2015-05-16 15:33:00

Rais Mahmoud Abbas wa Palestina akutana na Papa Francisko mjini Vatican


Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 16 Mei 2015 amekutana na kuzungumza na Rais Mahmoud Abbas wa Palestina ambaye, baadaye amekutana pia na kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.

Rais Abbas yuko mjini Roma kushiriki katika Ibada ya Misa Takatifu ya kuwatangaza Wenyeheri wawili kutoka Palestina kuwa watakatifu. Ibada hii ya Misa Takatifu inafanyika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 17 Mei 2015. Katika mazungumzo kati ya viongozi yao, wamegusia makubaliano yaliyofikiwa kati ya nchi hizi mbili kuhusiana na maisha na utume wa kanisa Katoliki nchini Palestina; Itifaki ambayo inatarajiwa kutiwa sahihi wakati wowote kuanzia sasa.

Viongozi hawa wamekita mazungumzo yao kuhusiana na mchakato wa amani kati ya Palestina na Israeli, kwa kuonesha matumaini kwamba, mazungumzo haya yataweza kuanza tena ili kupata suluhu ya kudumu ya mgogoro wa nchi hizi mbili. Ni matumaini yao kuwa Jumuiya ya Kimataifa, Waisraeli na Wapalestina wataweza kufanya maamuzi machungu kwa ajili ya kujenga na kudumisha amani. Mwishoni wamekazia pia umuhimu wa kuendeleza majadiliano ya kidini huko Mashariki, sanjari na mapambano dhidi ya vitendo vya kigaidi, vita na kinzani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.