2015-05-14 14:54:00

Familia ya Mungu nchini Bolivia inajiandaa kumpokea Papa Francisko!


Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kufanya hija ya kitume nchini Bolivia kuanzia tarehe 8 hadi tarehe 10 Julai 2015, habari ambazo zimewagusa wananchi wengi wa Bolivia. Baraza la Maaskofu Katoliki Bolivia limeanzisha kampeni ya upendo na mshikamano wa kidugu, ili kuchangia kwa hali na mali maandalizi ya ujio wa Baba Mtakatifu Francisko nchini mwao. Lengo ni kuhakikisha kwamba, Baba Mtakatifu anapata mapokezi mazuri kadiri ya uwezo wa wananchi wa Bolivia.

Padre Josè Fuentes, moja ya waratibu wa hija hii ya kitume nchini Bolivia anasema kwamba, Kanisa kimsingi ndiye mhusika mkuu katika maandalizi na hatimaye mapokezo ya Baba Mtakatifu Francisko, kwa kushirikiana na Serikali ya Bolivia pamoja na watu wenye mapenzi mema.

Waamini wanahamasishwa kuchangia ili kuliwezesha Kanisa kununua vifaa muhimu vya mawasiliano, vitakavyowawezesha waamini na watu wote wenye mapenzi nchini humo, kumsikiliza na kumwangalia kwa kutumia vyombo vya mawasiliano ya kisasa, kwani si wote watafanikiwa kuingia katika maeneo ambayo Baba Mtakatifu anatarajiwa kukutana na kuzungumza na makundi mbali mbali wakati wa hija yake ya kitume nchini Bolivia.

Kanisa Katoliki nchini Bolivia ni maskini na uwezo wake ni mdogo, kumbe linahitaji kutiwa shime na wasamaria wema, ili kufanikisha tukio hili la kihistoria katika maisha na utume wa Kanisa nchini Bolivia.

Baraza la Maaskofu Katoliki Bolivia, limezindua pia tovuti maalum itakayowawezesha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kufuatilia habari na matukio muhimu wakati wa hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Bolivia. Licha ya maandalizi haya ya kimwili, lakini kwa namna ya pekee, Maaskofu wanaliangalia tukio hili kama kielelezo cha neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kumbe wameandaa sala maalum ambayo waamini wameanza kusali kama sehemu ya mchakato wa maandalizi ya ujio huu.

Akiwa nchini Bolivia, Baba Mtakatifu atakutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali pamoja na wanadiplomasia; atasali na kuzungumza na Mapadre, Watawa, Wanovisi na Majandokasisi. Anatarajiwa pia kushiriki katika mkutano wa kimataifa wa vyama vya wananchi kutoka sehemu mbali mbali duniani. Atazungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Bolivia na baadaye atakamilisha hija yake ya kitume Amerika ya Kusini, tayari kurejea tena mjini Vatican kuendelea na maisha pamoja na utume wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.