2015-05-24 09:52:00

Dira ya maisha: Enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili


Siku ile ya Pentekoste, Roho Mtakatifu alipowashukia Mitume, alivunjilia mbali kuta za utengano zilizokuwepo katika akili na mioyo ya Mitume, akawajalia nguvu ya kutoka kimasomaso kutangaza Habari Njema ya Wokovu, huku wakitangaza matendo makuu ya Mungu kwa lugha mbali mbali. Bikira Maria alikuwa kati ya Mitume wakati wa kuzaliwa kwa Kanisa, akalisindikiza kwa njia ya amani na furaha. Roho Mtakatifu anatenda kazi kwa kuwaongoza watu na Jumuiya katika ukweli wote, anaumba upya sura ya nchi na kuwakirimia mapaji yake.

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, katika Sherehe ya Pentekoste, Jumapili tarehe 24 Mei 2015 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Anasema, Liturujia ya Neno la Mungu inaonesha kwamba, Roho Mtakatifu atawaongoza Mitume ili kufikia ukweli wote, kwani huyu ni Roho wa Ukweli atakayewasaidia kufahamu yale ambayo Yesu alitenda, lakini zaidi kifo na ufufuko wake, kwani kashfa ya Msalaba wa Yesu iliwatendea sana Mitume. Roho Mtakatifu anawasaidia kuwa na mwelekeo mpya ili kuangalia ukweli na uzuri wa Fumbo la Ukombozi.

Mitume ambao walikuwa wamejifungia kwa woga, wakihofia maisha yao baada ya kushuhudia “patashika nguo kuchanika” Siku ya Ijumaa kuu, hawataogopa tena kujitosa kimasomaso kutangaza Injili ya Kristo wala kusimama Mabarazani, kwani wamekwisha kumpokea Roho wa ukweli anayewaonesha kwamba, Fumbo la Msalaba ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo wa Mungu unaovunjilia mbali kifo na kumshuhudia Kristo mshindi na hai; Bwana na Mkombozi wa binadamu, historia na ulimwengu. Mitume wanakuwa ni mashuhuda wa ukweli na wanatumwa kuutangaza hadi miisho ya dunia.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, Roho Mtakatifu anabadilisha sura ya nchi na kuiumba upya, utenzi wa sifa kwa Mwenyezi Mungu, muumbaji wa vyote, dhamana inayoonesha uwepo wa Fumbo la Utatu Mtakatifu. Hii ni changamoto ya kuhakikisha kwamba, binadamu anatunza “Bustani” anamoishi, ili kuilinda na kuiendeleza, jambo linalowezekana, ikiwa kama atatambua uwepo wa Yesu Kristo Adam mpya kwa njia ya Roho Mtakatifu. Lengo ni kuisaidia Familia ya Mungu kuishi kama watoto huru wa Mwenyezi Mungu kwa kuwa na mahusiano mema na kila kiumbe ambacho kinaakisi utukufu wa Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake anaendelea kusema kwamba, Mtume Paulo anawataka Wakristo kuenenda katika Roho, kwani kamwe hawataweza kuzitimiza tamaa za mwili, kwani mwili hutamani ukishindana na Roho; dalili za ubinafsi kwa kujifungia dhidi ya neema ya Mungu. Mwamini anayemwachia nafasi Roho Mtakatifu anakirimiwa matunda kumi na mawili ya Roho Mtakatifu: Upendo, furaha, amani, uvumilivu, ukarimu, wema, utu wema, upole, uaminifu, utaratibu, kiasi na usafi wa moyo. Hii ndiyo dira na mwongozo wa maisha ya kikristo.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, ulimwengu mamboleo unawahitaji watu waliojazwa Roho Mtakatifu, kwani kukosekana kwa Roho Mtakatifu, ni dalili za dhambi na ukosefu wa uhuru wa kweli. Waamini wanaweza kumfungia nje Roho Mtakatifu kwa njia ya ubinafsi, sheria kali zinazojikita katika unafiki; ukosefu wa kumbu kumbu ya mambo msingi yaliyofundishwa na Yesu yanayopaswa kumwilishwa katika matendo  kama kielelezo cha huduma.

Dunia inahitaji watu wajasiri, wenye imani na matumaini na mitume wadumifu. Roho Mtakatifu amewakirimia waamini wote mapaji yake, ili waweze kuishi kwa imani, upendo na kueneza mbegu ya upatanisho na amani. Waamini wajifunge kibwebwe kupambana kufa na kupona na dhambi, rushwa na ufisadi; kwa kujikita katika mchakato wa kutafuta na kudumisha haki na amani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.