2015-05-15 14:06:00

Mshikamano na udugu ni amana bora katika mchakato wa maendeleo endelevu


Kardinali Oscar Andrès Rodriguez Maradiaga, Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa aliyemaliza muda wake katika hotuba yake ya ufunguzi kwa mkutano mkuu wa XX wa Caritas Internationalis anabainisha kwamba, Kanisa linaendelea kujikita katika ujenzi wa mshikamano wa umoja na udugu katika kukabiliana na changamoto mbali mbali za kitaifa na kimataifa, kwa kutambua kwamba, binadamu wote wanaunda familia moja ya Mungu, kumbe wanao wajibu wa kutunza na kuendeleza mazingira kwa ajili ya mafao na ustawi wa wengi.

Tema hii ni muhimu sana wakati huu Jumuiya ya Kimataifa inapojiandaa kwa ajili ya mkutano wa kimataifa kuhusu athari za mabadiliko ya tabia nchi unaotarajiwa kufanyika mjini Paris, Ufaransa, Desemba 2015. Jumuiya ya Kimataifa inataka pia kujipanga upya kwa ajili ya kujiwekea malengo ambayo yanapaswa kutekelezwa baada ya mwaka 2015.

Jumuiya ya Kimataifa inasubiri kwa hamu mchango wa Baba Mtakatifu Francisko katika utunzaji bora wa mazingira utakaobainishwa kwenye Waraka wake wa kichungaji kuhusu Ekolojia ya binadamu, unaotarajiwa kutolewa hivi karibuni. Ni waraka unojikita katika mwelekeo wa kimaadili na wala si katika masuala ya kisayansi, huo ni uwanja ambao kuna watalaam waliobobea huko. Ni mwaliko pia wa kuondokana na utamaduni usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu.

Baba Mtakatifu anawahamisha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujenga utamaduni wa upendo na mshikamano, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watu sanjari na kutetea utu na heshima ya binadamu. Vita, mateso, nyanyaso na dhuluma hidi ya Wakristo. Jumuiya ya kimataifa ijenge mshikamano pamoja na kuwasaidia maskini.

Dr. Michel Roy, Katibu mkuu  wa Caritas Internationalis anabainisha kwamba, Sudan ya Kusini imejiunga na Caritas na hivyo inakuwa ni nchi mwanachama wa 165. Mkakati wa Caritas kwa sasa ni kulielekeza Kanisa kujikita katika kuwasaidia na kuwahudumia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Padre Gustavo Gutierrez kwa upande wake anasema, umefika wakati kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumwilisha fadhila ya upendo katika uhalisia wa maisha, kwa kuguswa na mahangaiko ya watu kutokana na vita, majanga asilia, magonjwa, umaskini na njaa ili kujenga na kudumisha misingi ya haki na upendo inayojikita katika huruma. Hapa Kanisa linataka kutoa upendeleo wa pekee kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ushuhuda unaotolewa kwa namna ya pekee na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake. Kanisa linatambua na kuwathamini maskini, kwani hawa ni amana na kiini cha Injili.

Bwana Haridas Varikottil kutoka India anasema, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kutambua kwamba inaunda familia moja ya binadamu, kumbe inahamasishwa kushikamana katika mapambano dhidi ya baa la njaa na utapiamlo wa kutisha. Jambo  la msingi ni kuboresha uzalishaji katika sekta ya kilimo, ili kuhakikisha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inakuwa na uhakika wa usalama wa chakula. Ili kufikia lengo hili kuna haja ya kuwafundisha wakulima kujikita katika kilimo endelevu na rafiki kwa mazingira: kwa kulinda na kutunza mazingira pamoja na kuwa na matumizi safi na sahihi ya rasilimali ardhi, ambayo ni mtaji mkubwa kwa watu wengi duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.