2015-05-19 07:42:00

Simameni kidete kupinga rushwa na ufisadi unaowanyanyasa watu wengi!


Maaskofu wanapaswa kuwa ni sauti na watetezi wa wanyonge ndani ya jamii; Kanisa lisimame kidete kufichua rushwa na ufisadi unaowatumbukiza maelfu ya watu katika umaskini na kukata tamaa; nyaraka za Maaskofu ziguse maisha na mahitaji ya watu mahalia; waamini walei wajengewe uwezo wa kushuhudia na kumwilisha imani yao katika matendo kama sehemu ya mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu na kwamba, waamini wajiandae kikamilifu kwa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Haya ni kati ya mambo msingi ambayo Baba Mtakatifu Francisko amewashirikisha Maaskofu Katoliki Italia, CEI katika mkutano wao wa 68 uliofunguliwa, Jumatatu jioni, tarehe 18 Mei 2015, unaotafakari juu ya waraka wa kitume Injili ya Furaha, “Evangelii gaudii uliotolewa na Baba Mtakatifu Francisko. Baba Mtakatifu anawaalika Maaskofu kuwa kweli ni mashuhuda wa furaha na faraja inayobubujika kutoka kwa Yesu Kristo Mfufuka.

Maaskofu wawe tayari kuwasaidia, kuwatia shime na kuwasindikiza wale wote wanaoelemewa na Msalaba wa maisha bila ubaguzi, kwani wao kimsingi wao wanapaswa kuwa ni chumvi ya dunia na mwanga wa mataifa; dhamana wanayopaswa kuitekeleza kwa: hekima, unyenyekevu, huruma na mapendo; ili kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu kwani hiki ndicho kielelezo makini cha upendo wa Kristo unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika Maaskofu kusimama kidete kwa kuonesha mwamko wa Kikanisa unaopania kupambana kufa na kupona na saratani ya rushwa na ufisadi katika maisha ya hadhara na binafsi; ugonjwa ambao unasababisha majanga makubwa katika maisha ya wananchi wengi. Rushwa na ufisadi vimezitikisa familia, watu walioko kwenye pensheni, wafanyakazi waaminifu na waadilifu; Jumuiya za Kikristo; imewakatisha tamaa vijana, kiasi cha kukosa matumaini kwa siku za usoni; lakini mbaya zaidi, rushwa na ufisadi vimewatenga maskini na wahitaji zaidi. Kama wachungaji wema wanapaswa kutoka kimasomaso ili kuwatetea Watu wa Mungu dhidi ya mambo yote yanayotaka kudhalilisha utu wao kama binadamu.

Baba Mtakatifu Francisko anawataka Maaskofu wanapoandika nyaraka na barua zao za kichungaji ziangalie kwa upana zaidi Familia ya Mungu wanayoingoza na wala si kwa ajili ya makundi ya watu wachache ndani ya jamii. Hii ni changamoto ya kuwajengea waamini walei uwezo, ili kuwajibika barabara katika medani mbali mbali za maisha, tayari kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko.

Kuna haja kwa Kanisa kujenga na kudumisha umoja na mshikamano kati ya Maaskofu wenyewe; kati ya Maaskofu na Mapadre wao. Mshikamano huu ujioneshe pia kati ya majimbo tajiri na maskini; kwa kushirikishana rasilimali fedha na watu. Umoja na mshikamano uendelezwe kati ya Mabaraza ya Maaskofu na hatimaye na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Tayari kuna udhaifu ambao unajionesha katika Mabaraza ya Maaskofu kwa kukosa umoja na mshikamano katika mambo msingi kama vile mikakati ya shughuli za kichungaji; katika masuala ya kiuchumi na fedha: Hapa Maaskofu wanapaswa kumwchia nafasi Roho Mtakatifu ili awaoneshe dira na njia ya kufuata.

Baba Mtakatifu anawataka Maaskofu kusaidia mchakato wa kupyaisha maisha na utume wa watawa kutokana na matatizo na changamoto mbali mbali wanazokabiliana na zo kwa sasa, kiasi hata cha kushindwa kutoa ushuhuda wa utambulisho wao kama Wakristo na Kanisa. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Familia ya Mungu itafanikiwa kumwilisha huruma ya Mungu kwa kuwapatia watu wa nyakati hizi faraja.

Mara baada ya hotuba ya utangulizi iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, kilifuatia kipindi cha majadiliano ya faragha kati ya Baba Mtakatifu na Maaskofu. Waandishi wa habari, wakafunga vilago na kuondoka ukumbini, lakini Baba Mtakatifu amewashukuru kwa huduma yao makini kwa ajili ya Familia ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.