2015-05-12 11:19:00

Papa; msiogope mateso na kifodini maana ni sehemu ya maisha ya Mkristo


 Baba Mtakatifu Francisco anasema,  ingawa Wakristo wanapambana na mateso,  dhuluma na hata kifo kwa jina la Mungu , Roho Mtakatifu anaendelea kuwatia nguvu katika kukabiliana na kifodini kilichoko mbele yao wakati wakiishuhudia imani yao. Papa alieleza Jumatatu  katika mahubiri ya Ibada ya Misa mapema Asubuhi, katika Kanisa dogo la Mtakatifu Marta mjini Vatican. Homilia ya Papa ilivuviwa na somo la Injili ya siku ambamo Yesu anazungumzia kuja kwa mtetezi, atakayemtuma kutoka  kwa Baba , Roho wa Ukweli anayetoka kwa Baba , atakaye mshuhudia na wao watamshuhudia. Papa alifafanua Yesu alikuwa akizungumzia hali ya baadaye ya msalaba wa mateso unaowasubiri wafuasi wake , na alizungumzia juu ya Roho Mtakatifu atakayekuwa msaada katika kutoa ushuhuda kama Wakristo.

Alisema, leo hii sisi sote, tuna ushuhuda kwa  wote wanaotumia jina la Mungu kuua Wakristo. Watu wanaoua Wakristo, kutokana na kutomjua Mungu, kulingana na imani yao. Wanafanya dhuluma hiyo kwa kuwa hawamjui Baba wala Mwana. Hilo ndilo linalo tokea hata Kristo , kama Yesu  alivyowaambia wafuasi wake, kinachotokea kwangu pia kitatokea kwenye -  kukataliwa ,mateso, dhuluma na misukosuko hata kuuawa, lakini msiogope  wala kutishika , kwa kuwa Roho Mtakatifu atawaongoza na kuwasaidia kuelewa nini maana ya mateso hayo. 

Baba Mtakatifu aliendelea kuyazungumzia mateso ya Wakristo ambao wamekuwa wakiteswa kwa sababu ya imani yao kwa Kristo , wanaoteswa eti tu kwa kuwa ni Wakristo. Waamini ambao hawatishiki wala kupoteza imani kwa kuwa wanatiwa nguvu na Roho Mtakatifu, na hivyo hawakomi kutaja jina la Yesu katika midomo yao hata wakati wa hatari za kifo. Huu ni ushuhuda wao. Ni ushuhuda wa kweli  wa kifo dini , ushuhuda wa ngazi ya juu kuliko shuhuda zote.

Papa anaendelea kusema, kwa Mkristo ambaye hayuko tayari kuishuhudia imani yake hata katika hali za vitisho vya mateso na kifo, vitisho vya mauti  katika maisha yake huyo bado hajaijua njia ya maisha iliyofundishwa na Yesu , njia ya kuyafia maisha kila siku , kwa ajili ya kutetea haki za watu wote, njia ya kutetea maisha ya watoto , wazazi baba na mama , wanaotetea familia zao , waamini wanaotembea katika njia ya mauti kwa ajili ya kuyatetea maisha ya wagonjwa wengine wanaoteseka kwa ajili ya upendo wao kwa Kristo. Sisi sote anasema Papa tunao uwezo wa kuiishi hali hii ya Pasaka katika njia ya kifo dini .

Papa alieleza hayo kwa kurejea katika somo la Injili ambamo Yesu anatangaza kwa wanafunzi wake juu ya Roho Mtakatifu , akisema, alikuwa na mengi ya kuwaambia lakini sasa hawana uwezo wa kuyabeba yote hadi hapo watakaposhukiwa na Roho Mtakatifu, atakayewaongoza katika ukweli wote. Bwana alikuwa akizungumzia siku za baadaye , juu ya maisha ya kuubeba msalaba na kwamba Roho Mtakatifu , atawaandaa kuwa mashahidi wa Kristo. Na hivyo alikuwa akizungumzia kashfa ya mateso , kashfa ya msalaba.

Maisha ya Kanisa aliendelea kueleza Papa, ni njia inayoongozwa na Roho Mtakatifu, mwenye kukumbusha juu ya mafundisho ya Yesu hata na yale ambayo Yesu hakuyataja. Roho Mtakatifu huwasindikiza waamini katika njia yao ya maisha na hata huwalinda na kuwatetea dhidi ya kashfa zinazotolewa kwao.

Aliendelea kuzungumzia hali hii ya mauaji dhidi ya Wakristo , akirejea pia mazungumzo yake  na kiongozi Mkuu wa Kanisa la Kikoputiki la Kiotodosi la Alexandria , Papa Tawadros II, mazungumzo ya siku ya Jumapili kwa njia ya simu, ambamo Papa Francisko aliwakumbuka Wafuasi wa Kanisa la Kikoputiki la Kiotodosi ambao hivi karibuni waliuawa katika mwambao wa Libya kutokana na Imani yao . Walichinjwa kama Kuku na watu wanaotumia jina la Mungu kufanya mauaji ya kinyama.  Papa amewataja waamini hao  kwamba, walikuwa na ushupavu wa imani ulioongozwa na Roho Mtakatifu , na hivyo mateso na kifo havikuwatisha , bali waliendelea kusimama imara katika kuitetea imani yao . Wamekufa na jina la Yesu katika midomo yao, na ushuhuda wa Roho Mtakatifu.

Papa alimalizia na sala ya kuomba kwa Bwana , neema ya kupokea Roho Mtakatifu , mwenye kutukumbusha mambo yote aliyosema Yesu , na mwenye kutuongoza katika ukweli wote. 








All the contents on this site are copyrighted ©.