi ya Nchi za Afrika Mashariki si shwari sana kutokana na ukiukwaji wa Katiba ya nchi kwa baadhi ya viongozi kutaka kuendelea kung’ang’ania madarakani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.