2015-05-14 11:37:00

Tafakari ya Neno la Mungu: Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni!


Mpendwa mwanatafakari wa Neno la Mungu, leo tunasherehekea sherehe ya kupaa Bwana. Ni sherehe ambayo huitangulia Sherehe ya Pentekoste. Ni sherehe ambayo Bwana wetu Yesu Kristu anapaa mbinguni akirudi kwa Baba yake na zaidi pia kwa sababu ya upendo wake mkuu kwa wanadamu wote anakwenda kutayarisha makao ya baadaye tutakapokaa na Baba baada yakuwa tumemaliza safari ya maisha yetu hapa duniani. Anachotaka tufanye kabla ya kupaa kwake anasema mkahubiri Injili kwa kila kiumbe, mkabatize na atakayeamini ataokolewa. Ujumbe huu tunaupata katika somo la Injili.

Kama tulivyokwisha sema sherehe ya Kupaa Bwana mbinguni huja siku kumi kabla ya Pentekoste, kumbe ni sherehe ya hitimisho la maandalizi siku 40 kwa Mitume wanapomsubiri Roho Mtakatifu, wanaposubiri kuanza kazi yao ya kitume. Kupaa ni kuingia katika utukufu wa Mungu na kuachana na kifungo cha kifo. Ni kutenganisha dunia yetu na Mungu na hasa ni kuwa karibu na Mungu. Kupaa ni onesho la utukufu wa Mungu, paleambapo Kristu anapomalizia kazi yake ya kitume ya hadhara hapa duniani. Pamoja na hilo kupaa kwa Bwana ni mwanzo wa kupanuka kwa utume wa Kanisa, tunapomsikia Bwana akiwaambia Mitume nendeni duniani kote mkaihubiri Injili.

Kupaa ni hitimisho la sehemu ya kwanza ya historia ya wokovu ambayo imetendwa na Bwana mwenyewe na anaanzisha kipindi cha pili ambacho kitaongozwa na Roho Mtakatifu. Ni katika kipindi hiki Mitume wataalikwa kumshuhudia Mungu wakiongozwa na huyo Roho wa kweli: Watamshuhudia katika kutangaza Neno, kuadhimisha sakramenti na kuweka chachu ya Injili katika ulimwengu mzima.

Kristo anapopaa anaingia katika utukufu wa Mungu, ni utukufu ambao hatuwezi kuugusa bali kwa njia ya imani tunaweza kuufikia. Utukufu huo tunaoweza kuufikia kwa imani na kwa matendo yetu mema unahakikishwa pale ambapo Bwana anawaambia Mitume wasitoke Yerusalemu hadi ahadi ya Baba yake itimie yaani ya kuwapelekea Roho Mtakatifu atakayewasaidia katika utume wao, yaani watatenda na kubatiza katika Roho Mtakatifu. Anawaambia watapokea Roho wa Mungu na watakuwa mashahidi katika Uyahudi na Samaria yote. (Mdo 1:8).

Mpendwa msikilizaji hata hivyo ujumbe huu si kwa ajili ya Mitume tu bali kwa ajili ya Kanisa zima, ndiyo kusema tuaalikwa kuitikia wosia wa Mungu daima ambao tunaupata kwa njia ya Neno lake na hasa kuwa mashahidi wa upendo kwa mataifa kama tulivyosikia dominika iliyopita.

Mtume Paulo anakazia imani katika Bwana anapowaandikia Waefeso anawakumbusha kuwa Kristu ni mfufuka na ni kichwa cha Kanisa ameketi kuume kwa Mungu na atawala falme zote za dunia. Anasema maisha yao hayafungwi na ulimwengu bali wanaalikwa kuishi katika tumaini la kumsubiri Kristu ajaye. Mpendwa nasi tunaalikwa pia kukumbuka si watu wa ulimwengu huu bali tukishafufuliwa na Bwana tunatazama yaliyo ya juu, tunaishi pamoja na Kristo.

Mpendwa, Bwana anapopaa kuna matukio ambata yanayotokea. Kwanza kuna watu wawili wenye nguo nyeupe, hawa ni wawakilishi wa utakatifu wa Bwana, ni alama ya uwepo wa Mungu pamoja na Kristu, kumbuka pale kaburini yule aliyekuwa amekalia jiwe! Maneno waliyoyasema hawa watu wawili ni ujumbe toka kwa Mungu, yafaa na ni lazima kuyatimiza. Linatokea wingu, hili latukumbusha safari ya Waisraeli kule jangwani wakitoka Misri, waliongozwa na Mungu kwa njia ya wingu, na hivi wingu ni ishara ya uwepo wa Mungu. Kut.13:22 Mitume na wengine yaani watu wa Galilaya wanatazama juu na kisha ujumbe unatoka ukiwaambia vivyohivyo alivyokwenda ndivyo atakavyorudi. Kutazama juu kadiri ya wanamaandiko ni kumwelekea Mungu lakini pia watukumbusha kuhangaikia upendo hapa duniani ili kutazama kwetu juu kuwe na mzizi wa upendo uliojaa wajibu wa huduma kwa walio na mahitaji.

Mpendwa shamrashamra za kupaa Bwana zinaambatana na wajibu wa kuhubiri injili kwa kila kiumbe kwa mataifa na kwa nguvu mpya ya Bwana. Na katika kuhubiri, mwinjili anatuhakikishia ukuu wa kusadiki kwamba hatutweza kudhuliwa na kitu chochote cha kufisha. Basi ni kwa jinsi hiyo nakualika unaposhangilia kupaa Bwana uweke nia ya pekee kwa ajili ya kazi ya kimisionari kwa njia ya sala na majitoleo mbalimbali katika familia na kanisa kwa ujumla.

Mpendwa nikutakie furaha na mapendo ukisubiri ujio wa Roho Mtakatifu Dominika ijayo.

Tumsifu Yesu Kristo. Tafakari imeletwa kwako na Pd Richard Tiganya C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.