2015-05-16 08:48:00

Ujumbe wa Papa Francisko kwa Siku ya 49 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni


Mawasiliano katika familia: mazingira muhimu yanayowakutanisha watu katika majitoleo ya upendo, ndiyo kauli mbiu inayoongoza ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya Upashanaji Habari Ulimwenguni mwa mwaka 2015. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walitoa agizo kwa Mama Kanisa kusoma alama za nyakati, ili kukabiliana na changamoto za maendeleo ya sayansi na teknolojia katika ulimwengu wa mawasiliano ya jamii. Mwaka huu siku hii inaadhimishwa tarehe  17 Mei katika ngazi ya kimataifa.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, familia ni mahali muafaka pa mawasiliano kati ya watu, hapa ni mahali ambapo wanafamilia kwa ujumla wanajifunza kuwasiliana. Huu ni mwendelezo wa tafakari makini kuhusu familia kama ilivyochambuliwa wakati wa maadhimisho ya Sinodi maalum ya Familia n ani sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia itakayoadhimishwa mjini Vatican kuanzia tarehe 4 hadi 25 Oktoba 2015.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, tumbo la mama ni shule ya kwanza ya mawasiliano, kwani hapa mtoto tangu akiwa tumboni mwa mama yake anajifunza kuwasiliana na mama yake, kwa njia ya mguso na kusikilizana. Ikumbukwe pia kwamba, familia ni shule ya msamaha, kwani kwa mara ya kwanza katika maisha, mtoto anakutana na mama yake, mang’amuzi ya mawasiliano yanayofumbatwa katika maisha ya mwanadamu.

Ni katika familia mtoto anaanza kujifunza maneno na kuzungumza; ni mahali pa kwanza pa kujifunza kusali, hapa mawasiliano yanapata mwelekeo mpana katika maisha ya kidini. Hapa mawasiliano hayana budi kueleweka kuwa ni mchakato unaomwezesha mwanadamu kugundua na kujenga mahusiano na jirani zake. Hapa familia pia inakuwa ni mahali pa kukuza na kudumisha fadhila ya msamaha, kwa kupendana na kuheshimiana sanjari na kutambua mapungufu ya kila mwanafamilia, tayari kupokeana na kusaidiana kwa upendo.

Baba Mtakatifu Francisko anakiri kwamba, hakuna familia ambayo ni kamilifu, lakini hakuna sababu ya kuogopa kuwa na familia zinazojikita katika mchakato wa kutafuta ukamilifu, katika madhaifu na mapungufu yanayojitokeza; hata wakati ambapo kunawepo na migogoro na kinzani; hapa wanafamilia wanapaswa kujifunza kukabiliana na changamoto zote hizi kwa ukomavu na mwono unaopania  kujenga na kudumisha tunu msingi za maisha ya kifamilia.

Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu anasema msamaha ni mwendelezo wa mawasiliano kati ya watu, hapa mtoto anajifunza kusikiliza na kuwaheshimu wengine, kwa kuonesha msimamo na kuchangia mawazo yake bila ya kumdhulu mwingine. Katika mwelekeo kama huu, watu wa namna hii watakuwa ni vyombo makini katika mchakato wa ujenzi majadiliano ya kina na upatanisho.

Baba Mtakatifu anazigeukia familia zenye watoto wenye ulemavu, hali ambayo inaweza kuwafanya wajifungie katika hali ya upweke hasi unaoweza kuwaletea madhara katika maisha; lakini kwa njia ya upendo unaomwilishwa katika maisha ya kifamilia kwa kukutana na kuzungumza na ndugu, jamaa na majirani, ulemavu unakuwa si tena mzigo bali daraja la kukutana na watu wengine, ili kushirikishana, kujengana na kuwasiliana kwa kushikamana. Shule, Parokia na Vyama vya kitume viwe ni mahali ambapo kila mtu anajisikia kuwa nyumbani na kwamba, hakuna mtu anayetengwa.

Baba Mtakatifu Francisko anabainisha kwamba, hata pale ambapo hakuna amani wala utulivu, familia zinaweza kuwa ni shule ya mawasiliano na baraka. Hali hii inaweza kujitokeza hata pale ambapo vita, chuki na uhasama vinatawala, lakini familia inaweza kuwa ni nguvu inayobomoa kuta hizi za utengano kwa kuondokana na chuki pamoja na hali ya kudhaniana vibaya na hapa familia inakuwa ni chombo cha baraka, kwa kutembeleana na kuonjeshana ukarimu, ili kuwa kweli ni mashuhuda kwamba, wema unaweza kupatikana kama njia ya kuwafunda watoto kujenga na kudumisha umoja na udugu.

Baba Mtakatifu Francisko katika Ujumbe wake kwa Siku ya Upashanaji Habari Ulimwenguni anavigeukia vyombo vya mawasiliano ya jamii, ambavyo ni jambo la msingi katika familia nyingi. Lakini vyombo hivi pia vinaweza kuwa kikwazo cha mawasiliano ndani ya familia na kati ya familia, kwa kushindwa kuwasikiliza na hatimaye, kujitenga na wengine. Kwa bahati mbaya, familia nyingi bado zinajikuta zikigonga mwamba katika mchakato wa mawasiliano.

Lakini, familia zikijibidisha zaidi zinaweza kutumia mawasiliano ya kijamii kuwashirikisha wengine mawazo na mang’amuzi yao, huku wakiwa wameungana; wanaweza kushukuru na kuombana msamaha, kumbe, njia za mawasiliano ya kijamii zinaweza kuwasaidia watu kujenga madaraja ya kukutana na kusaidiana. Kwa njia hii, watu wanaweza kudhibiti na kuratibu mwingiliano wao na vyombo vya mawasiliano ya kijamii, kwa kuvitawala badala ya kuwa ni watumwa wa vyombo hivi.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika wanafamilia kutambua kwamba, familia ni mahali ambapo wanapaswa kuwaelimisha na kuwafunda watoto wao, huku wakisaidiwa na Jumuiya za Kikristo  kujenga na kudumisha mawasiliano bora, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu pamoja na mafao ya wengi. Watoto wafundwe vyema kutumia njia za mawasiliano ya kijamii kwa kuwa ni wazalishaji na watumiaji makini na kamwe wasiwe ni kama “dodoki” linalokusanya takataka zote za kijamii.

Vijana wawe na mwelekeo mpana unaotambua tofauti zilizopo na kutafuta njia ya kuwa na mwelekeo wa pamoja kwa ajili ya mafao ya familia. Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, familia si uwanja wa fujo na vurugu; mahali ambapo watu wanapambanisha sera na mikakati yao ya kisiasa bali ni mahali ambapo watu wanajifunza kuwasiliana kwa ukaribu zaidi katika mambo ambayo yanawaunganisha ili kuiwezesha familia kuwa ni jumuiya inayojikita katika mawasiliano.

Familia ni mahali pa mtu kujifunza kupokea na kuwamegea wengine tone la upendo; ni rasilimali kubwa katika jamii na wala si mzigo kama wanavyofikiri wengi mintarafu vyombo vya mawasiliano ya kijamii. Familia ni taasisi ambayo inapakwa “matope” na wengi kadiri ya vionjo vyao. Lakini hapa anasema Baba Mtakatifu, familia inapaswa kuwa ni mahali ambapo kila mtu anajifunza kupenda na kupendwa; kuwasiliana kwa njia ya ushuhuda wa uzuri, wema na utakatifu unaofumbatwa ndani ya familia, kwa njia ya mapendo kati ya bwana na bibi; kati ya wazazi na watoto wao.

Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku ya 49 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni kwa kusema kwamba,  mapambano haya si kwa ajili ya kuendeleza yale yaliyopita, lakini Kanisa linatekeleza yote haya kwa moyo wa uvumilivu na matumaini katika medani mbali mbali za maisha, ili kujenga matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.