2015-05-25 10:08:00

Kuenea kwa Boko Haram ni matokeo ya rushwa, udini, uchu wa mali na madaraka


Wachunguzi wa mambo ya kijeshi nchini Nigeria wanabainisha kwamba, Rais mteule Muhammadu Buhari anaanza kuonesha cheche za matumaini ya kutaka kutokomeza kabisa Kikundi cha Boko Haram, ambacho kwa miaka ya hivi karibuni, kimekuwa ni tishio la amani, haki, usalama na maridhiano kati ya wananchi wa Nigeria na nchi jirani. Idadi ya wananchi wanaokombolewa kwa sasa kutoka katika mikono ya Boko Haram inatia moyo na kwamba, kwa mwelekeo huu, Nigeria inaweza tena kuanza kupeta katika misingi ya amani.

Lakini Boko Haram kitaendelea kubaki katika historia ya Nigeria kwa kupandikiza mbegu ya chuki, uhasama na kifo kwa mamillioni ya watu na mali zao. Umoja, mshikamano, kanuni maadili na haki ni mambo msingi katika kufanikisha utawala wa sheria, kwani kushindwa kwa Serikali ya Bwana Goodluck Jonathan wa Nigeria katika mapambano dhidi ya Boko Haram ni matokeo ya rushwa, ufisadi, udini na uchu wa mali na madaraka.

Jeshi la Nigeria lina uwezo mkubwa, lakini wachunguzi wa mambo wanasema, lilishindwa kutekeleza dhamana na wajibu wake kutokana na usaliti uliokuwa unaandamana na ukiukwaji wa kanuni maadili ya kijeshi na usalama wa taifa. Huu ni uchambuzi ambao umefanywa hivi karibuni na Bwana Marco Massoni, mkurugenzi wa tafiti za Afrika katika kituo cha mikakati ya kijeshi nchini Italia, “CEMISS”.

Kinzani za kidini kati ya Wakristo na Waislam nchini Nigeria ni kati ya mambo yaliyopelekea Jeshi kushindwa kutekeleza wajibu wake barabara, hapa anasema Bwana Massoni kuna haja ya kuondokana na udini katika masuala ya kijeshi, vinginevyo, maafa yataendelea kutokea nchini Nigeria. Juhudu zilizofanywa na Nchi za Kaskazini mwa Afrika kwa kuunganisha nguvu ili kupambana na Boko Haram ni jambo la kutia moyo sana kwani Jumuiya ya Kimataifa inaonekana haikuwa na utashi wa kutaka kupambana kikamilifu na Boko Haram kwa sababu ya masilahi binafsi yanayojikita katika biashara haram ya silaha, mchezo mchafu unaogharimu maisha ya watu na mali zao.

Inashangaza kuona mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa mwaka mmoja tangu waliopotekwa wasichana 200 kutoka shule ya Chibok, lakini mataifa hayo hayo, yako kimya katika mauaji ya watu zaidi ya 2000? Hapa wapenda amani wanasema, kuna jambo ambalo haliendi sawasawa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.