2015-05-18 11:12:00

Askofu mkuu Rugambwa: Mnaalikwa kumfuasa Kristo, kutumikia na kuhubiri


Siku kuu ya Kupaa Bwana mbinguni ni tukio la mwisho la Yesu kwa mitume wake, na ni wakati huu Yesu alipoonekana akirudi mbinguni. Kupaa kuliwasadikisha wafuasi wa Yesu si tu kwamba, amefufuka bali pia alikuwa anashiriki utukufu wa Baba yake wa mbinguni, tukio ambalo liliwajaza wafuasi wa Yesu furaha kuu. Yesu alichukuliwa mwili na Roho Mbinguni na sasa anaketi upande wa kulia wa Baba. Huu ni mwaliko wa kukumbatia ukweli huu wa kiimani, ili kufuata nyayo za Yesu, kwa njia ya utumishi na ushuhuda unaomwilishwa katika ujenzi wa ufalme wa Mungu tayari kushiriki katika utukufu na maisha ya uzima wa milele.

Hii ni changamoto ambayo imetolewa Jumapili tarehe 17 Mei 2015, Siku kuu ya Kupaa Bwana mbinguni na Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu mwambata wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu na Rais wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa, wakati wa mahubiri kwenye Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuwaaga wanafunzi wanaohitimu masomo yao kutoka katika vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu mjini Roma, tayari kurejea tena nchini Tanzania kuendeleza utume na maisha ya Kanisa.

Askofu mkuu Rugambwa anasema, Yesu katika maisha yake ya hadhara alitangaza Habari Njema ya Wokovu na ujenzi wa Ufalme wa Mungu, uliompelekea hata akateswa, akafa na kufufuka kutoka kwa wafu. Leo Kanisa linaadhimisha Siku kuu ya Kupaa kwake mbinguni. Changamoto kubwa kwa Wakristo ni kuhakikisha kwamba, wanashiriki kikamilifu katika ujenzi wa ufalme wa Mungu, kwa kumtangaza Yesu Kristo, lakini zaidi kwa kumshuhudia kwa njia ya imani inayomwilishwa katika matendo, ili waapatia watu: imani, matumaini na mapendo Wakristo wanatumwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.