2015-05-14 09:44:00

Changamoto za Caritas Afrika: Mauaji, wakimbizi, njaa na magonjwa


Baba Mtakatifu Francisko katika Ibada ya ufunguzi wa Mkutano mkuu wa XX wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis anasema kwamba, dunia inaweza kuzalisha chakula cha kutosha kwa Familia nzima ya Mungu, lakini kunakosekana utashi wa kujenga na kuimarisha mshikamano wa upendo na udugu, ili kupambana na baa la njaa duniani. Caritas ni wahudumu wa Injili na kwamba, upendo ni sehemu ya vinasaba vya Kanisa katika huduma kwa binadamu. Caritas wanapotekeleza dhamana na wajibu wao, watambue kwamba, wao ni mashuhuda wa Kristo, wanaotumwa kuwahudumia watu wote bila ubaguzi.

Kanisa linaendelea kuwakumbuka, kuwaombea na kuwasaidia Wakristo wanaoteseka na kunyanyasika kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, sehemu mbali mbali za dunia. Maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii ndio walengwa wakuu wa huduma ya upendo inayotolewa na Mama Kanisa sehemu mbali mbali za dunia.

Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Barani Afrika, limehitimisha mkutano wake mkuu uliofanyika mjini Roma hivi karibuni kwa kuongozwa na kauli mbiu: Upendo wa Kristo unatuwajibisha. Mkutano huu umehudhuriwa na wajumbe 100 kutoka katika Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM. Askofu Francisco Joao Silota, Rais wa Caritas Afrika anabainisha kwamba, Caritas inakabiliwa na changamoto za: Mauaji, nyanyaso na madhulumu dhidi ya Wakristo; Ongezeko kubwa la wahamiaji, wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi maalum kutokana na vita, kinzani na migogoro ya kisiasa, kidini na kikabila inayojitokeza Barani Afrika; Umaskini; Baa la Njaa, Magonjwa hususan: Ebola na Ukimwi.

Caritas Afrika inatekeleza dhamana na majukumu yake katika nchi 46 katika Parokia 17, 000. Kanisa Barani Afrika kwa sasa linataka kujielekeza zaidi katika mchakato wa uhakika wa usalama wa chakula; kwa kusaidia maboresho ya shughuli za kilimo na lishe; kuwajengea uwezo wanawake ili waweze kushiriki kikamilifu katika ustawi na maendeleo ya familia na jamii inayowazunguka pamoja na kuendeleza maboresho katika sekta ya afya, ili kweli Familia ya Mungu Barani Afrika, iweze kuwa na afya bora, tayari kuchangia katika mchakato wa maendeleo endelevu.

Baada ya mkutano wa Caritas Afrika, ulihitimishwa kwa wajumbe kuchagua Kamati ya Caritas Afrika inayoundwa na wajumbe kutoka Ghana, Congo Brazzaville, Madagascar na Lesotho. Itakumbukwa kwamba, wajumbe kutoka Caritas Afrika kwa sasa wanaendelea kushiriki katika mkutano wa Caritas Internationalis unaoendelea hapa mjini Roma.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.