2015-05-18 12:13:00

Mahujaji, waombeni watakatifu wapya ili amani ipatikane nchini Palestina


Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku kuu ya Kupaa Bwana mbinguni, Jumapili tarehe 17 Mei 2015 amewatangaza Wenyeheri Giovanna Emilia De Villenueve, Maria Alfonsina Danil Ghattas, Maria wa Yesu Msulubiwa na Maria Cristina Brando kuwa watakatifu; mwaliko kwa Wakristo kuwa kweli ni mashuhuda wa Yesu Kristo mfufuka hadi miisho ya dunia; kwa njia ya huduma kwa maskini na wote wanaoonewa na kunyanyaswa; mwaliko wa kuwa ni Ekaristi na sadaka safi kwa wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; madaraja ya majadiliano ya kidini kati ya Wakristo na Waislam.

Baba Mtakatifu Jumatatu amekutana na umati mkubwa wa Watawa wa Shirika la Wakarmeli, Watawa kutoka Mashariki ya Kati na Watawa wa Shirika la Rozari Takatifu waliofika mjini Vatican ili kushuhudia wenyeheri hao wanne wakitangazwa kuwa Watakatifu. Baba Mtakatifu anasema kwamba, ujumbe kutoka Palestina umeongozwa na Rais Mahmoud Abbas wa Palestina na kwamba, ndege iliyokuja kutoka Yordan, ilikuwa imesheheni umati wa watawa.

Baba Mtakatifu anawataka mahujaji hawa kusali na kuwaomba watakatifu kutoka Palestina, ili waweze kusaidia kuomba, hatimaye, vita inayoendelea nchini Palestina iweze kukoma na watu kuanza kujikita katika mchakato wa amani na udugu. Anawaomba kusali kwa ajili ya Wakristo wanaouwawa na kulazimika kuishi kama wakimbizi; Wakristo wanaoendelea kudhulumiwa kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Waendelee kusali ili mauaji ya kigaidi yakome kwani huu ndio ukweli ambao hauwezi kufumbiwa macho! Baada ya maneno haya, Baba Mtakatifu pamoja na mahujaji hawa walisali kwa ajili ya kuombea amani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.