2015-05-22 07:33:00

Kitim tim! Roho Mtakatifu amewasha moto! Cheche zake zimeenea kote!


Ndugu yangu, tunaposherehekea Pentekoste, tunaongozwa na Injili kama ilivyoandikwa na Yohane: Yoh. 15:26-27; 16:12-15: Hapa leo kuna kazi kweli kweli! Roho Mtakatifu amewasha moto na cheche zake zimeenea duniani kote!

“Mbingu ni mbingu za BWANA, bali nchi amewapa wanadamu.” (Zab. 115:16). Ama kweli sisi ndiyo “wananchi” na dunia ndiyo nyumba na makazi yetu. Madirisha na milango ya nyumba hiyo ikifunguliwa hewa safi inaweza kuingia na kuburudisha waliomo. Hewa chafu au upepo vyaweza pia kuingiza vumbi na takataka zinazochafua nyumba. Milango na madirisha ya nyumba vikifungwa nyumbani mnakuwa na giza au kukosa hewa. Hata hivyo taa zinaweza kuwashwa na kuleta mwanga au moto unaweza kupasha nyumba joto. Makao na makazi hayo ya binadamu yaweza pia kuwa mwili na uhai wa mtu mwenyewe.

Wakati mwingine nyumba hiyo inashikwa na nguvu za giza la matatizo mengi yanayosababishwa na mtu mwenyewe au na wengine. Watu walioko katika ulimwengu ulio giza la utawala mbovu, umaskini, utengano, kinzani na magomvi,  daima wanakaa kusubiri labda wanaweza kumpata kiongozi atakayewapa mwanga wa maisha, yaani kiongozi atakayewaletea mwongozo, katiba au sera zinazowapa watu mwanga wa maisha bora zaidi kuliyo yalivyokuwa jana!. Kinyume chake wananchi wanaishia kuhadaika na sera za uwongo wanazoahidiwa zinapokosa kulingana na ahadi za viongozi hao.

Sikukuu ya leo tunasherekea Mwanga halisi utokao mbinguni na unaoangaza ulimwengu mzima. Mwanga huo unaoangaza ni Roho mtakatifu, aliye “Roho wa ukweli.” Roho tuliyeahidiwa ni yule anayeshuhudia Kristo yaani ushuhuda unaofanya kazi ndani ya moyo wa mtu anayesadiki (mkristo), roho inayoendana pamoja na dhamiri. Mtu mwenye roho safi anatoa ushahidi wa kweli. Kinyume cha ukweli huo siyo uwongo, kwani uwongo ni hali ya kidhahania au ya kufikirika, kumbe, Roho wa ukweli anaozungumzia Yesu una maana ya uhalisia. Mathalani, mtu mwonevu, mtu mwovu, mtu mdanganyifu, mlaghai, mwizi, mla rushwa, fisadi huyo kwa lugha ya kawaida “si mtu.” Kumbe, mtu halisi ni yule anayependa, mtu mkweli, mtu wa haki, huyo “ndiyo mtu,” tena mtu halisi. Waswahili husema "wengine wanaokena kama watu lakini ni soli ya kiatu"! Maneno hayo!

Ni ngumu sana kuipata lugha ya kibinadamu ya kumweleza ipasavyo huyo Roho wa kweli aliyetuahidi Yesu mfufuka. Hebu tuyaachie Maandiko Matakatifu yatusaidie kuelezea maana ya Roho wa kweli tunayebidi kumfuata. Kuna alama yapata nne zilizotajwa katika masomo ya leo zinazoweza kueleweka kirahisi, alama zinazodhihirisha uwepo wa Roho wa kweli. Alama hizo ni nyumba, upepo, moto na lugha (neno).

Alama ya kwanza ni nyumba: “Siku ile ya kwanza ya juma pale walipokuwa wanafunzi milango imefungwa kwa hofu ya wayahudi.” Milango iliyofungwa yaonesha kulikuwa na nyumba. Humo walikuwa mitume na wafuasi wa Yesu pamoja na Maria. Tunaweza kuilinganisha na nyumba yoyote ile linamoweza kukusanyika kundi la watu. Yaweza kuwa nchi au ulimwengu ulio makazi ya wananchi. Kadhalika nyumba hiyo yaweza kuwa mimi tena ndani kabisa ya mimi mlimo uhai, maisha na makazi yangu. Ndani ya nyumba hiyo ndimo anaingia Roho wa kweli. Roho huyo lakini anaingia katika nyumba walimo wafuasi wa Yesu na kufanya makao yake. Humo Roho anajisikia kuwa nyumbani au makaoni mwake. Roho huyo ni kama upepo unaoijaza na kuenea humo nyumbani. Ndani ya kila nyumba kunahitajika kuwa na Roho wa ukweli.

Alama ya pili ni upepo: “Kukaja ghafla toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote.” Kazi ya upepo ni kuvuma na kuipuliza nyumba, upepo unaweza kujaza nyumba na baadaye ukatoka nje kupitia mlangoni, madirishani au kipenyo chochote kile. Hivi unaingia ndani ya nyumba na hata kupitiliza na kuvuma kwenda unakotaka, kwani upepo uko huru. Upepo unapeperusha vumbi na hata kusafirisha mbegu ndogondogo, yaani unabeba uhai wa mbegu na kuzipeperusha sehemu nyingine zitakakoweza kumea. Kadhalika upepo unahamisha takataka, vumbi na vitu visivyoweza kuhamishika yaani unasafisha.

Taswira hii ya upepo unavyovuma na kuhamisha vitu toka pahala pamoja hadi pengine, ni sawa na hali ya mitume wanaoacha nyumba zao, na kwenda kuhubiri au kupanda mbegu ya Injili katika miji mingine, huko wanakutana na watu wanaowashangaa, kwani mitume hao wanatumia lugha inayowafanya watu wawaulize maswali ya msingi. Hiyo ni kazi ya Roho mtakatifu ni kama upepo. Ukifunga milango na madirisha na kushughulika na nyumba yako tu huwezi kuangaza ulimwengu, kumbe Roho Mtakatifu anataka tufungue milango na madirisha ili tuweze kuangaza ulimwengu mzima. Roho Mtakatifu anatufanya tupanue uwanja wa kufikiri. 

Pale unapoishia wewe, ndipo yanaanza maisha yasiyo na mwisho kama anavyosema Yesu: “Kuna mambo mengi bado ya kuwaeleza, lakini kwa sasa hamtaweza kustahimili lakini atakapofika mfariji atawaeleza ukweli wote,” yaani siyo mwanga na ukweli uliofungwa bali “ukweli uko mbele zaidi,” nami ninahusika na mradi ulio wazi mbele yangu, ya kwamba Mungu ni kama bahari mpya, ambayo jinsi mtu anavyoenda na kusukumwa na upepo akiongozwa na Roho anagundua uhalisia wa mambo. Ama kweli upepo utakusukuma matanga ili jahazi liende mbele hadi kieleweke!

Alama ya tatu ni moto: “Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao.” Roho anawasha moto fulani ndani mwetu pale palipo baridi na pamezima moto wa upendo, haki, msamaha, na wa kutotamani maisha, hapo Yeye anawasha mwali wa upendo, wa tabasamu, mwali wa kusamehe, kadhalika anawasha hali ya kupenda maisha. Roho ndiyo anayewasha na kulipusha mioyo yetu tuwamo katika safari refu ya maisha kama wale wanafunzi wawili wa Emaus waliowashwa na moto wa Roho hata wakasema: “Je, mioyo yetu haikuwaka pale barabarani alipokuwa anatuelezea Maandiko?” (Lk 24:32). Tunaweza daima kujiwasha mioyo yetu kwa moto wa Roho wa ukweli aliye moto usiozimika.

Alama ya nne ni Lugha au Neno: “Wote wakajazwa na Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka.” Mara nyingi, tunaposoma au tunaposikiliza Injili tunaweza kuguswa moyoni. Hilo ni tendo la Roho Mtakatifu. Neno la Mungu linagusa maisha yangu, mashaka yangu, ndoto zangu  na matatizo yangu. Hivyo ndivyo malaika alivyomwambia Maria: “Roho Mtakatifu atakufikia na kukupa Neno” (Lk 1:35). Yesu aliwaambia wanafunzi wake: “Roho mtakatifu atafika na kuwapa maneno yangu” (Yoh. 14:26).  Kwa “lugha nyingine” yaweza kumaanisha, lugha ya upendo, lugha ya haki, lugha ya huruma kinyume na lugha iliyozoeleka ambayo ni ya chuki, wongo, dharau na kashfa.

Leo tumwombe Roho mtakatifu awashe upendo ndani mwetu, upendo unaotia joto, upendo usio na woga; aumbe mwanga, atupe hekima ya moyo, yaani tuwe na moyo unaogusa, unaosukuma na kutia joto undani wa maisha yetu; atuletee zawadi nzuri ya moyo uliowaka; upepo wa uhuru unaopuliza matanga ya jahazi dogo la moyo wangu.

Ndugu yangu ninapenda kuhitimisha tafakari hii ya Siku kuu ya Pentekoste kwa kuonjesha „Single” bado inapikwa, lakini unaweza kuonja utamu wake, ili iweze kuwa ni sala inayoyasindika maisha yao kama mwamini na shuhuda wa ukweli katika upendo!

“Upumue ndani yangu Ee Roho Mtakatifu – Nipate kuyawaza matakatifu,Unisukumize Ee Roho Mtakatifu – Nipate kuyatenda matakatifu, Univute kwa utamu Ee Roho Mtakatifu – Nipate kuyapenda matakatifu, Uniimarishe Ee Roho Mtakatifu – Nipate kuyatunza matakatifu, Unitunze Ee Roho Mtakatifu – Nisije nikayapoteza matakatifu. Amina”

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.