2015-05-22 16:12:00

Mwenyeheri Sr. Irene Stefani alikuwa ni Mama mwenye huruma na mapendo


Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 23 Mei 2015 anatarajiwa kumtangaza Mtumishi wa Mungu Sr. Irene Stefani kuwa Mwenyeheri, katika Ibada ya Misa Takatifu itakayofanyika Jimbo Katoliki la Nyeri, Kenya. Sr. Irene Stefani ni mtawa aliyejitahidi kumwilisha upendo katika maisha yake kwa watu aliokutana nao. Huu ni upendo ambao uliwagusa na kuacha chapa ya kudumu katika maisha ya watu.

Hivi ndivyo anashuhudia Sr. Salesia Mugaya wa Shirika la Consolata katika mahojiano maalum na Radio Vatican, kutoka Jimbo Katoliki la Nyeri ambako, tayari Kanisa linajiandaa kwa ajili ya kumtangaza Mtumishi wa Mungu Sr. Irene kuwa Mwenyeheri. Ni mtawa ambaye ubinafsi hakuwa na nafasi hata kidogo katika maisha yake, akaonesha mshikamano wa umoja na upendo kwa watu wote pasi na ubaguzi, hii ndiyo changamoto kwa watu katika ulimwengu mamboleo.

Mwenyeheri mtarajiwa Irene alijisadaka kama muuguzi, akawahudumia watu kwa mapendo, kiasi cha kuyamimina maisha yake kwa kuambukizwa na ugonjwa wa Tauni wakati akimhudumia Mwalimu Julius Ngalya. Alikuwa ni mpishi mzuri, kiasi kwamba, wengi walifurahia chakula chake; alikuwa ni Mwalimu bora aliyefundisha kwa mfano wa maisha yake, akasimama kidete kuimarisha tunu msingi za maisha ya kifamilia kwa kukazia mawasiliano kati ya wazazi na watoto wao waliokuwa wanaishi Nairobi.Wengi wanamkumbuka kuwa ni Katibu muhtasi wa maskini na wale wasiojua kusoma wala kuandika. Sr. Irene Stefani alikuwa ni Mama mwenye upendo na huruma kama walivyomwita “Nyaatha”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.