2015-05-21 09:45:00

Mtumishi wa Mungu Sr. Irene Stefani kutangazwa Mwenyeheri, Jimboni Nyeri


Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 23 Mei 2015 anatarajiwa kumtangaza Mtumishi wa Mungu Sr. Irene Stefani kuwa Mwenyeheri, katika Ibada ya Misa Takatifu itakayofanyika Jimbo Katoliki la Nyeri, Kenya. Hili ni tukio la pekee kabisa kwa Familia ya Mungu katika nchi za AMECEA, Mama Kanisa anpoadhimisha Mwaka wa Watawa Duniani, wanaohamasishwa kutafakari yaliyopita ka moyo wa shukrani; kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini.

Mwenyeheri mtarajiwa Sr. Irene Stefani, aliyejulikana kama Mercede Stefani alizaliwa kunako tarehe 22 Agosti 1891 huko Brescia, Kaskazini mwa Italia. Kunako mwaka 1911 akajiunga na Shirika la Wamissionari wa Consolata na tarehe 12 Januari 1912 akavishwa vazi la kitawa katika hatua ya Unovisi na tangu wakati huo, akaanza kujulikana kama Sr. Irene.

Tarehe 29 Januari 1914 Sr. Irene akaweka nadhiri zake na mwishoni mwa mwaka huo akafunga vilago kuelekea nchini Kenya, ili kushiriki kikamilifu katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina, unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Ni mtawa aliyejisadaka kwa ajili ya huduma katika sekta ya elimu na afya, akawa ni muasisi wa shule na hospitali nyingi zilizoanzishwa na Wamissionari kwa wakati huo. Wakati wa Vita kuu ya Kwanza ya Dunia kati ya mwaka 1914 hadi mwaka 1920 alitoa huduma ya tiba kwenye Hospitali za kijeshi, kwa kuwasaidia wagonjwa na majeruhi wa Vita kuu ya Kwanza ya Dunia.

Katika shida na mahangaiko ya watu wakati wa Vita kuu ya Kwanza ya Dunia, Sr. Irene akiwa bado mtawa kijana kabisa, alitumia muda wake kwa ajili ya kuwahauudmia wagonjwa waliokuwa wanalazwa Voi, Kenya, Kilwa na Dar es Salaam Tanzania, ndiyo maana Familia ya Mungu kutoka AMECEA inamshukuru Mungu kwa upendo na ukarimu uliofumbatwa katika huduma ya Sr. Irene Stefani. Alitumia muda wake kwa kuwaganga na kuwaponya wagonjwa; kwa kufunga majeraha pamoja na kugawa chakula.

Sr. Irene alianza awamu ya pili ya maisha yake kati ya mwaka 1920 hadi mwaka 1930, akiwa Gekondi, akajikita katika kutoa huduma ya elimu. Aliwafunda wasichana waliokuja kujiunga na Shirika la Wamissionari wa Consolata; akawaonesha upendo na huruma ya kimama. Aliendelea kuwasindikiza watoto wake katika maisha ya kiroho kwa njia ya barua, licha ugumu na changamoto kubwa zilizokuwepo wakati ule.

Hawa ni watawa ambao walitumwa kutekeleza dhamana yao huko Nairobi na Mombasa, nchini Kenya. Akajenga mahusiano mazuri na familia za wasichana hawa ambao wengi wao walibahatika kuingia katika maisha ya utawa. Wakati alipokuwa anaendelea kuwahudumia wagonjwa wa tauni, akaambukizwa ugonjwa huo na hatimaye, kufariki dunia hapo tarehe 31 Oktoba 1930, akiwa na umri wa miaka 39 na kati ya miaka hiii yote, miaka 18 alifanya utume wake nchini Kenya. Huyu ndiye mtumishi wa Mungu Irene Stefani anayetarajiwa kutangazwa kuwa Mwenyeheri na Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Jimboni Nyeri kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.