2015-05-13 12:05:00

Ameweza, huyoo! Nendeni sasa mkamshuhudie kwa vitendo!


Ameweza hee, ameweza hee, heee ameweza!” Hiki ni kibwagizo cha wimbo wa ushindi anaoimbiwa mshindi wa mashindano fulani. Leo wimbo huo anaimbiwa mshindi halisi wa maisha na wala si mwingine ni Yesu Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai! Fasuli katika Injili ya dominika ya leo ni tamati ya masimulizi ya safari ya miaka mitatu aliyofanya Yesu na wafuasi wake. Tungetegemea safari hiyo sasa inafikia mwisho na hivi tungekuwa tumeishiana na habari za Yesu. Kumbe mambo bado na ndiyo kwanza yanaanza upya. Tunakuta jopo la wafuasi wa Yesu linatumwa rasmi kuanza safari refu ya kuzunguka kila mahali ulimwenguni. “Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe.”

Injili maana yake Habari Njema, Taarifa ya Furaha, Breking nyuuzi. Jina Injili alipewa pia mtangazaji wa Habari Njema, kama vile kuzaliwa kwa mtoto wa Mfalme au kutawazwa kwa mfalme au mtawala mpya ambaye daima anatazamiwa kuwa mkombozi wa taifa mathalani mtu yule aliyefika kutangaza kurudi kwa Wayahudi toka utumwani aliitwa Habari Njema: “ni vyema miguu ya yule anayetangaza habari njema kwamba Bwana wako anatawala.” (Isa. 52).

 

Yesu ni Habari Njema ya furaha, kwani ndiye aliyethibitisha kwa maneno na matendo yake kwamba Mungu anatupenda bila masherti. Tunamwona, tunamsikia, tunamshuhudia Mungu huyo akitenda mema na maajabu katika Kristu. Kwa hiyo alichohubiri na kutenda Yesu Kristu ni Habari Njema, kadhalika kilichoandikwa juu yake (Injili) ni Habari Njema. Baada ya Yesu Kristu wanafuata wafuasi wake wanaotumwa kufanya kazi ya kumdhihirisha Mungu katika Kristu na ya kusikiliza Injili yake. Wafuasi wa Kristu na wale wote wanaoiamini na kuiishi Injili yake nao pia wanaitwa Habari Njema.

 

Wafuasi hao wa Yesu hawatumwi kueneza dini, bali wanatumwa kuiishi Habari Njema yaani, kuonesha kwamba Mungu anatupenda. Habari Njema hiyo itaubadilisha uumbaji wote na kuugeuza kuwa mpya. “Tuma Roho wako na vitaumbwa na uso wa nchi utakuwa mpya.” Waaminio na kuiishi hiyo Habari njema ya Kristo wanadhihirika kwa maweza au ishara wanazoonesha za kuubadili ulimwengu kama alivyoahidi Yesu mwenyewe: “Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio kwa jina langu.” Kuna ishara tano anazojaliwa Mkristo anayeisadiki Habari Njema na kuiishi kwa dhati. Ishara hizo siyo miujiza kama wanavyodhani wengine, kwani Yesu mwenyewe hakutenda miujiza ili kuonesha ubabe na sifa kwani alisema: “Kizazi hiki ni kibovu, hakitapata ishara yoyote ile zaidi kuliko ile ya Yona.” Miujiza haimfanyi mtu awe mpya, bali kuipokea na kuiishi Habari Njema ndiko kunakomgeuza mtu kuwa mpya hadi aweze kudhihirisha ishara hizo mbalimbali. Kutokana na ishara hizo mtu au kanisa linakuwa kioo au dirisha la Habari Njema.

 

Ishara ya kwanza “Watatoa pepo.” Hayo mapepo au mashetani siyo viumbe vya ajabu-ajabu vinavyoruka angani na kutisha, la hasha, bali ni binadamu. Watu hao wanazo nguvu za ushetani, nguvu za uovu, nguvu za uwongo na za uonevu, nk. Nguvu hizo za kifo, ni nguvu za giza, nguvu za majivuno, nguvu zinazotegemea mali, nguvu za ubinafsi. Nguvu hizo zinatugeuza kuwa mapepo na mashetani, kama alivyokuwa yule mgerasi aliyepagawa na lukuki ya mashetani akaishia kukaa peke yake makaburini (Mk.5:1-14). Mfuasi wa Kristu anaahidiwa kufukuza mapepo na mashetani. Kwa sababu ametumwa kuihubiri na kuiishi Habari Njema ya haki, ya matumaini, ya upendo, ya uhuru na amani.

 

Ishara ya pili “Wataongea lugha mpya.” Kuwa mkristu haimaanishi kuwa na uwezo wa kumung’unya lugha ngeni kama ya kichina, kifaransa au kiingereza kama wanavyojidai wanaopagawa na majini, bali mkristu ametumwa ulimwenguni, kuhubiri Habari njema. Lugha ya zamani tuliyozoea kuisikia ni ile ya kashfa, ya kubezana kidini, ya kutengana na kudharauliana kimakabila, kimataifa, lugha ya matusi. Baada ya lugha ya kukashfiana inafuata vita na kulipizana kisasi. Habari njema ni lugha mpya ambayo kabla yake haikuwapo. Lugha hiyo mpya inayozungumza ni lugha ya haki, lugha ya upendo, lugha ya uvumilivu, lugha ya utulivu siyo makelele, lugha ihusuyo utu wa mtu, lugha ya heshima na ya kupendana,  nk. Hii ndiyo lugha mpya wanayotumwa kuiongea wafuasi wa Kristo.

 

Ishara ya tatu, “Watashika nyoka.” Katika Maandiko Matakatifu, Kitabu cha Mwanzo, nyoka anatajwa katika sura ya kwanza ihusuyo uumbaji. Humo kitabuni nyoka ameoneshwa kuwa ni mnyama mwerevu, mwongo, mdanganyifu, mwenye hila, mlaghai, mwenye wivu kwa mtu mwenye raha na mwenye kufanikiwa. Nyoka anayejipenyeza kila mahali, na mshawishi mkuu wa binadamu. Nyoka huyo ni adui wa Mungu, na anakuingizia mawazo mabaya dhidi ya Mungu. Nyoka hao ni binadamu nao wako wengi ulimwenguni. Kumbe Habari Njema inatufanya tuwe ngangali na kutuepusha na nyoka hao. Mzaburi anatutuliza tusiwe na woga na maadui hao anaposema: “Utawakanyaga simba na nyoka, mwanasimba na joka utawaseta kwa miguu.” (Zab 91:13). Tuiamini Injili itakayotupatia nguvu dhidi ya nyoka wabaya.

 

Ishara ya nne “Wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa.” Kuna mambo mengi sana yaliyo kama sumu tukinywa yanaweza kutudhuru hata kutuua. Mathalani vyombo vya habari, ulimwengu wa kisasa na maendeleo yake, makwazo, vishwawishi, tamaa mbaya, nk. Lakini kama umepokea ulimwengu mpya wa Habari njema, ulimwengu huu wa kufisha hautatudhuru kamwe, yaani hatutaathirika nao na tutabaki ngangali. Ulimwengu huo utatuimarisha badala ya kukuponza.

 

Ishara ya tano, “Wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.” Magonjwa na kuumwa ni hali halisi ya udhaifu wetu hapa duniani. Maneno haya watapata afya kwa kigiriki ni kalôs héxousin, na maana yake ni “kujisikia vizuri, kujisikia ahueni au kutulizika” Kwa hiyo uponyi huo haumaanishi moja kwa moja uponyi wa mwili, bali yahusu kujisikia ahueni, yaani kitendo cha kuwawekea mikono kitawapa faraja wagonjwa na “watajisikia vizuri na kutulizika.” Kuweka mikono juu ya wagonjwa ni kuwapa Habari njema ya Yesu inayowasaidia kuelewa maana ya mateso. Injili hiyo inawapa wagonjwa amani na utulivu moyoni na mwilini. Ingawaje tunasadikishwa kwamba kuna maradhi au magonjwa mengine yaliyo sugu na yasiyoponyeka, lakini tunaweza pia kuwaganga wagonjwa namna hiyo hata kimwili. Kwa sababu ukweli ni kwamba mbele ya Mungu hakuna kisichoponyeka, au hakuna ugonjwa usiohitaji kuponywa, bora tu uwe pamoja Mungu na kumwaminia.

 

Baada ya kuzitaja ishara hizi zinazotanguzana na wanaoamini Habari njema “Yesu akachukuliwa juu mbinguni akaketi mkono wa kuume wa Mungu.” Taswira hii ya mkono wa kuume wa Mungu, inamaanisha ukuu anaopewa Yesu aliyefaulu kuuonesha uso wa Mungu ulimwenguni, yaani aliyefaulu kuishuhudia Habari Njema ya upendo wa Mungu kwa binadamu. Huyu ni Binadamu pekee aliyeweza. Sasa kazi hiyo wamepewa wafuasi wake na wanatulizwa. “Nao wakatoka, wakahubiri kotekote, Bwana akitenda kazi pamoja nao, na kulithibitisha lile neno kwa ishara zilizofuatana nalo.” (Mk. 16:20). Kuna mawazo mawili ya kuwatuliza wafuasi: mosi, “Bwana akitenda kazi pamoja nao”.

 

Kwa kigiriki maneno hayo yamefasiriwa kwa neno moja tu synegyountos kwa kiingereza ni synergy lenye maana ya kutia nguvu, au kutia tafu, yaani Bwana alifanya kazi pamoja nao, alikuwa nguvu yao akiwatia tafu. Katika kila tendo jema hata lingekuwa dogo namna gani, unapotoa neno jipya la uhai, hapo Yesu anatenda kazi pamoja nawe ndani mwako kwa amani akikutia tafu. Pili, “na kuthibitisha neno kwa ishara zilizofuatana nalo”. Neno yaani Injili na ishara zile zilizotajwa zinaenda sambamba. Kumbe hata sisi ametuwezesha hivi tunaweza kujiimbia: “Tumeweza!”

Kwa hiyo sikukuu ya kupaa Yesu mbinguni inaweza kuonekana kuwa Sikukuu tata, kwa kuwa Yesu ametuaga. Kumbe anaaga bila kuondoka. Haendi sehemu nyingine bali anatutangulia. Hayuko na kumbe, yuko nasi. Yuko karibu na yuko mbali. Yuko mbinguni na yuko pia ndani ya kila kiumbe. Yuko nasi tayari kutuwezesha! Ama kweli ni mshindi na tumwimbie “Ameweza huyoooo!  ameweza hee heee, ameweza!

 

Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.