2015-05-20 08:30:00

Uchumi mpya wa tabianchi ukumbatie mafao ya wengi na ekolojia ya binadamu


Chuo Kikuu cha Kipapa cha "Santa Croce" kilichoko mjini Roma, tarehe 20 Mei 2015 kumefanyika kongamano la kimataifa ambalo limeongozwa na kauli mbiu “Uchumi mpya wa tabianchi”, tukio ambalo limeandaliwa na Ubalozi wa Holland mjini Vatican. Kongamano hili limefunguliwa kwa hotuba iliyotolewa na Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani pamoja na Bwana Felipe Calderòn, Rais mstaafu wa Mexico ambaye kwa sasa ni Rais wa Tume ya Kimataifa kuhusu uchumi na tabianchi. Kardinali Donald Wuerl, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Washington DC, Marekani ameshiriki pia.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Kardinali Turkson amekazia kwa namna ya pekee umuhimu wa kuzalisha bidhaa kwa ajili ya huduma; umahiri wa kuratibu kazi, ili kutoa fursa za ajira sanjari na kukuza vipaji na karama za wafanyakazi; kuzalisha utajiri unaopaswa kutumika kwa haki na kwa ajili ya mafao ya wengi pamoja na kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu.

Wazalishaji wanapaswa kuhakikisha kwamba, wanazalisha mazao na bidhaa kwa ajili ya mafao ya wengi na kuepukana na kishawishi cha kutafuta faida kubwa,  na wakati mwingine kuchangia katika uharibifu wa mazingira. Ndiyo maana Jumuiya ya Kimataifa inahamasishwa kuhakikisha kwamba, inadhibiti uzalishaji wa hewa ya ukaa ambayo kwa sasa imekuwa ni tishio kubwa kwa maisha, ustawi na maendeleo ya binadamu.

Kardinali Turkson anasema mchakato wa shughuli za kiuchumi hauna budi kujikita pia katika ujenzi wa mshikamano na maskini pamoja na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi, maskini wataendelea kudidimia katika umaskini wa hali na kipato. Jitihada za pamoja za kutaka kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi ni jambo muhimu kwa ajili ya mafao ya wengi, utu na heshima ya binadamu.

Utajiri unaozalishwa katika mchakato wa uchumi hauna budi pia kuwasaidia wengine kwa kutumia kanuni auni inayopania ustawi na maendeleo ya wengi kwa kutoa fursa kwa watu mbali mbali kutumia karama na vipaji walivyojaliwa na Mungu kwa ajili ya maendeleo yao. Rasilimali fedha, watu, ardhi na mazingira hazina budi kutumiwa vyema kwa ajili ya mafao ya kizazi cha sasa na kile kijacho, kwa kuzingatia kanuni za maendeleo endelevu. Faida inayozalishwa isaidie pia kukuza utunzaji bora wa mazingira.

Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI aliwahi kuonya kwamba, ikiwa kama faida itapewa kipaumbele cha kwanza, hapo haki inaweza kuwekwa rehani, kumbe kuna haja ya kuendeleza majadiliano kwa kuwa na maamuzi ya kidemokrasia kwa ajili ya mafao ya wengi. Mafundisho Jamii ya Kanisa yanakazia pamoja na mambo mengine maendeleo endelevu yanayojikita katika mshikamano unaosimamiwa na kanuni auni. Kila mtu anapaswa kuwajibika katika kulinda na kutunza mazingira.

Kardinali Donald Wuerl, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Washington DC., anasema kwamba, kuna uhusiano mkubwa kati ya kazi ya uumbaji, utu na heshima ya binadamu, changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kusoma alama za nyakati, ili kuweza kutoa majibu muafaka. Mama Kanisa amepembua kwa kina na mapana kuhusu maendeleo endelevu ya watu, utunzaji bora wa mazingira pamoja na maendeleo ya sayansi na teknolojia yanayopaswa kuwa ni vichocheo vya ustawi wa Familia ya binadamu.

Mama Kanisa anapenda kuchangia katika majadiliano ya kimataifa kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kukazia umuhimu wa kujikita katika kanuni maadili; utu na heshima ya binadamu na mafao ya wengi. Kuna haja ya kulinda na kuendelea kazi ya uumbaji. Uchafuzi wa mazingira, ukataji wa miti ovyo, ukuzaji wa jangwa, uhaba wa maji, ukosefu wa makazi maalum pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi ni mambo ambayo yanaathari kubwa katika maisha ya binadamu.

Kardinali Donald Wuerl anasema kwamba, utunzaji bora wa mazingira hauna budi kwenda sanjari na ukuaji wa uchumi unaozingatia ekolojia ya binadamu. Vichocheo vya uchumi lazima viratibiwe na kanuni maadili, hekima na busara pamoja na kuangalia mafao ya wengi yanayojikita katika haki.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.