2015-05-15 07:25:00

Burundi hali ni tete! Jikiteni katika majadiliano kuokoa maisha ya wengi


Baraza la Maaskofu Katoliki Burundi linaitaka Familia ya Mungu nchini humo kulinda na kudumisha amani na utulivu pamoja na kuendelea kujikita katika majadiliano katika ukweli, uwazi na mafao ya wengi, baada ya hali ya hewa kisiasa nchini Burundi kuendelea kuchafuka kutokana na jaribio la kutaka kuipindua Serikali ya Rais Peirre Nkurunziza kushindwa.

Watu wanaendelea kupoteza maisha na wengine wengi wameikimbia nchi yao kwa kuhofia usalama wa maisha na mali zao. Hakuna amani wala maridhiano kati ya wanasiasa wanaogombea Urais kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu nchini Burundi, ingawa, Umoja wa Afrika na Umoja wa Jumuiya ya Ulaya inaishauri Serikali ya Burundi kuhailisha uchaguzi, hadi pale amani na utulivu vitakaporejeshwa tena nchini Burundi.

Askofu mkuu Evariste Ngoyagoye wa Jimbo kuu la Bujumbura, Burundi katika mahojiano maalum na Radio Vatican anabainisha kwamba, kuna watu ambao wamekamatwa na wamewekwa kizuizini, matangazo katika vyombo vya habari yanaendelea kudhibitiwa na Serikali; mambo yote haya yanaonesha kwamba, uchaguzi mkuu hauwezi kufanyika katika mazingira ya haki, amani na utulivu.

Viongozi wa kisiasa hawana budi kuwatuliza mashabiki wao, ili amani na utulivu virejee tena Burundi, ambako bado wananchi wengi wana makovu ya vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo vilisababisha mpasuko mkubwa na mfungamano wa kitaifa. Kanisa linaitaka Serikali na vyama vya siasa kuhakikisha kwamba vinatoa majibu muafaka kwa hali tete inayoendelea kujitokeza nchini Burundi kabla ya mambo hayajaharibika sana.

Baraza la Maaskofu Katoliki Burundi kwa sasa linaendelea kusimamia mchakato wa uchaguzi mkuu kwa mwaliko kutoka kwenye Tume huru ya uchaguzi Burundi, ili kuhakikisha kwamba, kweli uchaguzi unakuwa: huru na wa kweli na kufanyika katika mazingira ya amani na utulivu. Ikiwa kama hakuna amani na utulivu, Kanisa litajitoa kusimamia mchakato wa uchaguzi mkuu nchini Burundi anasema Askofu mkuu Evariste Ngoyagoye.

Maaskofu wanasema kwa mara ya kwanza waliwataka wanasiasa kujikita katika majadiliano, ukweli, uwazi na mafao ya wengi, lakini hawakusikilizwa, ni matumaini yao kwamba, kutokana na hali tete ilivyo kwa sasa wataisikiliza sauti hii ya kinabii kwa ajili ya mafao ya wananchi wote wa Burundi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.