2015-05-23 14:51:00

Mwaka Mtakatifu: Huruma ya Mungu inafumbata msamaha inaleta faraja!


Mpendwa Msikilizaji wa kipindi cha Hazina yetu, Tumsifu Yesu Kristo. Karibu kwa mara nyingine katika kipindi chetu fundishi cha Hazina yetu, tuendelee kujichotea hekima kutoka katika Hazina ya Mama Kanisa. Kukumbusha tu mpendwa msikilizaji, kwa wakati huu, tunaipitia barua ya Kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko iitwayo Misericordiae vultus yaani  “Uso wa huruma”; maalumu kwa ajili ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Tunafanya hivyo ili kujiaandaa kuuadhimisha mwaka huo vema. Tufahamu vema umaana na umuhimu wa huruma ya Mungu, na maadhimisho haya yatusaidie katika safari yetu ya kiimani na kijamii; ili tuwe kweli uzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, tulioitwa tutoke gizani, tupate kuzitangaza fadhili zake Mungu (1Pet.2:9).

Tutaishi huku tukitangaza fadhila za Mungu endapo tu tunajua na tunasukumwa na huruma ya Mungu. Ni huruma hiyohiyo ya Mungu ndiyo iliyo msukuma Kristo Yesu kutekeleza kazi nzima ya ukombozi kwa njia ya maisha, mateso na kifo na hatimaye ufufuko. Ni huruma hiyo ya Mungu ndiyo iliyotufanya sisi kuwa ni uzao mteule kwa njia ya Kristo Yesu. Ni huruma hiyohiyo ya Mungu ndiyo iliyotufanya sisi kuwa ni Taifa Takatifu.

Ni huruma hiyo hiyo ya Mungu ndiyo iliyotufanya sisi kuwa ni watu tunaomilikiwa na Mungu mwenyewe. Ni huruma hiyo ya Mungu ndiyo inayotuita sisi siku zote, tutoke gizani: tutoke katika giza la dhambi, giza na magomvi na mafarakano, giza la vita na kinzani mbalimbali, giza la uvivu na uzembe, giza la kukwepa majukumu, giza la ubaridi katika imani na kila giza la hila na udanganyifu.

Ni huruma hiyohiyo ya Mungu ndiyo inayotutuma sasa kila mmoja wetu kwa nafasi yake na kwa namna yake ya maisha ndani ya Kristo, kwa njia ya Kristo na pamoja na Kristo, twende tukatangaze kwa wote fadhili za Mungu.

Mpendwa msikilizaji, tusisahau kwamba kazi ya kutangaza fadhili  za Mungu inajumuisha maisha yetu mazima katika Kristo. Hatuwezi kutangaza fadhila za Mungu kwa njia ya maneno tu au kwa njia ya vikao vya meza za mviringo visivyomwilishika. Tunahitaji kumwilisha daima yale tunayoyafikiri na kuyajadili na kuyafanyia makubaliano. Lakini kwa sisi tunaomsadiki Kristo Yesu, kamwe tusifanye chochote pasipo nguvu na uwepo wa Kristo mwenyewe. Yeye mwenyewe alisema “Bila nguvu yangu, ninyi hamwezi lolote” (Yoh. 15:5). Ni huruma ya Kristo Yesu, ndiyo inayomfanya daima apende kuwa pamoja nasi hata katika safari yetu ya maisha ya kila siku. Tukiliitia jina lake takatifu kwa msaada wa neema yake tutaweza kuyamwilisha vizuri yale mema tunayoyatamani.

Baba Mtakatifu anaendelea kututafakarisha, juu ya Kristo Yesu anayeidhihirisha nafsi ya Baba ambaye kamwe hachoki wala kukata tamaa hata atakapokuwa amesamehe uovu, na kushinda kukataliwa na kudharauliwa, kwa njia ya huruma na msahama. Hilo linajidhihirisha katika mifano mitatu: mfano wa kondoo aliyepotea, mfano wa shilingi iliyopotea na ule  baba pamoja na wanawe wawili, maarufu kama hadhithi ya Baba mwenye huruma, yaani mfano wa Mwana mpotevu (Rej. Lk. 15:1-32).

Katika mifano hii, Mungu daima anaoneshwa akiwa na furaha timilifu, hasa pale anaposamehe. Katika mifano  hiyo tunapata kiini cha Injili na cha imani yetu kwa sababu, huruma imeoneshwa kama nguvu inayoshinda kila kitu, huku ikiujaza moyo mapendo. Baba mtakatifu Francisko anasema ‘Huruma inayojionesha katika msamaha, inaleta faraja’.

Kutoka katika mfano mwingine, tunapata mafundisho muhimu kwa ajili ya maisha yetu ya Kikristo. Akimjibu Petro, alipouliza ni mara ngapi haswa anapasa kusamehe, Yesu anajibu “Sikuambii mara saba, bali saba mara sabini” (Mt 18:22). Kisha anaendelea kueleza mfano wa mtumishi mwovu, aliyeitwa na bwana wake na kuambiwa alipe deni kubwa alilokuwa akidaiwa. Yeye aliposihi sana kwa magoti na machozi asamehewe, bwana wake alimsamehe, akafuta lile deni lote. Lakini yeye alipokutana na mtu mwingine aliyemdai fedha kidogo sana, na yule ndugu alishindwa kulipa lakini alimwomba amvumilie atalilipa, alitataa kumsamehe na akamtupa gerezani.

Bwana mkubwa aliposikia jambo hili, alikasirika na akaagiza yule aliyesamehewa deni aletwe, akamwambia “hukuweza kumhurumia ndugu yako kama mimi  nilivyokuhurumia wewe? (Mt 18:33). Ndipo akaamuru huyu jamaa atupwe ndani hata atakapolipa ile deni yote. Yesu akahitimisha akisema “Ndivyo baba yangu wa Mbinguni atakavyomtendea kila mmoja wenu kama msipowasamehe ndugu zetu kutoka mioyoni mwenu” (Mt 18:35).

Baba Mtakatifu anasema, mfano huu umesheheni mafundisho mazito kwa ajili yetu sote. Yesu anathibitisha kwamba, tunaitwa kuonesha huruma kwa wenzetu kwa sababu Mungu mwenyewe ametuonesha kwanza huruma sisi wenyewe. Tunapohurumia na kusamehe, ndipo haswa tunajionesha kuwa ni watoto wa Mungu. Baba Mtakatifu anakaza kusema “kwetu sisi Wakristo kusamehe ni amri ambayo hatuwezi kuigeuzia shingo pembeni”. Wakati fulani kusamehe kunaonekana ni kugumu sana, lakini ni chombo kilichowekwa katika mikono yetu dhaifu kwa ajili ya kutupatia amani moyoni, kwani kwa njia ya kusamehe tunaiachilia mbali mchemko wa hasira, chuki, kisasi. Ni kwa njia ya kuhurumia na kusamehe tu, tutaishi kwa furaha.

Asante kwa kuitegea sikio Radio Vatican, tusikilizane tena kipindi kijacho. Kutoka katika Studio za Radio Vatican, ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.