2015-05-22 06:44:00

Wafanyakazi katika sekta ya afya saidianeni, ili mhudie kwa moyo mkuu!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne jioni tarehe 19 Mei 2015, amekutana na kuzungumza na ujumbe kutoka Hospitali ya Muniz, huko Buenos Aires, Argentina na kuwataka wahudumu wa afya kuhakikisha kwamba, wanasaidiana na kuhudumiana kwa ukamilifu zaidi, ili waweze kutoa huduma bora zaidi kwa wagonjwa na wale wote wanaohitaji msaada wao. Baba Mtakatifu anawapongeza kwa huduma kwa ajili ya wagonjwa na kwamba, anaendelea kuwasindikiza kwa njia ya sala na sadaka yake, ili kuendelea kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu.

Ujumbe wa watu 48 kutoka Argentina ni wa wafanyakazi wanaotekeleza dhamana na wajibu wao katika hospitali 34 kutoka Buenos Aires. Wajumbe hawa wamewasilisha kadi na salam kutoka Argentina, zinazoonesha: matumaini, mahangaiko na changamoto wanazokabiliana nazo. Baba Mtakatifu amepokea zawadi mbali mbali kutoka Argentina naye akawapatia zawadi ya vitabu vikiwa na baraka zake za kitume, vitabu ambavyo vitawekwa hospitalini mjini Buenos Aires.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.