2015-05-23 15:41:00

Tangazeni Injili ya Uhai; pambaneni na umaskini na mifumo yote ya utumwa


Baraza la Kipapa la haki na amani kwa kushirikiana na Shirikisho la Kimataifa la Wanawake kwa ajili ya maisha na familia, WWALF pamoja na Shirikisho la Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani, WUCWO, kuanzia tarehe 22 hadi tarehe 24 Mei, 2015 linafanya mkutano wa kimataifa uliokuwa unajadili kuhusu vipaumbele vya maendeleo endelevu baada ya mwaka 2015, kwa kuangalia dhamana na nafasi ya wanawake katika utekelezaji wa mikakati hii.

Baba Mtakatifu katika ujumbe aliomwandikia Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani, anawapongeza wanawake Wakatoliki kwa kusimama kidete, kutaka kuchangia mawazo katika utekelezaji wa mikakati ya maendeleo endelevu kadiri ya maelekezo ya Umoja wa Mataifa. Wanawake anasema Baba Mtakatifu wanataka kutangaza Injili ya uhai, kupambana na umaskini pamoja na mifumo yote ya utumwa mamboleo; kupinga unyanyasaji na ukosefu wa haki msingi kwa wanawake sehemu mbali mbali za dunia.

Baba Mtakatifu anasema wanawake wanakabiliana na changamoto mbali mbali katika maisha na utume wao; wakati mwingine wanalazimika kufanya maamuzi magumu kati ya kazi na familia, wanauwawa na kunyanyaswa. Wanawake katika nchi changa duniani wanabeba mzigo wa kutafuta maji na baadhi yao wanafariki dunia wakati wakijifungua; wanadhalilishwa na kunyanyaswa kijinsia; wakati mwingine wanalazimika kufunga ndoa za shuruti kinyume cha utashi wao. Matatizo yote ni kati ya mambo ambayo yanatajwa kwenye mikakati ya maendeleo endelevu baada ya mwaka 2015.

Baba Mtakatifu anawakumbusha wanawake kwamba, wanapaswa kusimama kidete kulinda na kutetea Injili ya Uhai, utu na heshima ya binadamu. Washiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya baa la njaa na umaskini; dhuluma, nyanyaso na uonevu. Kanisa liwe ni chemchemi ya kanuni maadili inayojikita katika utu na heshima ya binadamu; haki na amani.

Baba Mtakatifu anawatia shime wanawake kujifunga kibwebwe ili kulinda na kutetea utu na heshima ya wanawake; kwa kuguswa na utu na huruma kwa ajili ya huduma kwa jirani. Kazi zao ziwe ni kielelezo cha weledi pasi na kutafuta faida binafsi au wapigania haki, bali watu wanaojisadaka kwa ajili ya mafao ya wengi, ili kujenga na kudumisha majadiliano, uelewano na maridhiano kati ya watu, kwa kuanzia na mambo madogo madogo. Wanawake wawe ni vyombo vya huruma na wema, mambo msingi yanayoleta upatanisho na umoja kwa Familia ya Mungu. Dunia inahitaji kuonjeshwa mchango wa wanawake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.