2015-05-12 10:06:00

Expo Milano 2015: Nchi 34 kutoka Afrika zimo ingawa hazivumi!


Onesho la Chakula kimataifa Expo Milano 2015 lililofunguliwa Milano, Mei Mosi, 2015 kwa hotuba ya Baba Mtakatifu Francisko na viongozi wakuu kutoka nchini Italia, linazishirikisha nchi 34 kutoka Barani Afrika. Kwa mara ya kwanza kuna baadhi ya chi za Kiafrika zinashiriki katika onesho hili likiwa na banda lake maalum, ili kunadi sera na mazao yanayopatikana kutoka katika nchi hizi, kama sehemu ya mchakato wa mapambano dhidi ya baa la njaa na utapiamlo wa kutisha duniani.

Watu wengine wamevutiwa sana na umahiri ulioneshwa na Paula Nascimento msanifu wa majengo kutoka Angola, mwenye umri wa miaka 34 aliyechora michoro na kusimamia ujenzi wa banda la onesho la chakula Angola, kwenye Onesho la Expo Milano 2015. Kwa muda wa miaka ishirini, Paula Nascimento ameishi nje ya Angola, lakini baada ya masomo yake, akarejea nchini Angola, tayari kushiriki katika ujenzi wa nchi yake kwa kuchangia elimu, ujuzi na maarifa aliyojipatia akiwa ughaibuni. Huyu ndiye msichana kutoka Afrika ambaye amekuwa ni kivutio kikuu cha banda la onesho kutoka Angola.

Nchi za Nigeria na Angola wameamua kujenga mabanda yao binafsi, wakati ambapo nchi nyingine zinashiriki katika onesho la Expo Milano kwa kushirikiana mabanda na nchi nyingine kadiri ya mazao na tema wanazowasilisha katika onesho hili. Wengi wameshangazwa na Afrika ya Kusini kutoshiriki katika onesho hili, nchi ambayo ina nguvu kiuchumi ndani na nje ya Bara la Afrika.

Expo Milano 2015 ni onesho ambalo linajikita katika mchakato wa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inapambana kufa na kupona ili kutokomeza baa la njaa na utapiamlo wa kutisha duniani, kwa kuhakikisha kwamba, dunia inazalisha chakula,jambo ambalo ni muhimu sana kwa maisha ya mwanadamu. Huu ni mwendelezo wa mchakato wa utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Millenia yaliyobainishwa na Umoja wa Mataifa kunako mwaka 2000.

Expo Milano pamoja na mambo mengine inajumuisha masuala ya: lishe, mazingira, maendeleo endelevu na ustawi wa wananchi; mambo ambayo ni changamoto kubwa kwa Familia ya Mungu Barani Afrika. Kwa miaka mingi Bara la Afrika limekuwa likiwekwa pembezoni mwa mikakati na sera za kimataifa, lakini, mambo kwa sasa yanabadilika kwani Bara la Afrika linaendelea kucharuka katika sera za maendeleo. Ikiwa kama ardhi yenye rutuba Barani Afrika itatumiwa kikamilifu kuzalisha chakula, hapana shaka kwamba, baa la njaa linaweza kupewa kisogo Barani Afrika.

Afrika inachangamotishwa kujifunga kibwebwe kupambana na baa la njaa na utapiamlo kwa kushiriki kikamilifu katika mapambano haya na wala si kama mtazamaji. Kuna nchi ambazo zimeendelea kuwa mstari wa mbele katika tafiti za mazao ya chakula na mafanikio yanaanza kuonekana huko Nigeria, Ghana na Sierra Leone.

Kashfa ya baa la njaa kwa watu millioni 214 kutoka Barani Afrika ni changamoto pevu. Nchi za Kiafrika zisipokuwa makini kwa sera za ardhi, maeneo makubwa ya ardhi yatakwapuliwa na matokeo yake, wakulima wadogo wadogo ambao wanachangia kwa kiasi kikubwa uzalishaji wa mazao ya chakula na kilimo wanaweza kuathirika na hapo kukawa ni mwanzo wa migogoro ya ardhi kati ya wawekezaji na wananchi, kama ambavyo imeanza kujitokeza katika baadhi ya nchi Barani Afrika. Lengo la Jumuiya ya Kimataifa ni kupambana na baa la njaa duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.