2015-05-25 13:53:00

IOR yapata faida kubwa ya kiasi cha Euro millioni 69. 3 kwa Mwaka 2014!


Benki kuu ya Vatican, IOR imefunga mwaka 2014 kwa kupata faida ya Euro millioni 63.3, ikilinganishwa na mwaka 2013 ilipofunga mwaka kwa kupata faida ya Euro millioni 2.9, taarifa iliyotolewa na Bwana Max Hohenberg, msemaji mkuu wa IOR alipokuwa anahojiwa na Radio Vatican. Haya ni mafanikio makubwa baada ya kujikita katika  mchakato wa mabadiliko kwa kuzingatia weledi, ukweli na uwazi; uwajibikaji na tija. Akaunti 4, 600 zilifungwa kwa sababu wateja wake walikosa sifa za kutumia Benki ya Vatican au akaunti hizi zilikaa kwa muda mrefu pasi na kushughulikiwa na wateja.

Benki ya Vatican katika miezi ya hivi karibuni imedhibiti matumizi yasiyokuwa ya kawaida kwa kuzingatia sheria, kanuni na maadili ya kazi na matokeo yake ni faida ambayo kwa sasa inajionesha wazi pasi na upinzani. Hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko aliridhia sheria na kanuni za masuala ya fedha za Kanisa na kwamba, matokeo yake yanaanza kuonekana. Dhamana ya Benki ya Vatican ni kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kiulimwengu na Vatican na ndiyo maana haina budi kufanya mabadiliko makubwa kadiri ya vigezo na kanuni hizi.

Benki ya Vatican itaendelea kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa Kanisa zima kwa kutoa huduma za kifedha pamoja na kumsaidia Khalifa wa Mtakatifu Petro kutekeleza dhamana na wajibu wake wa kuliongoza Kanisa la Kristo, kama Mchungaji mkuu. Taarifa inaonesha kwamba, Benki ya Vatican inataka kuchangia kwenye Bajeti ya Vatican kiasi cha Euro millioni 55, kiasi ambacho kilitolewa pia kunako mwaka 2014.

Mabadiliko makubwa yaliyochangia kuleta faida kubwa kiasi hiki ni kujikita katika kanuni na maadili ya kazi. Changamoto kubwa iliyoko mbele ya Benki ya Vatican kwa sasa ni kuhakikisha kwamba, inaendelea kutoa huduma makini kwa wateja wake pamoja na kuendelea kuboresha mchakato na utunzaji wa rasilimali zake anasema Bwana Jean-Baptiste de Franssu, ambaye tangu kunako mwaka 2014 ameteuliwa kuwa Rais mtendaji wa Benki ya Vatican, maarufu kama IOR.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.