2015-05-18 08:25:00

Huduma ya upendo ni chanda na pete katika maisha na utume wa Kanisa!


Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis limehitimisha mkutano wake mkuu wa XX kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyewataka wajumbe kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu pamoja na mafao ya wengi; kwa kumtangaza Yesu Kristo kuwa ni Bwana na Mwalimu.

Caritas haina budi kuhakikisha kwamba, inatenda na kutekeleza dhamana na wajibu wake mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa na kweli za Kiinjili, mambo ambayo yanapaswa kumwilishwa kwanza kabisa na viongozi pamoja na wafanyakazi wa Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki pamoja na kuendelea kushuhudia utambulisho wao kama Wakristo. Huduma inayotolewa na Caritas haina budi kuendana na jina hili, anasema Kardinali Parolin pamoja na kuendelea kujipyaisha katika imani, matumaini na mapendo.

Ulimwengu mamboleo unakabiliwa na changamoto mbali mbali za: kiuchumi, kisiasa, kijamii, kiutu na kimazingira; changamoto ambazo zinapaswa kuangaliwa na kupewa tafsiri kwa jicho la Yesu Kristo. Hii ni changamoto kubwa katika maisha na utume wa Kanisa na kwamba, waamini hawawezi kufumbia macho matatizo yanayoendelea kumwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo. Majanga asilia, vita, nyanyaso na madhulumu kwa misingi ya kidini ni mambo ambayo kwa sasa yanapamba kurasa za vyombo vya upashanaji habari. Hadi sasa changamoto hizi hazijapewa ufumbuzi katika misingi ya usawa na inayokubaliwa na wengi.

Kardinali Parolin anasema, Kanisa kwa upande wake linapaswa kutoa majibu mintarafu imani na Mafundisho Jamii ya Kanisa; tayari kukutana na kuwasaidia wale wanaoteseka: kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu Francisko anazungumzia umaskini na wala si maskini peke yake, katika shida na mahangaiko katika medani mbali mbali za maisha, nyuma yake kuna binadamu, anayepaswa kuangaliwa kwa jicho la upendo na huruma. Kwa njia hii, Mama Kanisa anaendeleza kazi ya ukombozi iliyoanzishwa na Yesu Kristo.

Huduma ya upendo haina budi kupata chimbuko na utimilifu wake katika maisha na utume wa Kanisa Parokiani, Jimboni na katika uwanja wa Kimataifa. Viongozi na wafanyakazi wa Caritas wanayo dhamana ya ushuhuda na unabii, ili kuonesha ukarimu unaotolewa na Mama Kanisa kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ikumbukwe kwamba, huduma ya upendo ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa, huwezi kutenganisha huduma ya Caritas na Kanisa. Huu ndio mwelekeo sahihi katika maisha na utume wa Caritas Internationalis.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.