Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ametangaza rasmi kuwa Tanzania itafungua Ubalozi katika Algeria, kwa nia ya kuimarisha mahusiano thabiti ya kirafiki na ya kihistoria tokea yalipoanzishwa na waanzilishi wa mataifa hayo, Hayati Julius Kambarage Nyerere na Hayati Ahmed Ben Bella.
Nayo, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Algeria imeipongeza Tanzania na Rais wake, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, kwa jitihada zake za kusaka amani na utulivu katika Bara la Afrika kupitia michakato mbali mbali ya usuluhishi kama vile wa Sudan Kusini. Aidha, Algeria imepongeza na kukaribisha ushiriki makini wa Tanzania na majeshi yake katika shughuli za kulinda amani katika Darfur (Sudan), Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Lebanon.
Pongezi hizo zilitolewa, Jumapili, Mei 10, 2015 mjini Algiers na Rais Abdelaziz Bouteflika wa Algeria kwa Rais Kikwete wakati wa mazungumzo rasmi kati ya Tanzania na Algeria, ikiwa ni sehemu ya ziara rasmi ya Kiserikali ya siku tatu ya Rais Kikwete katika Algieria. Ziara hiyo imemalizika, Jumatatu, Mei 11, 2015. Naye, Rais Kikwete ametangaza uamuzi huo wa kufungua Ubalozi wa Tanzania katika Algeria , Jumapili, Mei 10, 2015 katika mazungumzo yake tofauti na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Algeria, Mheshimiwa Abdelaziz Bouteflika na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Mheshimiwa Abdelmalek Sellal.
Rais Kikwete alikutana na viongozi hao, ikiwa ni sehemu ya ziara yake rasmi ya Kiserikali ya siku tatu na yenye mafanikio makubwa ambayo ameifanya Algeria kwa mwaliko wa Rais Bouteflika. Ziara hiyo ilimalizika, Jumatatu, Mei 11, 2015. Ziara hiyo ya Rais Kikwete na uamuzi wake wa kuwa Tanzania inafungua Ubalozi katika Algeria, ambayo kwa sasa inahudumiwa na Ubalozi wa Tanzania ulioko mjini Paris, Ufaransa, inathibitisha utayari wa Tanzania na Algeria kuimarisha mahusiano ya kirafiki, kindugu na kiutengamano kama walivyotaka waanzilishi wa uhusiano huo.
Katika mazungumzo yao, viongozi hao walipata nafasi ya kutathmini upya mafanikio katika maeneo ambako Tanzania na Algeria zinashirikiana ambayo ni pamoja na elimu, nishati, madini, biashara, viwanda na hata kuangalia jinsi gani nchi hizo mbili zinavyoweza kuimarisha ushirikiano katika kilimo.
Viongozi hao wamewataka mawaziri wa nchi zote mbili wanaohusiana na sekta hizo kukutana haraka iwezekanavyo, kuangalia kwa ndani zaidi jinsi ya kuimarisha maeneo hayo. Aidha, viongozi hao wamewahamasisha wafanyabiashara wa nchi hizo mbili kuangalia jinsi ya kuanzisha mahusiano ya kibiashara kati ya Tanzania na Algeria. Viongozi hao pia wametaka Tume ya pamoja ya nchi hizo mbili kukutana haraka kujadili jinsi gani ya kuimarisha uhusiano katika sekta mbali mbali.
Rais Kikwete na Rais Bouteflika pia wamejadili masuala mengine ya kimataifa, ya kikanda ya Kiafrika na hasa migogoro mbali mbali na athari za vikundi vya kigaidi, ambavyo vinatishia utulivu wa Afrika na ustawi wa wananchi wake, kama vile Boko Haram katika Nigeria na nchi za jirani yake. Viongozi hao pia wameelezea wasiwasi wao mkubwa na kuongezeka na kusambaa kwa vikundi vya kigaidi, kuongezeka kwa biashara ya dawa haramu katika Afrika na kuongezeka na kusambaa kwa silaha haramu katika nchi mbali mbali za Afrika, mambo ambayo yanatishia kuvuruga jitihada kubwa za maendeleo
Viongozi hao pia wamejadili hali ya Mali na Libya na Rais Kikwete amepongeza juhudi kubwa zinazofanywa na Algeria katika kusuluhisha hali katika nchi hizo mbili pamoja na kuunga mkono jitihada zinazoendelea kufanywa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Mheshimiwa Ban Ki Moon katika suluhisho la haki na la haraka katika mgogoro wa Jamhuri ya Watu wa Sahrawi – SADR (Western Sahara). Wamesema kuwa suluhisho la haki ni wananchi wa SADR kupewa haki ya kuamua mambo yao wenyewe kupiga kura ya maoni.
Na mwandishi maalum.
All the contents on this site are copyrighted ©. |