2015-05-19 15:47:00

Mchakato wa diplomasia ya Vatican unapania kujenga haki, amani na upendo


Kardinali Dominique Mamberti, Mwenyekiti wa Mahakama kuu ya Kitume, gwiji katika masuala ya kidiplomasia ya Vatican anabainisha kwamba, Kanisa linapenda kudumisha mchakato wa haki, amani na utulivu, kwa kuzimisha moto wa machafuko, kinzani na vita kwa maji ya baraka, amani na utulivu. Ni mchakato wa majadiliano ya kidiplomasia unaojikita katika kubainisha mbinu mkakati wa mawasiliano, vikwazo na vizingiziti vinavyoweza kujitokeza pamoja na kuunda mazingira ya kuaminiana na kuthaminiana, ili kuendeleza majadiliano.

Kardinali Mamberti anasema kwamba, changamoto kubwa iliyoko mbele yao kama viongozi wa Kanisa ni kutoka katika ubinafsi wao, tayari kuanza kujisadaka kwa ajili ya kulitumikia Kanisa kwa furaha, kwani wao kimsingi ni wahudumu wa Injili ya Furaha; tayari kuwashirikisha wale ambao wamekata tamaa, wenye huzuni na watu ambao hawaoni tena maana ya maisha.

Kutoka katika undani wao, kuna maanisha, kuachana na utekelezaji wa majukumu, maisha na utume wa Kanisa kwa njia ya mazoea pengine na fahari zake, tayari kushiriki kikamilifu katika mchakato wa ujenzi wa umoja na mshikamano ndani ya Kanisa; kwa kutaabikiana na kusumbukiana katika maisha; changamoto makini inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa kutambua kwamba, Kanisa, kwa asili ni la kimissionari, linatumwa kuwatangazia watu Injili ya Matumaini.

Kardinali Mamberti anakiri kwamba, haki ni nguzo msingi katika mchakato wa kujenga na kudumisha amani. Kanisa linapaswa kuwa ni kioo cha haki, “speculum iustitiae” mbele ya watu wa mataifa, lakini haki hii inapaswa kwanza kabisa kung’ra katika maisha na utume wa Kanisa. Mahakam kuu ya Kitume ina dhamana na wajibu wa kuhakikisha kwamba, inalisaidia Kanisa kutekeleza wajibu wake barabara, kwa njia ya ushuhuda makini.

Ulimwengu mambo leo unaendelea kushuhudia vita, kinzani na migogoro, Vatican kwa upande wake, inaendelea kutekeleza wajibu wake wa kidiplomasia, kwani haikumbatii masuala binafsi, bali inataka kusimamia mafao ya wengi, utu na heshima ya binadamu, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Kanisa linapenda kujenga madaraja ya watu kukutana, kushikamana na kushirikiana anasema Baba Mtakatifu Francisko.

Ni mchakato unaojikita katika majadiliano katika ukweli na uwazi, heshima na utu wa binadamu. Maboresho ya mahusiano kati ya Cuba na Marekani ni matunda ya uwekezaji wa muda mrefu ambao umefanywa na Vatican, kwa kuguswa na mahangaiko pamoja na mateso ya wananchi wa Cuba. Baba Mtakatifu yuko mstari wa mbele katika kutetea mafao ya wengi, lakini pia Mabalozi wa Vatican wanatekeleza dhamana yao moja kwa moja katika uwanja wa kimataifa.

Umaskini, vita, kinzani na migogoro ya kijamii sehemu mbali mbali za dunia ni matokeo ya mipasuko mikubwa ya kijamii, kuna kundi dogo la watu linalofurahia rasilimali na utajiri wa nchi wakati huo huo, kuna umati mkubwa wa watu wanaoteseka kutokana na umaskini wa hali na kipato. Misigano ya kidini ni kati ya mambo ambayo yanaendelea kuhatarisha amani, utulivu na maridhiano kati ya watu. Bara la Afrika linaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika ustawi na maendeleo ya dunia kutokana na Bara la Afrika kuthamini: uhai pamoja na kuwa na matumaini makubwa kwa siku za usoni.

Mashariki ya Kati anasema Kardinali Mamberti kwa sasa umekuwa ni uwanja wa fujo, vita na kinzani za kila aina. Wakristo ni kati ya makundi ya kidini yalioathirika vibaya zaidi. Suluhu ya mgogoro wa Mashariki ya Kati, kuna maanisha maridhiano kati ya Israeli na Palestina na Syria kwa upande mwingine. Jambo la msingi ni kujenga na kudumisha majadiliano kati ya wananchi wa Syria, Jumuiya ya Kimataifa, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mafao ya wengi pamoja na kushikamana dhidi ya vitendo vya kigaidi na biashara haramu ya silaha, ambayo imekuwa ni chanzo cha maafa makubwa ya watu na mali zao huko Mashariki ya Kati.

Kardinali Dominique Mamberti kuhusu utunzaji bora wa mazingira anabainisha kwamba, mkutano wa kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi utakaofanyika nchini Ufaransa, mwezi Desemba, 2015 ni fursa makini kwa Jumuiya ya Kimataifa kuwajibika kikamilifu, ili kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi. Hii ni dhamana ya kimaadili, kisiasa na kiuchumi inayohitaji ushirikiano na mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa, ili kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa inayotishia usalama na maendeleo ya binadamu wengi duniani. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kufanya maamuzi machungu kwani taarifa za wanasayansi zinaitaka Jumuiya ya Kimataifa kuwa na maamuzi ya pamoja, kwa ajili ya Familia ya binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.