2015-05-12 08:30:00

Kilio cha damu ya watu wasiokuwa na hatia! Lindeni haki za wahamiaji!


Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inasitisha mauaji, dhuluma na nyanyaso wanazofanyiwa Wakristo sehemu mbali mbali za dunia sanjari na kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za wahamiaji na wakimbizi. Haya ni mambo msingi ambayo yamejadiliwa kwa pamoja kati ya Baraza la Maaskofu Katoliki Ghana na Baraza la Makanisa Ghana katika mkutano wao uliohitimishwa hivi karibuni, kwani haya ni mambo yanaendelea kuleta wasi wasi na majonzi makubwa kwa wananchi wa Ghana.

Viongozi hawa wa Makanisa wanabainisha kwamba, bado kuna idadi kubwa ya Wakristo wanaoendelea kuuwawa kikatiliki ndani na nje ya Bara la Afrika na waamini wenye misimamo mikali ya kidini sanjari na makundi ya kigaidi. Maaskofu wanawataka waamini wa dini mbali mbali kusitisha mauaji ya watu wasiokuwa na hatia na kuanza mchakato wa ushirikiano miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali ndani na nje ya Ghana kwa ajili ya mafao, ustawi na maendeleo ya wengi. Wananchi wawe macho ili vitendo vya kigaidi vinavyofanywa na Boko Haram na Al Qaida, visipenyezwe nchini mwao, ili wananchi wa Ghana waendelee kuishi katika misingi ya haki, amani, utulivu na maridhiano. Misigano ya kidini, kisiasa na kikabila isipewe mwanya kuwavuruga wananchi wa Ghana

Viongozi wa Makanisa wanasikitishwa na maafa makubwa yanayoendelea kuwakumba wahamiaji na wakimbizi kutoka Barani Afrika, wanaotafuta nafuu ya maisha Barani Ulaya. Wanasema, ni wajibu msingi kwa Serikali Barani Afrika, kuhakikisha kwamba, zinasimama kidete kulinda na kutetea usalama wa maisha ya raia wao, ili kusitisha maafa yanayosimuliwa kila siku na vyombo vya habari ndani na nje ya Bara la Afrika.

Serikali za Kiafrika zihakikishe kwamba, zinaibua mbinu na mikakati itakayosaidia vijana kupata fursa za ajira, ili kudhibiti kishawishi cha kutaka kukimbilia nje ya nchi kwa matumaini ya kupata maisha bora zaidi. Vijana wajifunze uzalendo na kwamba, viongozi mbali mbali waendelee kuwahamasisha vijana kubaki katika nchi zao na kufanya kazi kwa juhudi, bidii na maarifa ili kujipatia mahitaji yao msingi, kwani hakuna njia ya mkato. Vijana wanapaswa kuondokana na ndoto kwamba, maisha mazuri yanapatikana Barani Ulaya na Marekani, jambo ambalo si kweli, hata huko kuna shida na mahangaiko yake.

Viongozi wa Makanisa wanasema, Serikali ya Ghana inapaswa kutambua na kuheshimu mchango wa Makanisa katika sekta ya elimu; dhamana ambayo imeyawezesha Makanisa kuchangia katika malezi na makuzi ya wananchi wa Ghana: kiroho, kimwili, kitaaluma na kimaadili. Serikali ya Ghana kubeza mchango wa Makanisa katika huduma za kijamii ni kukosa moyo wa shukrani, kumbe kuna haja ya kuwa na hati ya makubaliano baina ya pande hizi mbili, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wa Ghana.

Makanisa nchini Ghana yanaonesha wasi wasi kutokana na kuchechemea kwa hifadhi za kijamii, kusua sua kwa huduma za afya zinazotolewa na Serikali pamoja na kuchakaa kwa miundo mbinu ya huduma ya afya. Kanisa limechangia kwa kiasi kikubwa katika utoaji wa huduma katika sekta ya afya. Kumbe, kuna haja kwa Serikali kuimarisha huduma ya afya pamoja na kuendelea kushirikiana na wadau mbali mbali kwa ajili ya mafao ya wananchi wa Ghana.

Uchumi wa Ghana unaendelea kuyumba sana kwani viwanda vingi nchini humo vinaendelea kufungwa na katika kipindi cha miaka mitatu, maendeleo ya viwanda yamedumaa sana, changamoto ya kuibua mbinu mkakati wa kufufua na kuendeleza sekta ya viwanda. Ghana haina budi pia kuwa na sera na mikakati makini itakayoiwezesha Serikali kutumia kikamilifu raslimali na utajiri wa nchi kwa ajili ya mafao ya wengi. Mabadiliko ya Katiba pia hayana budi kuendelezwa, kwa kujikita katika ukweli, uwazi na mafao ya wengi.

Viongozi wa Makanisa wanawataka wananchi wa Ghana kujiandaa kikamilifu kwa ajili ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika nchini humo kunako mwaka 2016. Wanaitaka Tume huru ya uchaguzi nchini Ghana kuhakikisha kwamba, mchakato wa uchaguzi mkuu unakwenda sanjari na mabadiliko yatakayoiwezesha nchi kuwa na Daftari la kudumu la wapiga kura. Viongozi wa Makanisa nchini Ghana wanahitimisha tamko lao la pamoja na kuwataka wananchi kuungana pamoja katika kudumisha misingi ya haki, amani, upendo, umoja na mshikamano wa kitaifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.