2015-05-24 11:48:00

Wenyeheri: Oscar Romero na Sr. Irene ni mashuhuda wa ujasiri wa Kiinjili


Roho Mtakatifu alipowashukia Mitume siku ile ya Pentekoste, huo ukawa ni Ubatizo wa Kanisa lililoanza hija ya maisha na utume wake katika historia, huku likiongozwa na Roho Mtakatifu. Mitume kwa Siku hamsini, walijifungia ndani, lakini Roho Mtakatifu alipowashukia, wakapata nguvu na ujasiri wa kutoka kifua mbele kwenda kutangaza Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Yesu Kristo. Mitume wakatangaza matendo makuu ya Mungu kwa njia ya lugha mbali mbali iliyoeleweka na wote, changamoto ya kuvunjilia mbali kuta za utengano zilizosababishwa na ujenzi wa Mnara wa Babeli. Roho Mtakatifu anawawezesha mitume kwenda duniani kote.

Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Anasema, Kanisa limezaliwa na linatumwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu duniani kote. Hili ni Kanisa Katoliki, lenya utambulisho makini na wazi, unaofumbata ulimwengu mzima bila kumtenga mtu yeyote.

Ujio wa Roho Mtakatifu kwa Mitume wa Yesu ni mwanzo wa nyakati mpya: kipindi cha ushuhuda na mshikamano wa kidugu; kipindi cha upendo unaopaswa kumwilishwa katika maisha ya watu kama kielelezo cha mwanga wa Injili ya Kristo unaogusa akili na mioyo ya wengi pasi na kizuizi cha lugha, rangi au taifa. Roho Mtakatifu anaendelea kutenda ndani ya Kanisa kwa kuwataka waamini kuwaonjesha jirani zao upendo unaobubujika kutoka katika huruma ya Mungu. Wakristo wamebahatika kupata karama za Roho Mtakatifu, changamoto ya kumtangaza na kumshuhudia Kristo ambaye ni njia, ukweli na uzima.

Mara baada ya Sala ya Malkia wa mbingu, Baba Mtakatifu Francisko amesema kwamba, anafuatilia kwa wasi wasi mkubwa mateso na mahangaiko ya wakimbizi kwenye Ghuba ya Bengala. Anazishukuru na kuzipongeza nchi ambazo zimeamua kuwapokea na kuwakirimia wakimbizi hawa ambao kwa sasa wanakabiliana na hali ngumu ya maisha. Baba Mtakatifu anaiomba Jumuiya ya Kimataifa kuwasaidia wakimbizi hawa kupata mahitaji muhimu.

Baba Mtakatifu amewakumbuka pia Wenyeheri wapya Askofu mkuu Oscar Romero wa Jimbo kuu la San Salvador, aliyeuwawa kutokana na chuki za imani wakati alipokuwa anaadhimisha Ibada ya Misa takatifu. Mwenyeheri Oscar Romero ni mfano wa Kristo mchungaji mwema aliyethubutu kuchagua kuwa kati ya watu kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini na wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii, kiasi cha kulipia gharama ya maisha yake.

Baba Mtakatifu amemtaja Mwenyeheri Sr. Irene Stefania, Mtawa wa Shirika la Waconsolata, aliyewahudumia wananchi wa Kenya kwa furaha, huruma na wema. Mifano ya wenyeheri hawa iwe ni changamoto ya kutamani kushuhudia Injili kwa ujasiri bila ya kujibakiza.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.