2015-05-23 08:04:00

Ujumbe wa Pentekoste kutoka kwa Baraza la Makanisa Ulimwenguni!


Utakieni Yerusalemu amani: na wafanikiwe wakupendao; amani na ikae ndani ya kuta zako, na kufanikiwa ndani ya majumba yako. Na ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja. Vifungu hivi kutoka katika Maandiko Matakatifu ndivyo vinavyoongoza ujumbe wa Siku kuu ya Pentekoste kutoka kwa Marais wa Mabaraza ya Makanisa Ulimwenguni, wanaomwomba Mungu wa maisha aweze kuwaongoza katika haki na amani, kauli mbiu waliyoifanyia kazi wakati wa maadhimisho ya mkutano mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni, uliofanyika nchini Korea ya Kusini, kunako mwaka 2013. Baraza la Makanisa linawaalika watu wote wenye mapenzi mema, kuungana pamoja katika hija ya haki na amani.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni linasema, inasikitisha kuona kwamba, amani inaendelea kutoweka sehemu mbali mbali za dunia na kwamba, pasi na haki, amani iko mashakani. Salam ya amani wanayotakiana Wakristo kimsingi ni matashi mema yanayomgusa mtu mzima: kiroho na kimwili; ni kuwatakia wengine usalama, amani, afya njema, ustawi, ukamilifu, mapumziko na utulivu wa ndani. Amani ni zawadi kubwa iliyonunuliwa na Yesu Kristo kwa njia ya mateso na kifo chake Msalabani.

Mama Kanisa anapenda kuwapatia watu amani ya kweli inayobubujika kutoka kwa Kristo, kwa kuchuchumilia haki na kukataa vita na kinzani zinazoendelea kuhatarisha maisha na ustawi wa binadamu sehemu mbali mbali za dunia. Yerusalemu bado ni mji ambao amani bado inakosekana kutokana na kukwama kwa majadiliano ya amani kati ya Israeli na Palestina pamoja na kukalia sehemu za Palestina kwa mabavu. Bado kuna kinzani na migogoro kati ya Wakristo, Wayahudi na Waislam na kwamba, hapa kuna haja ya kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini, maridhiano na upatanisho, ili kweli amani iweze kutawala katika mioyo ya watu.

Siku ya Pentekoste, yaani Siku 50 baada ya Ufufuko wa Yesu Kristo, Watu wa Mataifa walikuwa wamekusanyika, huku wakiendelea kusali na kumwomba Yesu Kristo Mfufuka. Wote walikuwa ni roho na moyo mmoja katika Kristo. Waliposhukiwa na Roho Mtakatifu wakawezeshwa kumzungumza katika lugha ambayo ilieleweka kwa wote na idadi ya Wakristo siku hiyo ikaongezeka maradufu. Roho Mtakatifu akawazawadia watu imani na ujasiri wa kumtangaza Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu kama alivyoshuhudia Mtakatifu Petro na kwamba, Yesu ndiye Mfalme wa amani.

Baraza la Makanisa linakumbusha kwamba, Siku kuu ya Pentekoste ni mwanzo wa Kanisa linalotumwa kumshuhudia Yesu kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka; tayari kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu sanjari na kukazia umoja wa Familia ya Mungu pasi na ubaguzi wala kinzani. Roho Mtakatifu anawahamasisha Wakristo pamoja na watu wote wenye mapenzi mema: kushikamana kwa kuonesha umoja katika tofauti, ili kujikita katika mchakato wa hija ya haki na amani.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni katika mateso na mahangaiko ya watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia, linapenda kuombea amani na ustawi dhidi ya utamaduni wa kifo kwa Familia ya Mungu duniani. Linaombea amani kati ya Israeli na Palestina; amani kwa nchi za Kiafrika; Barani Asia, Mashariki ya Kati, Amerika ya Kusini na sehemu mbali mbali za dunia.

Inakadiriwa kwamba, kuna zaidi ya watu 10, 000 wanaouwawa kila mwaka kutokana vita sehemu mbali mbali za dunia. Amani ni mhimili mkuu wa maisha na kwamba, Wakristo pamoja na watu wenye mapenzi mema wanatumwa ulimwenguni na Mfalme wa amani, kwenda kushuhudia tunu hii msingi katika ustawi na maendeleo ya binadamu, kama ilivyokuwa siku ile ya Pentekoste.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.