2015-05-12 08:10:00

Iweni mashuhuda wa Injili ya Familia na Uhai kwa kuwasaidia maskini!


Baraza la Maaskofu Katoliki Ureno kuanzia tarehe 10 hadi tarehe 17 Mei 2015 linaendesha Juma la kitaifa kwa ajili ya Injili ya Uhai, kwa kuwahamaisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Injili ya Uhai, utu na heshima ya binadamu; kwa kuwajali na kuwahudumia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii pamoja na kukuza tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Kuna haja kwa Familia ya Mungu nchini Ureno kusimama kidete kupambana na utamaduni wa kifo unaokumbatiwa na sera za utoaji mimba na kifo laini; mambo yanayodhalilisha utu na heshima ya binadamu.

Maaskofu wanaitaka Familia ya Mungu nchini Ureno kuhakikisha kwamba, inasimama kidete kulinda na kutetea Injili ya Uhai pamoja na kushuhudia Injili ya Familia. Mafundisho Jamii ya Kanisa yanatoa kipaumbele cha pekee kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na magonjwa na umaskini wa hali na kipato. Watoto wafundishwe kuheshimu na kuthamini Injili ya Uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.

Baraza la Maaskofu Katoliki Ureno linakiri kwamba, katika ulimwengu wa utandwazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, watu wanakabiliana na mahangaiko ya ndani, wanataka kusikia ujumbe wa faraja. Kanisa linaendelea kuhamasishwa na Baba Mtakatifu Francisko kuhakikisha kwamba, linawaendea watu ambao wako pembezoni mwa jamii, ili kuwaonjesha Injili ya Furaha na Matumaini. Katika maadhimisho haya, waamini wanahamasishwa kutafakari, kusali na kusimama kidete kulinda na kutetea Injili ya Uhai. Tarehe 15 Mei, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Familia Kimataifa, fursa makini ya kuendelea kutafakari tunu msingi za maisha ya ndoa na familia

Ni matumaini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Ureno kuwa, kwa kuwahusisha waamini wanajengewa uwezo wa kukabiliana na changamoto za maisha, tayari kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo. Wanasiasa hawana budi kuhakikisha kwamba, wanapanga sera na mikakati ya kiuchumi na kijamii inayozijengea Familia uwezo wa kukabiliana na changamoto za maisha kwa heshima na taadhima.

Maaskofu Katoliki Ureno wanasema kwamba, utamaduni wa kifo unaokumbatiwa na sera za utoaji mimba ni matokeo wakati mwingine ya mashinikizo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa. Wanawake wengi wanaogopa kupata ujauzito kwa kuhofia kukosa fursa ya kazi. Ikumbukwe kwamba, utoaji mimba ni uhalifu dhidi ya ubinadamu, ndiyo maana Mama Kanisa anawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kusimama kidete kulinda na kutetea Injili ya Uhai, dhidi ya Utamaduni wa kifo. Familia inapaswa kupewa adhi yake pamoja na kuthaminiwa, ili kuilinda dhidi ya vitisho mbali mbali.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.