2015-05-23 07:44:00

Pentekoste ni: Ujio wa Roho Mtakatifu; Mwanzo wa Kanisa na Utume wa walei


“Roho ya Bwana imeujaza ulimwengu, nayo inaviunganisha viumbe vyote, hujua maana ya kila sauti, Aleluya!” (Hekima 1:7) Leo ni Sherehe ya Pentekoste ambapo Kanisa linaadhimisha lile tukio kubwa la Roho Mtakatifu kuwashukia Mitume katika ndimi za moto na kuwajaza mapaji yake saba ambayo ni hekima, akili, shauri, elimu, nguvu, ibada na uchaji wa Mungu, tayari kumshuhudia Kristo kwa Watu wa Mataifa.

Zimetimia siku hamsini baada ya kusherehekea ufufuko wake Bwana wetu Yesu Kristo. Muda wa siku hizo hamsini, Kanisa limekuwa katika shamrashamra za kuutangaza ufufuko huo wa Bwana. Kristo Mfufuka anatupatia uzima mpya na kutufanya sisi wanadamu ambao tulikuwa tumeanguka katika dhambi kurudi katika hadhi yetu na zaidi kufanywa kuwa warithi pamoja na Kristo.

Katika sherehe hii kubwa mambo kadhaa makubwa yanaadhimishwa. Kwanza tunaadhimisha ukamilifu wa Fumbo la Pasaka ambapo kama nilivyodokeza hapo juu, ufufuko wa Kristo unatuunganisha tena na Mungu. Zawadi ya Roho Mtakatifu anayemiminwa ndani mwetu ni uthibitisho wa muunganiko huo kwani kwa njia yake tunapokea uzima wa kimungu. Mwanadamu kwa asili ameunganika na Mungu lakini baada ya ile mbegu ya uovu kupandwa ndani mwake uzima huo wa kimungu unafifishwa na kuchakachuliwa kabisa.

Ujio wa Bwana wetu Yesu Kristo umeturejeshea uhusiano huo uliopotezwa kwa sababu ya dhambi zetu na zaidi kutuunganisha kuwa warithi pamoja naye katika ufalme wa Mungu. Sherehe ya Pentekoste inatuletea zawadi ya Roho Mtakatifu, uzima wa kimungu ndani mwetu ambao ni ukamilisho wa muunganiko huo kati ya Mungu na mwanadamu.

Pili, leo tunasherehekea kuzaliwa kwa Kanisa. Ni baada ya tukio la Pentekoste ndipo Mitume walipokea nguvu ya kimungu na kupata ujasiri wa kutoka na kuanza kutangaza Habari Njema kwa watu wote. Hili lilitokana na agizo la Yesu mwenyewe kabla ya kupaa kwake mbinguni alipowaambia: “Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi” (Mdo 1:8).

Roho Mtakatifu analiongoza Kanisa liweze kuendelea kumshuhudia Kristo Mfufuka kwa watu wote. Kanisa limeenea Ulimwenguni kote baada ya mitume kupokea nguvu hii. Watu walisafiri mahali kote bila kuogopa chochote wakitolea maisha yao kwa ajili ya Injili. “Sauti yao imeenea duniani mwote, na maneno yao hata miisho ya ulimwengu” (Zab 19:4).

Wajibu huo wa ushuhuda wa Kristo mfufuka kwa Mataifa yote unawajia kwa namna ya pekee waamini Walei ambao kwa sehemu kubwa ndiyo wanaotimiza jukumu hili katika shughuli zao za kila siku katika jamii. Hivyo jambo la tatu ni kwamba leo pia ni siku ya Utume wa Walei. Hati ya Mtaguso Mkuu wa pili wa Vatikano ijulikanayo kama “Lumen Gentium” au “Mwanga wa Mataifa” inasema hivi katika ibara ya 31 juu ya Walei: “Walei kadiri ya wito wao wanautafuta ufalme wa Mungu kwa kushiriki katika shughuli za kiulimwengu na kuziratibu kadiri ya mpango wa Mungu. Wanaishi ulimwenguni, yaani, katika kila taaluma na huduma za kiulimwengu. Wanaishi katika mazingira ya kawaida ya familia na jamii ambapo maisha yao hufungamanishwa humo. Wao huitwa na Mungu katika mazingira haya kuwajibika kila mmoja kwa nafasi yake na wakiongozwa na roho ya Injili waweze kuutakatifuza ulimwengu kutokea kwa ndani kama chachu”.

Sherehe ya Pentekoste inahitimisha kipindi cha Pasaka na kutuingiza katika Kipindi cha kawaida cha mwaka. Huu ni mwaliko wa kuwa mashuhuda wa Kristo mfufuka katika maisha yetu ya kila siku. Tafakari ya masomo ya leo ituongoze kuona namna tunavyopaswa kutembea katika safari hii ya ushuhuda huku tukiongozwa na Roho wa Mungu.

Katika Somo la kwanza tunachota fundisho moja ambalo kwalo tutashuhudia uwepo wa Roho wa Mungu katika maisha yetu ya kila siku. “Tunawasikia hawa wakisema kwa lugha zetu matendo makuu ya Mungu”. Huu ni mshangao ambao unawapata jamii ambayo inashuhudia mitume ambao wamejazwa na Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu anawafanya watangaze matendo makuu ya Mungu na kueleweka kwa watu wote. Kwanza huu ni uthibitisho kuwa utendaji wa Mungu haufungwi na mipaka ya lugha ama jamii tunayotoka.

Mwanzoni mwa tafakari hii tulisema “Roho ya Bwana imeujaza ulimwengu, nayo inaviunganisha viumbe vyote, hujua maana ya kila sauti”. Hii ndiyo karama ambayo tunapokea kutoka kwa Mungu, karama ambayo inatuwezesha kuwa wafafanuaji wa kazi za Mungu. Huu ndiyo utume ambao Kristo alikuja kuufanya, kuutangaza Ufalme wa Mungu katika mazingira yetu ya kawaida kwa kutenda matendo makuu ya Mungu.

Ni wazi kwamba, Yeye alitenda mengi lakini tunaweza kuyaunganisha yote katika neno moja, alitufunulia upendo wa Mungu jinsi ulivyo katika ukuu wake, upana wake na kina chake. Wajibu tunaopokea sisi wafuasi wake ni kuushuhudia upendo huo kwa kila tulitendalo. Roho Mtakatifu ambaye anatenda kazi ndani ya Kanisa atatuwezesha kutimiza hili. Hii ni ahadi ya Kristo kwetu aliposema “Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia” (Yoh. 14:26). Hivyo, leo hii tunapokumbushwa tena kumpokea Roho huyo wa Mungu ndani mwetu na kuruhusu atende kazi ndani mwetu tunatumwa kwenda kushuhudia kwa matendo yetu, yaani, maisha yetu ya kila siku, tukiufunua upendo wa Mungu kwa watu wote kusudi nao waweze kuyaona matendo makuu ya Mungu.

Somo la pili linafafanua zaidi somo la kwanza kwa kuziangalia huduma mbalimbali ndani ya waamini kama kazi ya Roho Mtakatifu ambaye anatuunganisha kuwa kitu kimoja. Huo ni mwaliko wa kuzitambua karama na vipaji mbalimbali ambavyo waamini hutunukiwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kuujenga ufalme wake hapa duniani. Uwepo wa Roho huyo mmoja unatuhimiza kuheshimiana na kujaliana kila mmoja kwa nafasi yake na pia kushirikishana huduma zetu.

Mwandamu kwa asili ni mjamaa. Kila mmoja anamhitaji mwenzake katika ukamilifu wake. Wahenga wanasema “kidole kimoja hakivunji chawa”. Mwanasheria hawezi kukamilisha huduma yake sawasawa bila ya msaada wa huduma za watu mbalimbali. Hapa watahusika wakulima ambao huzalisha chakula ili apate nguvu, pia wapo wafanyakazi wa idara mbalimbali ambazo hutoa vifaa vitakavyomsaidia kutimiza wajibu wake huo wa kisheria.

Kwa upande mwingine na hao wengine pia watamtumia mwanasheria huyu kwa ajili ya kuratibu sawa shughuli zao kadiri ya taratibu za mahala husika. Katika wito huu wa kumshuhudia Kristo neno hili, “pana tofauti za karama; bali Roho ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote”, litugutushe na kubaki katika umoja. Ushuhuda wa kweli hupatika katika umoja wa kindugu.

Katika Injili tunaona jinsi Roho Mtakatifu anatuunganisha na Mungu. Hii ni zawadi ambayo tumeipokea toka kwa Krsito mfufuka. Baada ya kufufuka kwake Kristo anawatakia amani Mitume wake na kujidhihisha kwao kwamba ni Yeye. Anawaonesha mikono yake iliyotobolewa kwa misumari na ubavu wake uliochomwa kwa mkuki. Neno la Mungu linatuambia kwamba “Basi wanafunzi wakafurahi walipomwona Bwana”. Lakini Kristo anawapeleka katika furaha kubwa zaidi ya kuunganika na Mungu. “Pokeeni Roho Mtakatifu, wowote mtakaowaondolwa dhambi, wameondolewa; na wowote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa”. Hapa tunaona mambo mawili. Mwanadamu anapokea uzima wa kimungu kwa kuvuviwa Roho Mtakatifu ndani mwake na kwa nguvu hiyo pia anapewa uwezo wa kimungu wa kuunganisha watu na Mungu kwa kuwasamehe dhambi zao. Dhambi ambayo hutenga mwanadamu na Mungu sasa inapata kiboko yake. Roho Mtakatifu anayelijaza Kanisa anawafanya watumishi wake waweze kumfukuza shetani ndani ya wanadamu na kuwaunganisha tena na Mungu. Hivyo, ushuhuda wetu unapata nguvu zaidi kwani tunakuwa tumemiminiwa nguvu ya kimungu ndani yetu ambayo “kwa hiyo twalia, ‘Aba!’, yaani, Baba” (Rom 8:15).

“Roho ya Bwana imeujaza ulimwengu, nayo inaviunganisha viumbe vyote, hujua maana ya kila sauti, Aleluya!” (Hekima 1:7). Jamii yetu ya leo ni mseto wa aina yake ambamo tunasikia sauti za kila aina. Teknolojia ya mawasilianao na mwingiliano wa watu kwa njia ya utandawazi unaifanya jamii kuwa wazi na pana zaidi katika kutoa, kuelezea na kuhariri habari za matukio mbalimbali ya kijamii. Matokeo yake ni mchanyato wa habari ambao mara nyingine huishia kutuchanganya na kutupotosha katika ukweli.

Kwetu sisi kama wana Kanisa hatupaswi kuishia katika mkanganyiko huu, tunaye Roho Mtakatifu ambaye anatusaidia kutambua maana ya kila sauti na kutenda kadiri ya mpango wa Mungu. Ni wajibu wetu kumpatia Roho Mtakatifu kipao mbele ili sote tuisikie sauti moja na kudumu katika umoja. Itakuwa ni bahati mbaya kwetu wana kanisa pale tutakapoacha kumpatia kipao mbele Roho Mtakatifu ili atuongoze na badala yake kujiongoza na sauti za kidunia ambazo hutupeleka katika maangamizi.

Hivyo, leo tunaposherehekea Sherehe ya Pentekoste tuombe neema ya Mungu ili kwa ujasiri tumruhusu Roho Mtakatifu atuongoze katika ukweli na tukiujua huo ukweli tutaishi katika uhuru wa wana wa Mungu (Rej Yoh. 8:32). Twendeni leo Ulimwenguni kote kuitangaza habari njema. Tunaye Roho Mtakatifu ambaye ni msaidizi, ni mfariji na ni mwalimu wetu ambaye anatuongoza si kwa shauri lake bali katika kweli yote. Kwa niaba ya Mtayarishaji wa Kipindi hiki Padre Agapito Mhando, Sr. Marximilliana Massawe na Padre Pambo Martin Mkorwe, Mimi ni Padre Joseph Mosha, nikikuaga kutoka Studio za Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.