Ijumaa 15 Mei 2015, Baba Mtakatifu Francisko alikutana na Maaskofu Katoliki toka Jamhuri ya Kati(CAR) , kama sehemu ya ziara yao ya kitume katika Kiti Kitakatifu. Katika hotuba yake kwa Maaskofu hao, alisisitiza kuboresha mazungumzo baina ya dini na imani mbalimbali, kama njia ya kujenga mapatano, ushirikiano na kusameheana kwa upendo, kwa jamii yao, iliyotumbukizwa katika dimbwi la chuki na vurugu.
Papa alitoa wito huo kwa Maaskofu wa CAR, kama jibu kwa maelezo ya Maaskofu wa CAR, juu ya hali halisi za maisha ya Kanisa na kijamii katika taifa la Afrika Kati ambalo kwa kipindi cha karibia miaka miwili, limeishi katika vurugu mbaya za kivita kati ya Waislamu na makundi ya Kikristo yaliyoasi na kuchukua silaha kupambana na Waislamu. Vurugu zilizo sababisha maelfu ya watu kuuawa na Mamilioni wengine, kulazimika kuhama makazi yao.
Baba Mtakatifu katika hotuba yake kwa Maaskofu kwa moyo wa kibaba na udugu, alionyesha
kujali mateso makubwa ya watu wa CAR, yanayotokana na utengano wa kidini na kimadhehebu.Na
alishukuru pia kwa juhudi zinazofanywa na Kanisa Katoliki, hasa katika kusaidia waathirika
wa unyanyasaji na wale waliokimbia makazi yao bila ubaguzi . Alionyesha kutambua
ugumu wa kazi za kitume na kichungaji kwa wakati huu. Lakini akasisitiza kwamba, wakati
chuki na vurugu vinapopamba moto , ni wakati kwa Wakristo, kutoa jibu la kwa upole,
msamaha na upendo wa Kiinjili. Papa alionyesha kujuta kwamba, bahati mbaya , jibu
hilo bado halijapata nafasi kwa mioyo mingi ya Wakristo, wanapopambana na ukatili
na matatizo ya nyakati , kama ilivyotokea huko CAR. Hivyo hii inakuwa ni ishara wazi
kwamba ,Injili bado kujipenyeza kwa dhati ndani ya mioyo ya watu kila mahali, kuwashawishi
mabadiliko huru chanya katika tabia za Wakristo.
Pamoja na hili, Papa pia aliwahimiza Maaskofu kutokatishwa tamaa na migogoro hiyo
lakini waendelee kupata mbadala katika njia ya imani na matumaini, kuleta upya hisia
za msisimko na mabadiliko, kupitia kazi zao za uinjilishaji. Na kwamba wao kama Maaskofu
wanao wajibu usiokwepeka katika utoaji wa shuhuda za kinabii, katika utendaji wa
kimaadili , kama msingi wa muhimu wa haki, ukweli na uaminifu msingi wa mchakato
wowote upya. Katika hali hii, pia aliwasihi waendelee na Juhudi zao, kuboresha mazungumzo
na amani, kupitia ukuzaji wa ushirikiano kati ya waamini wa dini mbalimbali na makabila,
akisema kufanya hivyo kutasaidia kuhamasisha maridhiano na mshikamano wa kijamii.
Pia Papa aligeukia suala la malezi ya Kikuhani, akisema kuna haja kutoa msisitizo
juu maana ya ubinadamu na upendo wa Kristo katika malezi Waseminaristi, kwa ajili
ya kujenga ufahamu wa kutosha juu ya maisha aminifu katika viapo vya useja, kwa kuwa
hakuna makubaliano mengine yanayoweza kukubalika kwa maisha ya Kipadre. Papa alihitimisha
hotuba yake, na maneno ya kutia moyo na msaada kwa ajili ya familia, akisema , familia
isisahaulike katika juhudi zao ziote kwa kuwa familia ni nafasi nzuri ya kujifunza,
na kutenda mazoezi utamaduni wote wa maisha ya kusamehe, amani na maridhiano, vipengere
vinavyohitajika sana katika taifa la Jamhuri ya Afrika Kati.
All the contents on this site are copyrighted ©. |