2015-05-20 07:35:00

Jubilei ya miaka 75 ya huduma na uaminifu kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Jumanne, tarehe 19 Mei 2015 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumbu kumbu ya Jubilei ya Miaka 75 ya huduma ya Watawa wa Shirika la Orioni kwenye Posta ya Vatican. Ibada hii imehudhuriwa na viongozi waandamizi kutoka Vatican pamoja na wanashirika la Waorioni. Katika mahubiri yake, Kardinali Parolin amemtaja Mtakatifu Luigi Orione kuwa ni hazina kubwa ambayo Mwenyezi Mungu amelipatia Kanisa lake.

Mtakatifu Orione aliyezaliwa katika mji maskini wa Pontecurone, ulioko nchini Italia, akaishi katika hali ya umaskini wa kutupwa, lakini kwa neema na baraka zake Mwenyezi Mungu akafanikiwa kuanzisha Shirika ambalo leo hii limechanua sehemu mbali mbali za dunia na linatoa huduma za kichungaji kwa ajili ya mafao na ustawi wa wengi. Aliwasaidia wengi kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu, kwa njia ya upendo na ushuhuda wa maisha yake.

Mtakatifu Paolo alikuwa ni mfano bora wa kuigwa katika maisha na utume wa Mtakatifu Luigi Orione, kiasi cha kuchuchumilia utakatifu wa maisha kama dira na mwelekeo wa shughuli zake za kitume. Alionesha upendeleo wa pekee kwa ajili ya malezi na makuzi ya vijana maskini. Alijitahidi kuhakikisha kwamba, anamwilisha matendo ya huruma katika mikakati na shughuli zake za kichungaji, kiasi cha kuwa kweli ni mtume wa upendo kwa maskini na wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Kwa njia hii akawavuta watu wengi kwa Kristo na Kanisa lake.

Kutokana na juhudi zilizofanywa na Mtakatifu Luigi Orione, leo hii kuna Mashirika ambayo yameanzishwa na yanaendelea kutoa huduma za shughuli za kichungaji ndani ya Kanisa. Baada ya Vita kuu ya Kwanza ya Dunia, alianzisha mji ambao ulikuwa unatoa huduma kwa maskini na wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Huduma hii ya upendo wa Kristo ikamwilishwa kwa namna ya pekee nchini Italia, Amerika ya Kusini, Uingereza, Albania na kuendelea sehemu mbali mbali za dunia.

Kardinali Parolin anabainisha kwamba, Mtakatifu Orione alikuwa na Ibada ya pekee kwa Bikira Maria; kiasi cha kujenga Madhabahu makubwa kwa heshima ya Bikira Maria. Alionesha utii wa pekee kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, kiasi cha watawa wake kuweka nadhiri ya nne ya Uaminifu kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro; kielelezo cha umoja na mshikamano wa Kanisa. Kunako mwaka 1904 Katiba ya Shirika ikatamka bayana kwamba, Shirika linalenga kusaidia kujenga na kukuza umoja miongoni mwa Wakristo waliokuwa wametangana.

Ni kutokana na ubunifu, sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya ustawi na mafao ya Kanisa, kunako mwaka 1904, watawa wa Orione wakapewa dhamana ya kuongoza na kusimamia Parokia ya Mtakatifu Anna iliyoko mjini Vatican. Kunako mwaka 1940 wakapewa pia dhamana ya kutoa huduma kwa Posta ya Vatican, kazi ambayo wameifanya kwa weledi na umakini mkubwa, kiasi cha kupongezwa na wengi. Miaka 75 ya huduma ni kielelezo cha uaminifu kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro na neema ya Mungu kwa ajili ya Kanisa lake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.