2015-05-22 08:28:00

Huduma msingi za afya zipewe kipaumbele cha kwanza na Jumuiya ya Kimataifa


Shirika la Afya Duniani, WHO, kuanzia tarehe 18 hadi tarehe 26 Mei 2015 linafanya mkutano wake mkuu huko Geneva, Uswiss na unahudhuriwa pia na Askofu mkuu Zygmunt Zimowski, Rais wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya wafanyakazi katika sekta ya afya ambaye katika hotuba yake, aliyoitoa hapo tarehe 20 Mei 2015 amekazia umuhimu wa kuwa na miundo mbinu bora ya afya ili kukabiliana na magonjwa pamoja na majanga ya maisha katika ngazi mbali mbali; jambo ambalo linahitaji mshikamano wa kimataifa. Anasema, huduma msingi za afya, zinapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza na Jumuiya ya Kimataifa.

Askofu mkuu Zimowski anabainisha kwamba, nchi changa duniani zinakabiliwa na uhaba wa huduma makini za afya kutokana na ukosefu wa watalaam, vifaa tiba, taarifa pamoja na ufinyu wa bajeti. Changamoto zote hizi zinahitaji mikakati ya muda mrefu na mfupi unaowajumuisha wadau na serikali mbali mbali katika kukabiliana na changamoto za afya na ubora wake kama ilivyojitokeza wakati wa mlipuko wa ugonjwa wa Ebola, ambao umesababisha maafa makubwa kwa baadhi ya nchi kadhaa Afrika Magharibi.

Uwekezaji wa muda mrefu katika sekta ya afya unafumbatwa katika mafunzo makini kwa wafanyakazi katika sekta ya afya; uwepo wa dawa na vifaa tiba; miundo maalum ili kukabiliana na milipuko ya magonjwa; usahihi wa takwimu, bajeti ya kutosha pamoja na miundo mbinu ya huduma kwa wagonjwa katika ngazi mbali mbali. Ni changamoto kwa wafadhili kuwa na mwelekeo mpya wa kufadhili mipango na mikakati ya muda mrefu, kuliko hali ilivyo kwa wakati huu.

Takwimu za afya kimataifa zinaonesha kwamba, watu wanaoishi vijijini wanakabiliwa na hali ngumu zaidi katika kupata huduma za afya na kwamba, wengi wao wanakabiliwa na umaskini kutokana na ukata, changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inalivalia njuga tatizo hili kwa kuliweka katika Malengo ya maendeleo kimataifa baada ya mwaka 2015, kwa kutambua na kuheshimu maisha ya mwanadamu ambayo ni matakatifu na yanapaswa kuendelezwa. Hii ni sehemu ya utekelezaji wa haki msingi za binadamu.

Ujumbe wa Vatican kwenye mkutano huu unapenda kukazia ubia kati ya huduma zinazotolewa na Serikali pamoja na watu binafsi katika sekta ya afya hasa katika Nchi zinazoendelea. Lengo ni kuwahudumia wananchi wengi hasa wale wanaoishi vijini. Kanisa Katoliki ni kati ya wadau wakuu wa huduma za afya vijijini na kwamba, ina miliki na kuendesha zaidi ya vituo vya afya 110, 000 sehemu mbali mbali za dunia. Ni vyema ikiwa kawa Kanisa pia litasaidiwa kutekeleza dhamana hii nyeti kwa wananchi wengi wanaoishi vijijini; watu ambao wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha.

Askofu mkuuZygmunt Zimowski, mwishoni, amewakumbuka waathirika wa ugonjwa wa Ebola huko Afrika Magharibi pamoja na wafanyakazi katika sekta ya afya waliojitosa kimasomaso kwa ajili ya kutoa huduma kwa wagonjwa wa Ebola huko Afrika Magharibi, licha ya changamoto na utata uliokuwa umetanda katika huduma hii nyeti. Anawakumbuka na kuwaombea wale wote waliofariki dunia kutokana na ugonjwa wa Ebola na kwamba, ujumbe wa Vatican unaunga mkono ushauri uliotolewa kuhusu mapambano dhidi ya Ebola unaojadiliwa, ili hatimaye, uweze kupitishwa wakati wa mkutano mkuu wa 68 wa Shirika la Afya Duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.