Baba Mtakatifu Francisko Jumanne jioni tarehe 12 Mei 2015 aliongoza Ibada ya Misa kwa nia ya kufungua Mkutano Mkuu wa XX wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki,” Caritas Internationalis”. Ibada hii ilifanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro na ilihudhuriwa na wajumbe wa Mkutano huu Mkuu wa Caritas Internationalis, kutoka pande zote za dunia. Kati ya Ajenda muhimu za mkutano huu, ni pamoja na kupitisha Mbinu mkakati wa kufanyia kazi na Bajeti kwa ajili ya miaka minne ijayo.
Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake, alikiri kwamba , Utume wa Caritas , kwa hakika ni ushuhuda wa kweli kwa mafundisho ya Yesu Kristo . Chombo hiki Katoliki kwa ajili misaada ya ubinadamu na maendeleo , huonyesha nguvu ya upendo wa Kristo na hamu ya kanisa katika kumfikisha Yesu kwa kila binadamu , na hasa kwa watu maskini na wanaoteseka.
Baba Mtakatifu alieleza hayo kwa kutafakari ujumbe wa somo kutoka Matendo ya Mitume, aya zinazoeleza miujiza, iliyowatokea Paulo na Sila walipokuwa wamefungwa gerezani . Jinsi Bwana alivyowatendea maajabu, na jinsi mtu anaye sikiliza Neno la Bwana toka kwao, alivyookoka na kuchukua hatua muhimu, katika njia ya kuelekea imani na wokovu. Mtu huyo na familia yake , walilisikiliza Neno kutoka kwa Paulo na Sila , na maisha yao kubadilika. Mtu huyo aliguswa na mateso ya Paulo na Sila na kuwahudumia kwa upendo mkuu, kuyasafisha madonda na majeraha yao, na kuwakaribisha nyumbani kwake, na familia nzima kuwa na furaha kamili.
Aidha Baba Mtakatifu alirejea somo la Injili, linalohimiza kuosha miguu na madonda ya wale walio katika mateso na dhiki na kuandaa meza ya chakula kwa ajili yao, akisema hii ni ishara ya unyenyekevu , katika kulikubali Neno na Sakramenti ya ubatizo kwamba daima huandamana na ukarimu , huduma na kupokea wengine. Utendaji wote huu umefungamana pamoja na kuwa na maana moja tu kwamba ni kumkaribisha Mungu na wengine. Ni kuwapokea wengine kwa neema ya Mungu; kumkaribisha Mungu kwa kielelezo cha huduma kwa ndugu zetu wake kwa waume. Neno, Sakramenti na huduma , inakuwa kwa ajili ya ustawi wa wote , kama shuhuda za tangu mwanzo wa Kanisa zinavyoeleza.
Papa alieleza na kugeukia utume wa Caritas, akisema katika kazi zake za kila siku, tunaona ishara ya wito mzima wa Caritas. Caritas ambayo kwa sasa ni asasi kubwa yenye kutambuliwa duniani kote, kutokana na mafanikio ya kazi zake. Papa, aliitaja huduma ya Caritas, kuwa ni ukweli wa Kanisa katika maeneo mengi ya dunia, na hivyo ni lazima iendelee kupanua huduma zake katika Parokia na jumuiya mbalimbali ambako bado kufika. Ni lazima kupeleka huduma hii katika parokia na jumuiya mbalimbali ambazo bado kufikiwa. Na ni lazima kufanya upya, utendaji wa kanisa, ili iwe kama ilivyokuwa katika siku zake za mwanzo wa Kanisa. Papa aliendelea kufafanua utume wa Caritas kwamba, kwa kweli, chimbuko la huduma ya Caritas ni fadhila za kawaida za kumpokea Mungu na jirani kwa utulivu. Na ukarimu huu unapaswa kuanzia ndani ya moyo wa mtu mwenyewe na kutoka kwenda nje, kwenda kuhudumu wengine katika Jina la Kristo , wote wale wanaokutana nao na wale watakaoendelea kukutana nao na wale watakaowaendea kama majirani. Papa alishukuru kwa hili lakini pia akaonya dhidi ya lengo lake kuu la kuinjilisha kusahaulika na Caritas kufanywa kama asasi ya kawaida la misaada ya kibinadamu.
Papa aliendelea kuonya kwamba , kila mhudumu wa Caritas, si mfanyakazi wa kawaida tu kama mtoa misaada, lakini anapaswa kuwa shahidi wa kweli wa Kristo. Ni lazima awe mtu anayeitafuta sura ya Kristo inayoonekana kwa wateswa na wahitaji , na kumruhusu Kristo kuingia kwake; ni mtu mwenye kuwa na upendo na roho ya Kristo, roho ya fadhila na tulizo.
Hivyo Papa akasisitiza , mipango na mikakati yote , ni lazima iandamane na upendo unaochipuka kutoka kwa Kristo mwenyewe , vinginevyo mikakati na mipango yote ya caritas inakuwa ni mipango tupu isiyokuwa na maana. Si kutenda kwa upendo wa kibinadamu bali kwa upendo wake yeye, upendo wa kusafishwa na kuimarisha upendo wa Kristo.
Kwa namna hiyo Papa alisema , kila mmoja anaweza kumtumikia mwingine , kuandaa
meza kwa ajili ya wote, kama Mungu alivyoiandaa meza ya Ekaristi, kwa wote na wakati
wote. Na kufikiri juu ya meza ya Ekaristi, tusisahau Wakristo wenzetu, wanaonyimwa
haki ya kushiriki katika furaha ya meza hii ya Ekaristi, kutokana na ghasia na vita.
Pia wale waliofukuzwa kutoka makazi yao na makanisa yao kuharibiwa . Papa alirudia
kukata rufaa upya ya kutosahaulika watu hao wanaoteswa na udhalimu usioweza vumilika.
Na alikamilisha homilia yake akisema ,Caritas , kama ilivyo pia kwa asasi zingine
za fadhila kwa upendo wa Kanisa, huonyesha nguvu ya upendo wa Kikristo na hamu ya
Kanisa kumfikisha Yesu kwa kila mtu, hasa wakati wale wanaoteswa na umaskini na dhuluma.
Hii ni njia iliyoko mbele ya kila Mkristo. Papa kwa mtazamo huo, alitumaini, ndiyo
kazi kubwa kwa kila mmoja kwa siku hizi. Na alikabidhi utendaji wote kwa kwa Bikira
Maria, katika kumkaribisha Mungu na jirani, kama msingi ya maisha Papa alieleza na
kukumbusha kwamba , Jumatano hii 13 Mei ni Siku Kuu ya Mama Yetu wa Fatima, aliyetokea
kutangaza ushindi dhidi ya maovu. Kwa msaada huo mkubwa , hakuna hofu katika kuendelea
na dhamira ya kanisa.
All the contents on this site are copyrighted ©. |