2015-05-20 14:54:00

Kanuni maadili, mshikamano wa kidugu na mafao ya wengi ni muhimu sana!


Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuwa macho na mikakati ya uchumi ya muda mrefu na mfupi sanjari na kufanya tafakari ya kina kuhusu maana ya uchumi na malengo yake; mfumo wa maendeleo unaofaa kwa ajili ya mafao ya wengi; kwa kuzingatia ekolojia ya binadamu pamoja na kutoa kipaumbele cha kwanza kwa kanuni maadili ili kukabiliana na changamoto za kumong’onyoka kwa maadili katika ulimwengu mamboleo.

Ni changamoto inayotolewa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI katika Waraka wake wa kitume, Upendo katika ukweli, Caritas in veritate. Ni ujumbe mahususi hasa wakati huu Jumuiya ya Kimataifa inapoendelea kujadili kuhusu mikakati ya uchumi mpya wa tabianchi, katika kongamano la kimataifa lililoandaliwa na Ubalozi wa Uholanzi mjini Vatican na kuwashirikisha viongozi mashuhuri kutoka ndani na nje ya Kanisa; kongamano ambalo limefanyika, mjini Roma, kwenye Chuo kikuu cha Kipapa cha “Santa Croce”, Jumatano tarehe 20 Mei 2015.

Udhibiti wa tabianchi unaweza kwenda sanjari na ukuaji wa uchumi endelevu. Huu ndio ujumbe ambao Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anapenda kuwashirikisha wajumbe wa kongamano hili kama sehemu ya maandalizi ya mkutano wa kimataifa juu ya mabadiliko ya tabianchi utakaofanyika mjini Paris, Ufaransa, Desemba, 2015. Lengo ni kuiwezesha Jumuiya ya Kimataifa kuwajibika zaidi kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Kardinali Parolin anabainisha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inaweza kupata suluhu ya kudumu ya matatizo na changamoto za mabadiliko ya tabianchi ikiwa kama itashikamana na kufanya maamuzi ya pamoja kwa ajili ya mafao ya wengi; kwa kuheshimiana na kuthaminiana, ili kujenga utamaduni wa mshikamano, watu kukutana na kujadiliana, tayari kusimama kidete kulinda na kutetea mazingira na familia ya binadamu katika ujumla wake.

Hapa hakuna tena nafasi ya kuendekeza utandwazi usioguswa na mahangaiko ya watu wala uchumi unaowatenga na kuwabagua watu. Maendeleo ya sayansi na teknolojia yawe ni kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi, kwa kubainisha sera na mikakati itakayosaidia kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi katika medani mbali mbali za maisha;  kwa kupambana na umaskini, ili kukuza na kudumisha utu na heshima ya binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.